2016-06-05 11:32:00

Wasifu wa watakatifu wapya!


Baba Mtakatifu Francisko Jumapili tarehe 5 Juni 2016 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican ili kuwatangaza wenyeheri Stanislaus wa Yesu na Maria pamoja na Sr. Maria Elizabeth Hesselblad kuwa watakatifu. Kabla ya Misa Takatifu Kardinali Angelo Amato, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la kuwatangaza waamini kuwa wenyeheri na watakatifu alisoma wasifu wa watakatifu hawa wapya.

Mtakatifu Stanislaus wa Yesu na Maria alizaliwa nchini Poland kunako tarehe 18 Mei 1631. Akajiunga na Shirika la Watawa Scolopi na baada ya majiundo yake ya kitawa akapadrishwa kunako mwaka 1616. Katika maisha yake, akaonesha umahiri mkubwa wa kughani, mhubiri mzuri na muungamishaji asiyekuwa na makuu. Alikuwa ni muunganishaji wa Askofu mkuu Antonio Pignatelli aliyekuwa Balozi wa Vatican nchini Poland ambaye baadaye alichaguliwa kuwa Khalifa wa Mtakatifu Petro na kuitwa Papa Innocent XII.

Baadaye alianzisha Shirika la Mapadre wa Maria ili kueneza Ibada kwa Bikira Maria Mkingiwa dhambi ya asili; kwa kuwakumbuka na kuwaombea marehemu walioko toharani, hususani marehemu waliokufa kutokana na vita na magonjwa ya milipuko. Kuanzia mwaka 1677, makao makuu ya Shirika yakawa huko Gora Kalwaria. Hapa akajikita zaidi katika kuwahudumia maskini, akawa ni kielelezo makini cha utawala wa sheria na uongozi bora Shirikani kwake. Akafariki dunia kunako tarehe 17 Septemba 1701na kuacha utajiri mkubwa wa nyaraka za maisha ya kiroho na kunako mwaka 2007, Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI akamtangaza kuwa Mwenyeheri.

Mtakatifu Sr. Maria Elizabeth Hesselblad alizaliwa kunako tarehe 4 Juni 1870 huko Uswiss kutoka katika familia ya Waluteri. Tangu utotoni mwake, alijifunza Maandiko Matakatifu, akakazia umoja wa Kanisa chini ya Kristo mchungaji mkuu. Akiwa na umri wa miaka kumi na nane, alihamia nchini Marekani ili kutafuta ajira kwa ajili ya kuisaidia familia yake. Katika mazingira yake, akakutana na mashuhuda wa imani ya Kanisa Katoliki waliomvuta kwa mtindo wao wa maisha. Hatimaye akabatizwa kunako mwaka 1902.

Kutokana na maradhi aliyokuwa nayo tangu alipokuwa mtoto mdogo, alitamani kuaga dunia akiwa kwenye nyumba ya Mtakatifu Bridgida wa Uswiss mjini Roma. Alipokuja Roma, akahisi cheche za wito wa kitawa na hatimaye, akaanzisha Shirika la Mkombozi la Mtakatifu Bridgita. Katika maisha yake alionesha kwa namna ya pekee ari na moyo wa kimissionari uliojikita katika umoja wa Kanisa; akawa ni mfano bora wa kuigwa katika huduma kwa maskini na wale waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii, hasa wakati wa Vita kuu ya Pili ya Dunia. Tarehe 24 Aprili 1957 akaitupa mkono dunia, huku akisadaka maisha yake kwa ajili ya umoja wa Wakristo. Mtakatifu Yohane Paulo II, kunako mwaka 2000 wakati wa Maadhimisho ya Jubilei kuu ya Ukombozi akamtangaza kuwa Mwenyeheri. Baadaye, Kanisa mwezi Machi, 2016 likatambua ukuu wa Mungu uliokuwa unajidhihirisha kupitia kwa Mwenyeheri Maria Elizabeth Hesselblad.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.