2016-06-04 16:12:00

Iweni na shahuku ya kuwa ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu!


Baba Mtakatifu Francisko Jumapili tarehe 5 Juni 2016 anatarajiwa kuongoza Ibada ya Misa Takatifu kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro Mjini Vatican kwa ajili ya kuwatangaza Mwenyeheri Padre Stanislaw Papczynski na Sr. Maria Elizabeth Hesselblad kuwa Watatakatifu. Katika maisha na utume wake, Padre Stanislaw alitamani daima kuwa ni chombo na shuhuda wa huruma ya Mungu. Hivi ndivyo Baraza la Maaskofu Katoliki Poland linavyosema katika barua yake ya kichungaji kwa Familia ya Mungu nchini humo, Kanisa linapomtangaza Mwenyezi Padre Stanslaw kuwa Mtakatifu, matendo makuu ya Mungu.

Maadhimisho haya ni mwaliko kwa familia ya Mungu kupokea na kuambata tena na tena huruma ya Mungu sanjari na kuendeleza mchakato wa kupyaisha ile neema ambayo Wakristo walikirimiwa wakati walipokuwa wanabatizwa; tayari kujibu upendo wa Mungu kwa dhati kabisa, pamoja na kuonesha huruma kwa walio hai na wale ambao tayari wamekwisha kutangulia mbele za haki.

Padre Papzcynski aliishi kunako karne ya XVII, akaonesha kwa namna ya pekee Ibada kwa Moyo Safi wa Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya asili. Miaka 150 kabla ya Kanisa kutangaza na kuungama Ubikira wa kweli na wa daima wa Maria, kunako mwaka 1673 alianzisha Shirika la kwanza la Mapadre wa Maria nchini Poland.

Kunako mwaka 2011, Bunge la Poland likamtambua kuwa ni raia ambaye alijitosa kimasomaso bila ya kujibakiza ili kuonesha moyo wa uzalendo kwa nchi yake. Baraza la Maaskofu Katoliki Poland linafafanua kwamba, Mwenyezi Mungu anaendelea kuamsha vyombo na mashuhuda wapya wa Injili ya huruma katika nyakati na mahali pasipo na mipaka. Mashuhuda hawa ni msaada mkubwa kwa waamini kupokea Injili ya huruma ya Mungu na kuimwilisha katika uhalisia wa maisha yao ya kila siku.

Mama Kanisa kwa kumtangaza Padre Stanislaw Papczynski kuwa Mtakatifu pamoja na watakatifu wengine ambao kweli wamekuwa ni mashuhuda wa Injili ya huruma ya Mungu, inaonesha kwamba, Kanisa linaendelea kupata waombezi na watetezi mbele ya Mungu, changamoto kwa waamini kuendelea kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 








All the contents on this site are copyrighted ©.