2016-06-05 11:46:00

Watakatifu wapya ni mashuhuda wa Fumbo la Ufufuko!


Liturujia ya Neno la Mungu, Jumapili ya 10 ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa inaonesha kiini cha imani ya Kanisa, yaani ushindi wa Mungu dhidi uchungu na kifo. Injili inaonesha matumaini yanayobubujika kutoka katika Fumbo la Pasaka ambalo kwalo Kristo Yesu anashuhudia na kufunua Uso wa huruma ya Mungu unaowafariji wale wanaoteseka na kuvunjika moyo, changamoto kwa waamini kuendelea kuambatana na Kristo Yesu, ili aweze kuwaonesha nguvu ya Fumbo la Ufufuko.

Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko kwenye Ibada ya Misa Takatifu ya kuwatangaza Wenyeheri Stanislaus wa Yesu na Maria pamoja na Sr. Maria Elizabeth Hesselblad kuwa watakatifu, Jumapili tarehe 5 Juni 2016 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Katika mateso ya Kristo, Mwenyezi Mungu anaonesha umuhimu wa kufumbata Msalaba kama alivyofanya Bikira Maria pale Mlimani Kalvari alipomwona Mwanaye mpendwa akiinama kichwa na kukata roho, akajaliwa kupata neema ya matumaini dhidi ya matumaini yote!

Baba Mtakatifu Francisko anasema, hivi ndivyo ilivyokuwa kwa watakatifu waliotangazwa na Mama Kanisa mwanzoni mwa Ibada ya Misa takatifu. Hawa ni mashuhuda wa imani walioamwambata Kristo Yesu ambaye hatimaye, aliwaonesha nguvu ya ufufuko wake, kama inavyojidhihirisha katika muujiza uliotendwa na Nabii Eliya pamoja na ule wa Yesu aliyemfufua Mtoto wa mjane wa Naini. Katika shida na mahangaiko ya binadamu, Mwenyezi Mungu anajitwalia dhamana ya kushuhudia ukuu wake dhidi ya kifo! Kwa njia ya Sala, Nabii Eliya alipambana na Mwenyezi Mungu, akimwomba kurudishia tena yule mtoto zawadi ya uhai, mwishoni, Mwenyezi Mungu akaridhia ombi la Eliya na kumfufua yule kijana.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, Injili inaonesha jinsi ambavyo Yesu alivyokuwa na huruma kwa yule mwanamke wa Naini, akajitwalia dhamana ya kupambana na mauti na hatimaye kushinda na kumrudisha yule mtoto kwa mwanamke wa Naini, ushuhuda wa huruma na upendo wa Mungu unaomwilishwa katika maisha na utume wa Kristo Yesu. Mtume Paulo anashuhudia akisema, katika maisha yake alikuwa ni mtu wa hatari kabisa kwani aliwatesa na kuwadhulumu Wakristo, lakini sasa ni shuhuda wa Injili ya Kristo, zawadi ya huruma ya Mungu iliyomwita, ikamchagua na hatimaye, kumfunulia Mwanaye mpendwa, ili kumtangaza na kumshuhudia kati ya Watu wa Mataifa.

Mwenyezi Mungu kwa wema na upendo wake amemfunulia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu! Kwa neema hii, Paulo mtume amekuwa ni mjumbe na shuhuda wa Injili ya Kristo. Yesu anaendelea kuwaangazia na kushuhudia neema inayoleta maisha. Mama Kanisa anabeba dhambi za watoto wake ili kuwatakasa na kuwarejesha tena ndani ya Kanisa wakiwa na maisha mapya. Haya ndiyo matunda ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Na watakatifu Stanislaus wa Yesu na Maria pamoja na Sr. Maria Elizabeth Hesselblad ni mashuhuda amini wa Fumbo la Ufufuko. Hawa ndio wanaomwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa kugeuza kilio chao kuwa ni wimbo wa sifa na shukrani, wanamshukuru kwa sababu amewanyanyua na kuwapandisha juu kabisa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.