2016-06-11 11:08:00

Kanisa katika mapambano dhidi ya baa la njaa na umaskini duniani!


Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu tarehe 13 Juni 2016 anatembelea Makao Makuu ya Shirika la Mpango wa Chakula Duniani, WFP linalotoa huduma ya chakula kwa watu zaidi ya millioni 100 katika nchi 78 wanachama wa Mpango huu. Baba Mtakatifu anakuwa ni kiongozi mkuu wa kwanza wa Kanisa Katoliki kutembelea Makao makuu ya Shirika la Mpango wa Chakula Duniani pamoja na kuzungumza na wajumbe na wafanyakazi pamoja na familia zao.

Akiwa kwenye Makao makuu ya Shirika hili hapa mjini Roma, atasimama na kusali kidogo kwa ajili ya kuwakumbuka na kuwaombea wafanyakazi wa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani waliopoteza maisha yao wakati wakiwa kazini pamoja na kusalimiana na wafanyakazi ambao wamekumbwa na ajali mbali mbali wakati wakitoa huduma. Katika mahojiano maalum na Radio Vatican Monsinyo Fernando Chica Arellano, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Shirika la Mpango wa Chakula Duniani, WFP na Shirika la Kilimo na Chakula, FAO anasema, viongozi wakuu wa Kanisa katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni walipata nafasi ya kutembelea na kuzungumza na wajumbe wa FAO kuanzia na Mwenyeheri Paulo VI, Yohane Paulo II na Papa Mstaafu Benedikto XVI.

Hija ya Baba Mtakatifu Francisko ni muhimu sana kwani ni kielelezo makini cha Kanisa katika mapambano dhidi ya baa la njaa na umaskini duniani, kwa kuhakikisha kwamba, njaa na umaskini vinapewa kisogo kama ilivyobainishwa na Malengo ya Maendeleo Endelevu. Shirika la Mpango wa Chakula Duniani lina jumla ya wafanyakazi 11, 500 wanaotekeleza dhamana na wajibu wao hata wakati mwingine katika mazingira magumu na hatarishi, ili kuhakikisha kwamba, walau watu wanaombana na baa la njaa wanapata chakula. Kwa namna ya pekee, Monsinyo Arellano anakumbuka Haiti na nchi nyingi za Amerika ya Kusini bila kusahau baa la njaa kwa nchi kadhaa Barani Afrika.

Haya ni maeneo ambayo yameathirika kutokana na mabadiliko ya tabianchi. Takwimu zinaonesha kwamba, kuna zaidi ya watu millioni 800 ambao wanadhalilishwa utu na heshima yao kutokana na baa la njaa duniani. Baba Mtakatifu Francisko amekuwa mstari wa mbele kuwahimiza waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kwanza kabisa kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote pamoja na kuwasaidia maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii zao kupambana na baa la njaa na umaskini, kama kielelezo cha imani tendaji, hasa wakati huu Mama Kanisa anapoadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu.

Baba Mtakatifu amekuwa mstari wa mbele kuihamasisha Jumuiya ya Kimataifa kuonesha mshikamano wa dhati kwa waathirika wa vita huko Mashariki ya Kati, waathirika wa Ugonjwa wa Ebola huko Afrika Magharibi pamoja na kuendelea kusimama kidete kupambana na magonjwa, umaskini na baa la njaa. Baba Mtakatifu anawahamasisha waamini, lakini yeye pia yuko mstari wa mbele kwa kuonesha kwa vitendo yale anayosema. Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican wanasema: furaha na matumaini; uchungu na fadhaa ya wanadamu wa nyakati zetu, hususan maskini na wale wote wanaoteseka ni furaha na matumaini; uchungu na fadhaa ya wafuasi wa Kristo pia.

Binadamu wote wanaunda familia moja ya watu wa Mungu na kwamba, maskini ni kiini cha utangazaji na ushuhuda wa Habari Njema ya Wokovu. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, atasaidia walau kuchachusha mshikamano wa huruma na upendo miongoni mwa Jumuiya ya Kimataifa, ili watu waweze kuguswa na mahangaiko ya jirani zao badala ya kudekezwa na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.