2016-06-06 10:10:00

Deni la Taifa ni zigo lisilokwepeka!


Serikali ya Tanzania imesema imeendelea kusimamia Deni la Taifa kwa kuzingatiasheria ya mikopo, dhamana na misada sura 134 ambapo kwa mwaka 2015/16, serikali ilitenga Sh. bilioni 504.57 kwa ajili ya kulipa riba ya deni la nje. Pia imeweka msisitizo umewekwa kukopa mikopo yenye masharti nafuu ambayo inakopwa kwa uangalifu na kutumika kwenye miradi yenye vichocheo vya ukuaji wa uchumi, ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya barabara, reli, ujenzi wa mitambo ya kufufua umeme na ujenzi wa viwanja vya ndege.

Hayo yalielezwa bungeni hivi karibuni mjini Dodoma na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philipo Mpango, wakati akiwasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2016/17. Alisema, kwa mwaka wa 2015/16, serikali ilitenga Sh. bilioni 504.57 kwa ajili ya kulipa riba ya deni la nje.ikali ilitenga Sh.899.89 kwa ajili ya kulipa riba ya deni la ndani. “Hadi Machi, 2016 Sh. bilioni 414.66 sawa na asilimia 82 zilitumika kwa ajili hiyo,”alisema.

Dk. Mpango alisema, hadi Machi, 2016 Sh. bilioni 547.88 sawa na asilimia 61 zilitumika kwa ajili hiyo. Alisema, kwa mwaka wa fedha 2015/16 serikali ilitenga pia Sh. bilioni 421.20 kwa ajili ya kulipa mtaji wa deni la nje. Waziri huyo alieleza kuwa hadi Machi, 2016 Sh. bilioni 395.90 sawa na asilimia 94 zilitumika kwa ajili hiyo. Pia alisema, serikali ilitenga Sh. trilioni 2.7 kwa ajili ya kulipa mtaji wa deni la ndani, na hadi kufikia Machi, 2016 Sh. trilioni 1.86 sawa na asilimia 69 zilitumika kwa ajili hiyo.

Alisema, katika jukumu la usimamizi wa mali ya serikali, Wizara hiyo imefanya uthamini wa ardhi, majengo mali nyingine za serikali ambapo taasisi kumi zinaendelea kufanyiwa uthamini, kuondosha mali chakabu katika wizara na Idara za serikali. Dk. Mpango, aliainisha kuwa katika kutekeleza hilo jumla ya Sh. bilioni 2.06 zilikusanywa kutokana na mauzo ya magari na vifaa chakavu na vibali vya uondoshaji wa mali chakavu vilivyokuwa na thamani ya Sh. bilioni 1.68 vilitolewa kwa mamlaka na taasisi mbalimbali za serikali.

Alisema, kati mwaka 2015/16 Wizara imepitia sheria ya ununuzi wa umma Na.7 ya mwaka 2011 na kupendekeza marekebisho ya sheria hiyo. “Kukamilisha uandaaji wa Sera ya Taifa ya Ununuzi wa Umma na mkakati wa utekelezaji wake kuanza kutekeleza mpango wa mahitaji ya mafunzo wa maafisa ununuzi na ugavi kwa kuwajengea uwezo wa namna ya kupunguza vihatarishi katika ununuzi wa umma,”  alisema. Alifafanua kwamba kuhakiki taarifa za maafisa ununuzi na ugavi na kuziweka katika daftari la maafisa ununuzi na ugavi serikalini pamoja na kukamilisha maandalizi ya kufanya thathminiya ufanisi wa mfumo wa ununuzi wa umma nchini Tanzania.

Sambamba na hilo alisema, katika usimamizi wa ununuzi wa Umma imefanya uchunguzi katika zabuni 26 zinazohusu manunuzi yaliyofanywa taarifa za uchunguzi wa zabuni 18 zimekamilikana kuwasilishwa kwenye mamlaka husika, na zabuni 8 zilizobaki bado zinaendelea. Wizara imefanya ukaguzi wa taratibu za utoaji wa zabuni na utekelezaji wa miradi na mikataba itokanayo na ununuzi wa umma kwa taasisi 126, zikiwemo wizara na Idara zinazojitegemea 23, mashirika ya umma 36 na serikali za mitaa 67. Alisema, ukaguzi huu umehusisha jumla ya mikataba 5,206 yenye thamani ya Sh. bilioni 420.01. “Maeneo yaliyobainika kuwa na upungufu kwa ukaguzi uliofantika ni katika usimamizi wa mikataba, utunzaji wa nyaraka, utumiaji wa mfumo wa uwasilishaji wa taarifa za ununuzi kwa njia ya kielekroniki pamoja na kushuhulikia malalamiko ya wazabuni,” alisema.

