2016-06-09 14:50:00

Filamu bubu iliyokuna sakafu ya mioyo ya watu!


Kuna filamu moja ilishutiwa katika nyumba ya Watawa Wakartusi huko Ufaransa mwaka 2005 inaitwa: Le grand silence au Unyamavu Mkuu tungeweza kuiita: Filamu Bubu. Filamu hiyo inaonesha maisha ya watawa hao wa maisha ya kujifungia ndani wanaowasiliana kimyakimya kwa matendo na ishara tu bila kutoa sauti. Mahali pekee unapoweza kuzisikia sauti zao ni kanisani wanaposali pamoja. Filamu hiyo imepata umaarufu na mvuto wa pekee kutokana na mafundisho mazito ya maisha ya ukimya ya watawa hao. Ama kweli  “Matendo yana nguvu zaidi kuliko maneno” au “Kimya kingi kina mshindo mkubwa.”

Leo tutaiona filamu bubu ya namna yake itakayomkuna kila mmoja wetu kwa namna yake na kumtafakarisha katika maisha. Ni Mwinjili Luka pekee yake kati ya Wainjili wote ndiye aliyeishuti hiyo Move. Mazingira yalikuwa hivi, “Mfarisayo mmoja alimwalika Yesu kwenda kwake kula chakula cha jioni,” Yaonekana ilikuwa siku ya Jumamosi yaani Sabato. Kwa kawaida siku hiyo Waisraeli wanaenda kwenye Sinagogi au Kanisani kusali na jioni kuliandaliwa chakula cha pekee kama wanavyoandaa wakristu siko ya Jumapili. Siku hiyo baba wa familia aliweza kumwalika mtu mmoja kuja kutoa neno na maelezo ya Maandiko Matakatifu yaliyosomwa siku hiyo kwenye Sinagogi.

Walialikwa pia watu wenye heshima, na nyadhifa katika jamii, kama vile viongozi wanaoshika vizuri dini pamoja na sheria za Tora nk. Aidha mlo ulifanyika barazani penye nafasi nzuri na mlango uliachwa wazi kusudi wapita njia waweze kusalimia na  hata kusifia madikodiko yaliyoandaliwa bila kuingia ndani. Hawa walishibishwa kwa harufu nzuri ya  maakuli, sawa na kula ugali kwa picha ya samaki! Yaani hapa sipati picha kabisaaaa!

Katika mazingira kama hayo, kwa ghafla akaja mpita njia, mzamiaji wengine wanawaita watu kama hawa “gatecrashers” naye ni “mwanamke mmoja wa mji ule,” na mji unaosemwa hapa nadhani ni ule wa Nain ambao Yesu alimfufua mwana wa mama mjane tuliyemsikia wiki iliyopita. Aidha tunaambiwa kuwa “mwanamke huyo alikuwa mwenye dhambi.” Hapa hatajwi jina lakini wengi wanamhusisha na Magdalena. Nadhani kwa sababu mwisho ya Injili ya leo unakuta katika kundi la wanawake wanaofuatana na Yesu anatajwa Magdalena ambaye Yesu alimtoa pepo saba. Maana yake Magdalena huyu alikuwa mgonjwa wa kupagawa mashetani na akaponywa kama wagonjwa wengine waliokuwa hapo. Kwa hiyo Magdalena huyo alikuwa mgonjwa na hakuwa mtenda dhambi, na hivi hana uhusiano wowote na mwanamke huyu mdhambi asiyetajwa jina katika Injili ya leo ili kuhifadhi utu na heshima ya heshima yake, kwa kumwinua ili aweze kuonja huruma na upendo wa Mungu katika maisha yake.

Hebu tumwache kabisa Magdalena atulie na “kula shavu” baada ya kuponywa mapepo yake, sisi tuendelee na mwanamke huyu mwenye dhambi asiye na jina.“Mwanamke huyo alipopata habari ya kuwa Yesu ameketi chakulani katika nyumba ya yule Farisayo, akajitosa humo na chupa ya marimari yenye marhamu.” Yaani, chupa kizuri chenye parfyumu. Kulikoni! Wengine wanasema si bure, alifika kuungama dhambi. Kama ndivyo mbona hatusikii neno la kuomba msamaha kutoka kwa mwanamke huyu. Yaonekana mwanamke huyu alikuwa na yake moyoni. Mambo yaliyojaa moyoni mwa mwanamke huyu yanaweza tu kuelezeka kwa mfano hai ufuatao.

