2016-06-04 15:54:00

Mashemasi ni wahudumu wa Injili ya upendo na ukarimu!


Kituo cha Mashemasi Kimataifa kinaendelea kuadhimisha Jubilei ya Miaka 50 tangu kilipoanzishwa, fursa kwa wajumbe wa kituo hiki kufanya hija ya shukrani kwa Mwenyezi Mungu sanjari na maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, ili kuambata huruma na upendo wa Mungu katika maisha na utume wao. Huu ni mwendelezo wa utekelezaji wa Amri ya Upendo kwa Mungu na jirani, hali inayoonesha upya katika mafundisho ya Kristo Yesu, kwa kuyamwilisha katika uhalisia wa maisha ya watu.

Amri ya Upendo kwa jirani ni wosia uliotolewa na Kristo Yesu, siku ile iliyotangulia kuteswa kwake, akawaosha wanafunzi wake miguu na kuwataka kuoshana miguu wao kwa wao kama alivyowafanyia. Kwa kupendana wao kwa wao, wafuasi wa Kristo wanaendeleza utume  wa huduma ambayo Mwana wa Mungu alikuja kuitekeleza hapa duniani, kiasi hata cha kuyamimina maisha yake ili yaweze kuwa ni fidia ya wengi.

Amri ya upendo inajikita katika huduma makini kwa jirani, ndiyo maana tangu mwanzo wa Kanisa, Mitume waliwachagua Mashemasi, yaani wahudumu kwa ajili ya Injili ya upendo na ukarimu kwa familia ya Mungu. Haya yamesemwa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi, tarehe 4 Juni 2016 alipokutana na kuzungumza na wajumbe wa Kituo cha Mashemasi Kimataifa wakati huu kinapoendelea kuadhimisha Jubilei ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwake.

Baba Mtakatifu Francisko anasema kwamba, Mashemasi ni mashuhuda wa Amri ya Upendo, kwa kumuiga Mwenyezi Mungu katika huduma kwa jirani; upendo ambo ulimsukuma hata kuwahudumia binadamu. Huu ndio utendaji wa Mungu unaojikita katika uvumilivu, wema, upendo na utayari, ili kuwawezesha Mashemasi kuwa wema zaidi, hali ambayo inaweza pia kuwatofautisha na viongozi wengine wa Kanisa kwani: Maaskofu ni waandamizi wa Mitume na Mapadre ni wasaidizi wao wa karibu, kumbe, Mashemasi ni wahudumu wa meza ya Neno na huduma ya upendo inayotekelezwa na Mama Kanisa katika maisha ya watu kila siku. Hii ni Jumuiya ya wahudumu inayoishi na kutembea kati ya watu kwa ajili ya watu katika huduma makini.

Baba Mtakatifu Francisko anahitimisha hotuba yake kwa wajumbe wa Kituo cha Mashemasi Kimataifa kwa kuwatakia heri na mafanikio katika hija yao mjini Roma, hasa wakati huu wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, ili kweli mwaka huu uwasaidie kuwa na mang’amuzi ya kina juu ya huruma ya Mungu, tayari kukua na kuendelea kukomaa kama watumishi wa Kristo. Mwenyezi Mungu aendeelee kuwaenzi katika huduma na hatimaye kuwawezesha kufikia ukomavu wa imani katika upendo wake mkuu na hivyo kuuishi katika furaha na majitoleo thabiti. Amewahakikishia sala, sadaka na baraka zake za kitume katika huduma yao kwa familia ya Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.