2016-06-07 11:15:00

Kenya: Chagueni viongozi waadilifu na wachapakazi!


Askofu Emmanuel Barbara wa Jimbo Katoliki Malindi Kenya katika mahojiano maalum na “Gazeti la Mirror” linalomilikiwa na Kanisa Katoliki nchini Kenya amewataka wanasiasa kuachana na ukabila usiokuwa na mashiko; uchoyo na ubinafsi na badala yake kujielekeza zaidi katika misingi ya umoja wa kitaifa, haki, ustawi na maendeleo ya wananchi wote wa Kenya.

Askofu Barbara anawahimiza wananchi wote wa Kenya kuwachagua viongozi waadilifu, wakweli na wawazi; watu wanaoweza kujisadaka kwa ajili ya maendeleo ya wananchi wote wa Kenya wakati wa uchaguzi mkuu, unaotarajiwa kufanyika nchini Kenya kunako mwaka 2017. Familia ya Mungu inawahitaji viongozi wanaojipambanua kwa kutafuta na kusimamia mafao ya wengi kwani haitoshi kusema “Sisi watu wa Kenya”, wakati ambapo mawazo na akili zao, wanazielekezwa kwingine kabisa!

Askofu Barbara anawataka wananchi wote wa Kenya kuondokana na vitendo vya uvunjifu wa misingi ya haki, amani na utulivu pamoja na kuachana na ukabila usiokuwa na mashiko wala mvuto kwa ustawi na maendeleo ya Kenya, wakati huu Kenya inapoendelea kukaribia uchaguzi mkuu, ambamo hadi sasa kumeanza kujitokeza vitimbwi kadhaa! Familia ya Mungu nchini Kenya isaidie mchakato wa ujenzi wa Kenya iliyo bora zaidi, kwa kuwajibika barabara kama raia wema.

Askofu Barbara ameishauri Serikali ya Kenya kuwashirikisha viongozi wa dini katika maamuzi makubwa hata kama wakati mwingine wanaweza kuwa na mawazo tofauti, lakini daima ni kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wananchi wengi wa Kenya. Amesema, Kanisa Katoliki nchini Kenya ni mdau mkubwa wa maendeleo katika sekta ya elimu, afya na ustawi wa jamii. Pande hizi mbili zikishirikiana kwa dhati, malengo makubwa yanaweza kufikiwa kwa kuzingatia mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili; ustawi na maendeleo ya wengi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.