Kulikuwa na wanawake wanne hivi walichaguliwa kupeleka vipaji altareni wakati wa Misa ya Kipaimara iliyoongozwa na Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa pili huko Songea-Tanzania. Hao wamama baada ya kukabidhi vipaji na kupeana mikono na Baba mtakatifu, mara wakajiangusha chini na kuanza kugaagaa.  Kadiri ya utamaduni wa kingoni kitendo hicho kinaitwa ‘kugarawuka’ nacho kilifanyika kimyakimya huku wakitoka machozi bila kulia kwa sauti. Kisha wakainuka na kupiga vigelegele vya furaha na kuondoka. Wamama hawa walijisikia kubahatika sana kumshika mkono Halifa wa Petro wakabaki kujieleza bila maneno bali kwa matendo, furaha iliyojaa mioyoni mwao. Walijisikia kama Elizabeti alipotembelewa na Maria, na kusema: “Ne na yani!” yaani “Mimi ni nani hata Mama ya Bwana wangu anitembelee.”

Kadhalika kwa mwanamke huyu mdhambi. Dhambi maana yake ni kuvunja mahusiano na Mungu pamoja na jirani; ni kwenda njia potovu inayokupeleka kwenye maumivu na uchungu, kumbe msamaha ni kuacha njia hiyo na kwenda njia yenye kukuletea furaha. Mwanamke huyu alijisikia kusamehewa dhambi yaani, kumfahamu Yesu aliyemwonyesha njia ya kweli ya kufuata, akajifahamu kwamba njia aliyokuwa anaifuata kabla ilikuwa inampeleka kubaya, haikuwa inampeleka kwenye furaha ya kweli. Sasa yuko katika njia sawa yaani anaweza kumfuata Yesu aliye njia ukweli na uzima. Kwa hiyo mwanamke huyu hauingia mle barazani kuungama dhambi, bali alienda kujieleza furaha iliyokuwa fuadini pake kutokana na makuu aliyoishatendewa.

Mle barazani, Yesu alikuwa amekaa mkao wa kujilegeza kwenye kiti cha uvivu kadiri ya desturi ya Wayahudi wakati wa kula. Yule mwanamke akaingia barazani kimyakimya bila kusema neno, anaenda moja kwa moja hadi miguuni kwa Yesu. Ili kuifikia miguu kwa vyovyote ilimbidi kupiga magoti. Tendo hili alilifanya pia Yesu alipowaosha miguu mitume katika karamu ya mwisho likimaanisha utumishi. Aidha, miguu ni alama ya safari ya Bwana arusi aendaye mbali kumtafuta bi arusi wake. Kwa hiyo bi arusi anapogundua upendo wa Bwana arusi aliyesafiri toka mbali kumfuata, hapo atapiga magoti, kuikumbatia na kuibusu.

Baada ya kupiga tu magoti unaoiona lugha ya viungo vinne vya mwili wake yaani macho, mikono, nywele na midomo, jinsi vinavyozungumza kimyamya na miguu ya Yesu. Mosi, lugha ya macho ni kulia machozi kama unavyoona:“akilia, akaanza kumdondoshea miguu machozi yake” Wengine wamefasiri tendo hili kuwa ni la majuto na kuomba msamaha kwa Yesu. La hasha, kama tulivyosema, mwanamke huyu alishasamehewa na sasa amegundua thamani ya maisha yake katika Kristo. Kwa hiyo haya ni machozi ya furaha. Pili lugha ya mikono ambayo ni kupaka mafuta miguu na kupangusa machozi kwa nywele. Tatu lugha ya nywele waswahili wanasema mwanamke nywele bwana! Nywele zinatumika kufutafuta machozi aliyodondosha kwenye magoti. Nywele zina thamani kubwa sana ya uzuri na ushawishi kwa mwanamke. Kwa kawaida nywele husukwa au hufungwa ushungi, au hufunikwa hijabu. Nywele hufumuliwa na kichwa huachwa wazi mbele ya mume mtu wake tu. Kutokana na uthamani wa nywele kama sehemu ya siha na uzuri kwa mwanamke Pauli anasema: “Kila mwanamke asalipo, au anapohutubu bila kufunika kichwa, yuaaibisha kichwa chake; Mwanamke asipofunikwa na akatwe nywele.” (IKor 11:5-6). Kadhalika: “Wanawake na wajipambe kwa mavazi ya kujisitiri, pamoja na adabu nzuri, na moyo wa kiasi; si kwa kusuka nywele.” (I Tim 2:9-10).