Alisema, wizara imefanya kaguzi katika miradi ya ujenzi 385 inayotekelezwa na taasisi 126, miradi hiyo imejumuishwa barabara, madaraja, majengo, ukarabati wa reli, ununuzi wa vifaa pamoja na huduma za washauri waelekezi. Pia alisema , katika mwaka wa 2016/17 wizara imepanga kuendelea kutoa udhamini wa masomo kwa wahasibu, wagavi na wataalamu wa kompyuta kutoka serikali kuu na mfumo wa TISS katika halmashauri zipatazo 58 zilizopo katika Mikoa ya Dar es Salaam, Mbeya, Mwanza, Arusha, Tanga Morogoro na Dodoma.

Alisema, wizara imepanga kuunganisha mfumo wa malipo wa EFT katika wizara ya Fedha na Mipango, afya na ustawi wa Jamii na Wizara ya Fedha na Mipango, Afya na Ustawi wa Jamii na Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi. Alisema lengo ni, kuunganisha mfumo wa uwasilishaji mapato wa Mamlaka ya mapato Tanzania-Tanzania ‘Revenue Gateway System (RGS)’ na mfumo wa Hazina ‘Treasury Revenue Accounting System’ kwa lengo la kupata taarifa za mapato ya kodi kutoka TRA kielektoniki. Aidha , bunge lilikubali kuidhinisha jumla ya Sh. trilioni 8.7 kwa ajili ya wizara hiyo kwa mwaka 2016/17.

Wakati huo huo, Kamati ya Bajeti imesema kuwa moja ya eneo ambalo Serikali ina changamoto kubwa ya kulitatua ni eneo linalohusu madeni ya mifuko ya jamii ambayo kwa pamoja inadai Serikali zaidi ya Sh 6 trilioni. Akiwasilisha taarifa ya kamati hiyo makamu mwenyekiti Josephat Kandege alisema, pamoja na kuwa Serikali ilionyesha nia njema ya kulipa madeni hayo likiwemo kubwa la PSPF bado utekelezaji wake umekuwa wa kusuasua. “Mfano kwa mwaka wa fedha 2015/16, Serikali iliahidi kutoa kiasi cha Sh 150 bilioni pamoja na kutoa Non Cash Bond ya Sh 2.6 trilioni ili kulipa deni la PSPF lakini hadi sasa ni Sh 83 bilioni tu zilizotolewa na hakuna Non Cash Bond yoyote iliyotolewa,”alisema Kandege.

Alisema kuwa kamati inaona madeni hayo ni tishio kubwa linaloathiri utekelezaji wa majukumu ya mifuko husika hasa ulipaji wa pensheni ya wastaafu wanaongezeka kila mwaka. “Pamoja na kwamba kwa mwaka huu Serikali imetenga kiasi cha Sh 157 bilioni kulipa malimbikizo ya deni hilo, kamati inaitaka Serikali kuongeza kasi ya ulipaji madeni ya mifuko ya jamii pamoja na kutumiza ahadi yake ya kutoa Non Cash Bond ya Sh 2.6 trilioni kwa mfuko wa PSPF ili uweze kupunguza mzigo mkubwa wa malipo y awastaafu,”alisema Kandege.

Kwa mujibu wa hotuba ya upinzani ambayo iliwasilishwa bungeni na msemaji wa wizara hiyo David Silinde lakini hakuisoma wameeleza kuwa Serikali inatumia fedha nyingi kulipa madeni badala ya kuzitumia fedha hizo kugharamia miradi ya maendeleo. “Tutarajie deni hili kuongezeka kwa kiwango kikubwa kwa kuwa mwaka huu pekee tunatarajia kukopa mkopo wa biashara (wa ndani na nje) wenye thamani ya Sh 7.4 trilioni,” alisema Silinde. Alisema kuwa Kitabu cha Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2016/17 kinaeleza kuwa hadi kufikia Januari, 2016 deni hilo limefikia Sh 42.9 trilioni na kwa nyongeza ya Sh 7.4 trilioni kwa mwaka ujao wa fedha deni hilo litafikia Sh 48 trilioni.

Na mwandishi maalum kutoka Dodoma.








All the contents on this site are copyrighted ©.