2016-06-08 15:08:00

Kongamano la Ekaristi Kitaifa Mwanza: Ndoa na Ekaristi


Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wake wa kitume “Furaha ya Upendo ndani ya familia” “Amoris Laetitia” anapembua kwa kina na mapana utume wa familia katika mwanga wa angavu wa Neno la Mungu; anagusia ukweli na changamoto za kifamilia; mwelekeo wa Yesu katika wito na maisha ya kifamilia; umuhimu wa upendo ndani ya familia kadiri unavyobainishwa na Mtakatifu Paulo kuhusu utenzi wa upendo. Baba Mtakatifu katika wosia huu anaangalia upendo kama asili ya maisha; anatoa mapendekezo katika shughuli za kichungaji; umuhimu wa kuimarisha elimu kwa watoto; dhamana ya kuwasindikiza, kung’amua na kuishirikisha familia dhaifu katika maisha na utume wa Kanisa na mwishoni, Baba Mtakatifu anafafanua tasaufi ya ndoa na familia katika mapana yake.

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania tarehe 8 Juni 2016 limeanza maadhimisho ya Kongamano la tatu la Ekaristi Takatifu Kitaifa, huko Jimbo kuu la Mwanza. Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania katika mahojiano maalum na Radio Vatican anabainisha uhusiano uliopo kati ya Sakramenti ya Ndoa na Ekaristi Takatifu katika maisha ya waamini. Anasema, Sakramenti ya Ndoa ni mfano na kielelezo cha upendo na uaminifu wa Kristo Yesu kwa mchumba wake Kanisa.

Huu ni upendo endelevu unaojikita katika uvumilivu na uaminifu, changamoto kwa waamini kuambata tunu hizi msingi katika maisha ya ndoa na familia. Wanandoa wanaofarakana na hatimaye kuamua kuoa au kuolewa wanakosa sifa za kushiriki Ekaristi Takatifu, ingawa wanapaswa kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa.

Ikumbukwe kwamba, “Ekaristi Takatifu si zawadi kwa watakatifu, bali masufuru ya njiani kwa wanyonge na maskini”. Ekaristi Takatifu ni mfano, sadaka na majitoleo ya Kristo kwa Kanisa lake, mwaliko kwa wana ndoa na familia kushirikishana tunu hizi katika hija ya maisha yao ya kila siku.

Askofu Ngalalekumtwa anakaza kusema, Kanisa litaendelea kuonesha moyo wa huruma na mapendo kwa kutambua kwamba, huruma ni msingi thabiti wa uhai wa Kanisa. Shughuli zote za kichungaji zinapaswa kufungamanishwa katika upole unaoshuhudiwa kwa waamini na kwamba, umahiri wa Kanisa unajionesha kwa namna ya pekee katika huruma na upendo, mada inayofafanua kwa kina na mapana na Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu.

Huruma na upendo huu unaziambata familia ambazo zinakabiliwa na mgogoro wa imani. Kumbe, wachungaji wanapaswa kuwaheshimu, kuwathamini na kuwasaidia kikamilifu. Askofu Ngalalekumtwa anasema upendo huu unapaswa kushuhudiwa kwa kuwapokea na kujenga utamaduni wa kusikiliza na kusikilizana; kuheshimiana na kuthaminiana. Upendo pia unajikita katika kweli za kiimani ambazo zinapaswa kushuhudiwa kikamilifu pamoja na kukosoana katika chumba cha upendo.

Viongozi wa Kanisa wasiwe na majibu ya haraka kwa wandoa wanaoogelea katika migogoro na kinzani za maisha ya ndoa na familia, wajitahidi kuvuta subira, kwani ukweli utawaweka huru! Anasisitiza Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa ambaye ameshiriki katika maadhimisho ya Sinodi mbili za Maaskofu kuhusu utume wa familia ziliozoadhimishwa kunako mwaka 2014/2015.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.