2016-06-05 11:57:00

Sheikha Moza Binti Nasser akutana na Papa mjini Vatican


Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi tarehe 4 Juni 2016 amekutana na kuzungumza na Sheikha Moza Binti Nasser, Rais wa Mfuko wa Elimu, Sayansi na Maendeleo ya Jamii wa Qatar ambaye amemfahamisha Baba Mtakatifu shughuli zinazofanywa na Mfuko huu katika medani ya elimu na maendeleo jamii katika ngazi ya kitaifa na kimataifa.

Ameelezea hali mbaya ya elimu katika maeneo ambayo kwa sasa yamekumbwa na vita na Baba Mtakatifu Francisko amemtia moyo kuendelea kusaidia mchakato wa maboresho ya elimu kwa ajili ya mafao ya watoto kwa sas ana kwa siku za usoni. Padre Federico Lombardi, Msemaji mkuu wa Vatican anabainisha kwamba, mazungumzo kati ya Baba Mtakatifu na mgeni wake yamefanyika katika mazingira ya amani na utulivu na kwamba, wamepeana zawadi.

Sheikha Moza Binti Nasser pamoja na ujumbe wake, baadaye walikutana na kuzungumza na Askofu mkuu Angelo Becciu, Katibu mkuu mwambata wa Vatican aliyekuwa anaongoza ujumbe wa viongozi waandamizi kutoka Vatican, ili kutiliana sahihi makubaliano yatakayouwezesha maandishi ya mkono 80, 000 kutoka katika Maktaba Kuu ya Vatican kuingizwa kwenye mfumo wa Digitali, mradi ambao unaendelea kufanyiwa kazi tangu kunako mwaka 2010.

Lengo ni kuwawezesha wasomi kupata maandiko haya kwa njia ya mfumo wa digitali kwa ajili ya tafiti za kina. Tume ya pamoja imeundwa ili kusimamia na kuratibu shughuli za kuhifadhi, kukarabati, kuweka katika mfumo wa digitali, kuandika na kuwawezesha watu wengi zaidi kufaidika na huduma hii inayojikita katika masuala ya kihistoria, kitamaduni, mali kale na sayansi ya Qatar na nchi nyingine kutoka katika Falme za Kiarabu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.