Nne, lugha ya midomo ni kubusubusu sana miguu kwa mfululizo kama anavyothibitisha Yesu mwenyewe anapomwambia Simoni:“Wewe hukunibusu; lakini huyu tangu nilipoingia hakuacha kunibusu sana miguu yangu.” Kubusu ni alama ya kujitoa na kujiaminisha moja kwa moja kwa yule anayekupenda na unayempenda. Kisha “akaipaka miguu ile kwa yale marhamu.” Kwa kawaida watu wanajipaka marashi na kujikung’utia parfyumu wanapoenda kwenye dhifa. Harufu ya parfyumu ni alama ya upendo wa dhati. Tena harufu ile ilijaza nyumba nzima. Kwa hiyo yabidi upendo wa Wakristu unukie vizuri na uenee katika jumuia nzima. Ama kweli mwanamke huyu aliingia kujieleza furaha yake. Yesu akaridhia na kumwacha bila kumdhalilisha.

Mbele ya watu wenye heshima zao na wakereketwa wa dini kama yule Mfarisayo filamu hii ilitakiwa ipigwe marufuku kwa vile imejaa makwazo kama tunavyoona kwamba. “Yule Farisayo aliyemwalika alipoona vile akakwazika.” Kwa vyovyote Mfarisayo huyu alikuwa mtu wa haki, mtu wa dini, mkarimu lakini kilichomwuma ni kwamba hata mafarisayo wenzake wasingeridhika kuona kituko kitendo kile kinafanyika ndani ya nyumba yake. Jinsi alivyomheshimu Yesu alitamani sana kumtetea lakini alishindwa afanyeje, basi akishia kuwaza tu moyoni kwamba: “Mtu huyu kama angekuwa nabii, angemtambua mwanamke huyu amgusaye, ni nani, naye ni wa namna gani, ya kwamba ni mwenye dhambi.”

Kumbe, Yesu aligundua mapema mawazo ya mfarisayo yule kwa sababu anaitambua dhambi inaanza ndani ya moyo. Ndiyo maana alisema ni budi kuizima dhambi toka mbali, kama vile jicho lako likimtazama mwanamke kwa tamaa uling’oe. Yesu kwa upande wake alikuwa safi moyoni, na hivi hakuwa na shida yoyote kumwacha mwanamke huyu ambusu na kumpapasa miguu yake. Kumbe mfarisayo alikwazika kwa vile hakuwa safi moyoni mwake. Hapa tujihoji hali zetu wenyewe tunapoonesha vidole wengine. Kwa hiyo Yesu anaona atoe tafsiri ya hiimuvi iliyoshuhudiwa. Anamwita mfarisayo kwa jina: “Simoni,” Kuitwa kwa jina ni mwito, kama vile alivyomwita  Simoni Petro, Yuda, Martha, Zakayo Ni mwito wa kwenda njia sahihi. Hata wewe mkristo umeitwa na Yesu kwa jina. Baada ya kumwita anamtonya: “Simoni nina neno nitakalo kukuambia.” Ili kumtambulisha njia potovu anayoifuata, anamtolea mfano wa watu waliokuwa na madeni. Yule anayetambua kuwa amesamehewa zaidi huyo anapenda bure na zaidi, lakini yule aliyesamehewa kidogo au hajisikii kusamehewa na kujidhani yuko katika njia sawasawa, huyo hawezi kupenda bure bila malipo. Mungu anatupenda bure bila malipo na mtu mwenye fikra kama mfarisayo hawezi kupenda. Kumbe, njia sawa ni kupenda bila mipaka na ubaguzi.

Lengo la Yesu ni kutuonesha kasoro ya Mfarisayo, na kutufunulia wingi wa upendo alio nao mwanamke yule aliyesamehewa bure na anapenda bure. Mfarisayo anahukumu wengine na kuwalaumu kwa sababu anajiona mwenye haki na kustahili kupendwa na Mungu. Hivi ndivyo tufanyavyo sisi. Tunaweza kuwa tunafanya mambo vizuri lakini kasoro yetu daima ni kuhukumu wengine. Tunaalikwa kutafiti dhamiri zetu kama tunaye Simoni mioyoni mwetu au mwanamke yule mdhambi aliyesamehewa. Upendo wa Mungu ni wa bure na hauna masherti, na yabidi kutangaza upendo huo wa bure wa Mungu ili wote wajifunze kuuishi.

Na Padre Alcuin Nyirenda, OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.