2016-06-10 16:01:00

Sakramenti ya Kitubio ni mlango wa huruma ya Mungu!


Leo tutafakari juu ya Sakramenti ya Kitubio kama mlango wa huruma ya Mungu. Sakramenti hii ni Sakramenti inayotuondolea dhambi baada ya Ubatizo wetu. “Wanaoijongea Sakramenti ya Kitubio hupokea kutoka humo huruma ya Mungu ondoleo la kosa lililotendwa dhidi yake, na papo hapo hupatanishwa na Kanisa ambalo dhambi yao imelijeruhi, na ambalo kwa mapendo, mfano na sala huangaikia wokovu wao” (KKK 1422). Hivyo hii ni Sakramenti inayoturudishia tena uzima wa Mungu ambao tunakuwa tumeupoteza kwa dhambi zetu. Ni Sakramenti inayoturejesha nyumbani kwa Baba mithili ya mwana mpotevu kusudi kuendelea kuonja upendo wake na huruma yake.

Katika adhimisho la Jubilei ya Huruma ya Mungu, Baba Mtakatifu Francisko anatuonya juu ya umuhimu wa Sakramenti hii ya kitubio kama njia mahsusi ya kutuunganisha tena na Mungu pale anaposema: “Watu wengi wakiwemo vijana wanarudi kwenye Sakramenti ya Upatanisho, ambao kwa njia hii wanaigundua tena safari ya kumrudia Bwana ili waiishi sala kwa uzito zaidi na kutambua tena maana ya maisha yao. Tunaweka tena kama kiini kwa uhakika sakramenti ya Upatanisho, kwa sababu inamfanya mtu aguse kwa mkono wake ukubwa wa huruma. Kwa kila mfanya toba hii itakuwa chimbuko la Amani ya ndani” (MV 17). Kwa ndani kabisa hapa linaonekana paji la imani kama hatua msingi ya kuijongea vema Sakramenti hii na kufaidika na matunda yake. Mwanadamu anaongea na Muumba wake ndani kabisa nafsini mwake. Roho inazungumza na Roho na kuwekana sawa.

Mtume Paulo anatufafanulia juu ya msingi huo wa kiimani, yaani kuunganika na Mungu pale anaposema “sisi tulimwamini Kristo Yesu ili tuhesabiwe haki kwa imani ya Kristo, wala si kwa matendo ya sheria”. Hapa tunaonywa kuepa kuwa watu wa kutekeleza tu matendo ya kiibada sababu tu ya sheria na taratibu zilizowekwa. Katika moja ya Katekesi zake takribani kama majuma mawili yaliyopita Baba Mtakatifu Fransisko alionya kwamba, katika sala la muhimu si wingi wa sala bali ni namna gani unasali. Muunganiko wetu na Mungu katika utu wetu wa ndani ni hatua ya kwanza inayotufanya kujinyenyekeza mbele yake na kuomba msamaha.

Kuna kasumba mbaya inayoonea leo hii kati ya Wakristo na pengine ni katika kumwelewa vibaya Baba Mtakatifu. Wengi wetu tunajidanganya na kufikiri kwamba Huruma ya Mungu ni kwa njia bwerere tu bila hata ya kufanyia kazi. Sote tumeshuhudia kwa namna moja au nyingine baadhi ya watu walivyoipokea kwa namna potofu waraka wa Baba Mtakatifu “Furaha ya upendo ndani ya familia” “Amoris laetitia” mathalani suala la kushiriki Sakramenti ya Ekaristi Takatifu kwa wale waliotengana na wenzi wao wa ndoa za kikanisa na kufunga ndoa na wengine katika mamlaka za kidunia. Lakini tujiulize je! Ushiriki huo wa Ekaristi Takatifu unatangulizwa tu sababu ya mazoea ya kawaida au ni kwamba mmoja ameguswa na Mungu na imani yake ndiyo inamsukuma kwenda mbele na kuungana na Kristo? Je! Hakuna hatari ya kudai jambo hili katika hali ya mazoea tu huku tukisahau kwamba la kwanza na la muhimu si taratibu bali ni muunganiko wetu na Mungu?

Tunapaswa kufahamu fika kwamba huruma ya Mungu inatudai kufanya kitu; nacho ni mabadiliko ya ndani. Papa Francisko anatuambia kwamba, “Huu ni wakati mwafaka wa kubadili maisha yetu! Huu ni muda ambapo kila mmoja anatakiwa aguswe moyoni. Mbele ya uovu uliotendwa, hata uhalifu mkubwa, ni wakati wa kusikiliza kilio cha watu wasio na hatia wanaodhulumiwa na kunyimwa mali zao, hadhi yao, mapendo, hata na maisha yenyewe. Kubaki katika njia ya uovu ni chemchemi ya kudanganyika na uchungu. Maisha ya kweli ni mengine. Mungu hachoki kunyosha mkono. Yupo tayari daima kusikiliza, hata mimi niko hivyo, kama ilivyo kwa ndugu zangu maaskofu na mapadre. Inatosha kupokea mwito wa wongofu na kwenda mbele ya haki huku Kanisa likitoa msamaha” (MV 19).

