2016-06-04 16:34:00

Waamini wote wanawajibu wa kuchangia mchakato wa Uinjilishaji!


Kuamsha dhamiri ya utume kwa nyakati hizi: Mashirika ya Kipapa ya Kazi za Kimissionari katika huduma ya Makanisa machanga ndiyo kauli iliyoongoza maadhimisho ya mkutano mkuu wa Mashirika ya Kipapa ya Kazi za Kimissionari. Mkutano huu umekuwa ni wakati muafaka wa kusali, kutafakari na kushirikishana uzoefu, mang’amuzi, changamoto na fursa zilizopo kutoka sehemu mbali mbali za dunia.

Huu ni utangulizi uliotolewa na Kardinali Fernando Filoni, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu, Jumamosi, tarehe 4 Juni 2016 wakati wajumbe wa mkutano huu walipokutana ili kuzungumza na kumshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa huduma yake kwa Kanisa la Kristo! Wanatambua umuhimu wa kuyahusisha Makanisa machanga katika maisha na utume wa Kanisa la Kiulimwengu, ili Kanisa liweze kupata utambulisho wake wa Kimissionari.

Kardinali Filoni amewashukuru na kuwapongeza waamini walei wanaoshiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa, kiasi hata cha kumwezesha Khalifa wa Mtakatifu Petro kuweza kutoa msaada kwa Makanisa machanga duniani, dhamana inayohitaji kuwa na mwono mpya na dhamana ya majiundo na maisha ya kiroho kwa Makanisa machanga. Uwepo wa Mashirika haya ya Kipapa na mengineyo, yanapaswa kuwa ni nyenzo muhimu sana kwa ajili ya huduma ya majiundo endelevu katika mwono wa kimissionari kwa ajili ya Makanisa machanga na Makanisa kongwe zaidi.

Wajumbe wa mkutano huu wakati walipotembelea na kusali kwenye kaburi la Mwenyeheri Paolo Manna huko Dycenta, wamesali na kuwomba Roho Mtakatifu alisaidie Kanisa kuwaendea wote pamoja na kukuza moyo wa ushirikiano na udugu kwa Makanisa mahalia katika mchakato wa kuendeleza utume wa Kanisa. Wajumbe wamemwombea pia Baba Mtakatifu ili aweze kulisindikiza Kanisa zima ili liweze kuishi utambulisho wake wa Uinjilishaji unaotekelezwa kwa namna ya pekee na Mashirika ya Kipapa ya kazi za kimissionari, yanayomsaidia Khalifa wa Mtakatifu Petro kutekeleza dhamana na utume wake kwa Kanisa la Kristo! Wajumbe wanatambua umuhimu wa toba na wongofu wa ndani pamoja na mang’amuzi endelevu kwa taasisi wanazozihudumia kwa niaba ya Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.