2016-06-09 11:47:00

Askofu mteule Flavian Matindi Kassala: Hongera, Pole na Karibu!


Familia ya Mungu Jimbo Katoliki Geita, Tanzania inaendelea kukamilisha mapokezi ya kishindo ya Askofu mteule Flavian Matindi Kassala, Jumamosi tarehe 11 Juni 2016. Ratiba inaonesha kwamba, Askofu mteule atapokelewa majira ya saa 3:00 asubuhi kwenye kivuko cha Busisi na baadaye kuelekea Parokia ya Nyampande na kupitia Parokia ya Sengerema mjini, huko atasali na kutoa baraka zake za kichungaji. Akiwa kwenye Parokia teule ya Shulabela, Askofu mteule ataweka jiwe la msingi. Baada ya chakula cha mchana Parokiani Kasamwa ataelekea Parokia ya Geita atasalimiana na familia ya Mungu kwenye Parokia ya Bikira Maria Afya ya wagonjwa na baadaye jioni kuadhimisha Ibada ya Masifu na hapo atakabidhiwa ufunguo wa Kanisa kuu la Bikira Maria Malkia wa amani.

Katika mahojiano maalum na Radio Vatican, Askofu Agapito Ndorobo wa Jimbo Katoliki Mahenge anawaalika waamini na watu wite wenye mapenzi mema kumpokea na kumpatia ushirikiano wa dhati Askofu mteule Flavian Matindi Kassala katika utume wake wa kufundisha, kuongoza na kuwafundisha watu wa Mungu. Kwa Askofu mteule Kassala anamwambia: Hongera, Pole na Karibu!

Askofu mteule Flavian Matindi Kassala aliyeteuliwa hivi karibuni na Baba Mtakatifu Francisko kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki Geita, anatarajiwa kusimikwa rasmi tarehe 12 Juni 2016 Jimboni Geita, tukio ambalo ni la kukata na shoka, baada ya familia ya Mungu nchini Tanzania kuadhimisha Kongamano la Ekaristi Takatifu Kitaifa huko Jimbo kuu la Mwanza kuanzia tarehe 8 hadi 12 Juni 2016. Itakumbukwa kwamba, Askofu mteule Kassala hapo tarehe 16 Mei 2016, kwenye Makao makuu ya Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu mjini Roma alikiri Kanuni ya Imani na kula kiapo cha utii, wakati atakapokuwa anatekeleza dhamana yake ya kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu Jimbo Katoliki Geita.

Kabla ya uteuzi huu, Askofu mteule Kassala alikuwa ni mkurugenzi wa Kitivo cha Stella Maris, Mtwara, Chuo kikuu cha Mtakatifu Agostino cha Tanzania. Askofu mteule Kassala alizaliwa tarehe 4 Desemba 1967, Parokia ya Sumve, Jimbo kuu la Mwanza. Alipata masomo yake ya Sekondari kutoka Seminari Ndogo ya Mtakatifu Pio wa X, iliyoko Makoko, Jimbo Katoliki la Musoma.

Alijiendeleza zaidi kwenye Seminari Ndogo ya Sanu Jimbo Katoliki Mbulu. Akapata majiundo ya falsafa kutoka Seminari ya Mtakatifu Anthony wa Padua, Maarufu kama Ntungamo, iliyoko Jimbo Katoliki la Bukoba. Askofu mteule Kassala alijipatia majiundo yake ya kitaalimungu kwenye Seminari kuu ya Mtakatifu Paulo, maarufu kama Kipalapala iliyoko Jimbo kuu la Tabora. Baada ya safari hii ndefu katika maisha na wito wa kipadre, akapewa Daraja Takatifu la Upadre hapo tarehe 11 Julai 1999 kama Padre wa Jimbo Katoliki Geita.

Baada ya Upadrisho kati ya mwaka 1999 hadi mwaka 2002 alikuwa ni Paroko usu, Parokia ya Sengerema, Jimbo Katoliki la Geita. Mwaka 2002- 2004 alikuwa ni mlezi na Padre wa maisha ya kiroho Seminari ndogo ya Bikira Maria Malkia wa Mitume, Jimbo Katoliki Geita pamoja na kuwa ni Mkurugenzi wa Jimbo Mashirika ya Kimissionari ya Kipapa.

Askofu mteule Flavian Kassala kuanzia mwaka 2004 hadi mwaka 2012 alitumwa na Jimbo kujiendeleza zaidi katika utume wa vijana na katekesi katika Chuo Kikuu cha Kipapa cha Wasalesiani, kilichoko mjini Roma na hapo akajipatia shahada ya nguvu ya uzamivu. Akiwa mjini Roma kwa miaka kadhaa alishiriki kuandaa makala ya vijana Radio Vatican, makala zilizokuwa zinagusa maisha na changamoto za vijana wa kizazi kipya.

Kunako mwaka 2013 Askofu mteule Kassala akarejea Jimboni Geita na huko akapewa dhamana ya kuratibu miradi ya Jimbo. Kuanzia mwaka 2013- 2015 akepewa dhamana ya kusimamia na kufundisha Chuo Kikuu cha SAUT, Kitivo cha Utalii, Arusha. Kunako mwaka 2015, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania likamhamishia Kitivo cha Stella Maris, Mtwara kama mkurugenzi. Itakumbuka kwamba, Jimbo Katoliki Geita limekuwa wazi kuanzia tarehe 14 Machi 2014, baada ya Baba Mtakatifu Francisko kumhamisha na kumpandisha hadhi Askofu Damian Dallu kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Songea.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.