Hatua ya kwanza ili kufikia muunganiko huu thabiti na Mungu ni kukubali kuwa umekosa mithili ya Mfalme Daudi katika somo la kwanza. Mfalme Daudi anamwambia Nathani: “Nimemfanyia Bwana dhambi” hapo ndipo Mungu anatenda baada ya kuanzisha huo uhusiano wa toba ndani mwako na anakuambia kupitia huduma ya makuhani wake “Bwana naye ameiondoa dhambi yako; hutakufa”. Mungu wetu anajua yote tuliyoyatenda, hakuna tunaloweza kumficha na wala tusifikiri hata mara moja huo utayari wetu wa kujifunua mbele yake kunamuongezea taarifa fulani juu ya matendo yetu. Mfalme Daudi mwenyewe analikiri hilo katika  Zaburi ya hamsini na moja akisema “Tazama wapendezwa na kweli iliyo moyoni ... usitiri uso wako usitazame dhambi zangu”.

Hatua ya kuwa tayari kujifunua mbele ya Mungu iangusa uhuru wa mwenye dhambi na kumfanya kushiriki kikamilifu kuelekea wongofu. Uhuru huu unapatikana pale tu tunapouelewa ukweli na kuwa tayari kushirikiana na ukweli huo kwa maana “ukweli ndiyo utatuweka huru”. Hatua hii ya kuufikia ukweli inatudai jambo jingine muhimu zaidi la kumpatia Mungu nafasi na kutawala maisha yetu. Hapa unaonekana umuhimu wa fadhila ya unyenyekevu, paji hili la kimungu ambalo litatuongoza kuelewa nafasi yetu mbele ya muumba na hivyo kukiri kwa dhati namna tulivyokurupusha nafasi hiyo adhimu.

Hatua ya pili ni kukuza upendo kwa Mungu. Upendo kwa Mungu unatufanya kumjua yeye zaidi. Upendo wetu unapokuwa basi tunakuwa tayari hata kuona maovu yetu na kuyatubu vema. Ni hatua ya kwenda ndani zaidi katika mahusiano yetu na Mungu. Kristo katika Injili anakiri juu ya yule mwanamke kuwa “Amesamehewa dhambi zake ambazo ni nyingi, kwa kuwa amependa sana”. Mmoja wa waandishi katika Injili ya Marko alikiri vema juu ya umuhimu wa Upendo kwa Mungu na kwa jirani akisema “Mungu ni mmoja, wala hakuna mwingine ila yeye; na kumpenda Yeye kwa moyo wote, na kwa ufahamu wote, na kwa nguvu zote, na kumpenda jirani kama nafsi yako, kwafaa kuliko sadaka nzima ya kuteketezwa na dhabihu zote pia”, jibu ambalo Kristo alilitilia muhuri akisema “Wewe hu mbali na ufalme wa Mungu” (Mk 12: 33 – 34).

Hapa tunagutushwa kuepa kutofungamanisha maisha yetu na sadaka tunayomtolea Mungu. Wengi tunaweza kuingia katika kishawishi cha kujidai tunatimiza sadaka au kufanya matendo fulani fulani ya kisheria lakini mapendo yetu kwa Mungu na jirani ni aghalabu kushuhudiwa. Tunakuwa na maisha ya mchanganyo ambayo kwenye maovu ya kidunia tunaonekana na bado katika ibada tunaonekana. Upendo kwa Mungu unatupeleka katika utayari wa kuzifuata njia zake. Neno upendo halipingani na utii. Huwezi kamwe kutii halafu usipende au kupenda kisha usitii. Upendo unamaanisha kuunganika na nafsi yake unayempenda na unanuia kumtendea mema yule unayempenda. Sakramenti ya Kitubio inapoambatana na upendo thabiti kwa Mungu, upendo ambao unatufungulia huruma yake, inadhihirisha utayari wetu wa kuungana naye na kuionja huruma yake.

Hivyo tunakumbushwa katika Dominika hii juu ya hatua hizo mbili muhimu kwa Sakramenti ya kitubio, yaani utayari wa kujifunua mbele ya Mungu na pili kudhihirisha upendo wetu wa dhati kwake. Hapa ndipo tunaweza kweli kuunganika naye ndani kabisa katika nafsi zetu na kuepuka hatari ya kuijongea huruma yake katika Sakramenti ya Kitubio katika hali ya kufuata sheria tu na si katika hali ya kutupatia uongofu wa kweli na kuimarika kiroho.

Kutoka Studio za Radio Vatican mimi ni Padre Joseph Peter Mosha, Tumsifu Yesu Kristo, Laudetur Iesus Christus!








All the contents on this site are copyrighted ©.