2016-06-04 15:28:00

Baraza Jipya la Kipapa: Walei, Familia na Maisha!


Baba Mtakatifu Francisko kwa kuzingatia ushauri wa Baraza la Ushauri la Makardinali, Jumamosi tarehe 4 Juni 2016 amepitisha Katiba mpya ya Majaribio kwa Baraza jipya la Kipapa la Walei, Familia na Maisha, litakaloanza kutekeza dhamana na wajibu wake hapo tarehe 1 Septemba 2016, kwa kuyaunganisha Mabaraza ya Kipapa ya Walei na Familia. Kuanzia tarehe hiyo, Mabaraza haya mawili yatakoma kuwepo na hivyo Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha kuanza kushika hatamu.

Baraza hili jipya litakuwa na dhamana ya kuhamasisha maisha na utume wa waamini walei; litajikita katika utume wa familia mintarafu mpango wa Mungu katika maisha ya mwanadamu pamoja na kusimama kidete kutetea maisha ya binadamu. Baraza hili litakuwa na Mwenyekiti atakayesaidiwa na Katibu mkuu anayeweza kuwa hata mwamini mlei akisaidiwa na Makatibu wakuu wasaidizi watatu ambao wote watakuwa ni waamini walei. Baraza hili limegawanyika katika vitengo vikuu vitatu: Waamini walei; Familia pamoja na Maisha na kila kitengo kitakuwa  na katibu msaidizi.

Wajumbe wa Baraza hili ni waamini ambao wamejipambanua katika maisha na utume wa Kanisa kutoka sehemu mbali mbali za dunia wanaoshuhudia taswira ya Kanisa la Kiulimwengu. Litakuwa na washauri wake na kufuata sheria zote zilizowekwa na Vatican. Baraza hili litakuwa na dhamana ya kuandaa na kusimamia makongamano ya kimataifa kwa ajili ya utume kwa waamini walei; litasimamia taasisi za ndoa, ukweli wa familia na maisha ndani ya Kanisa mintarafu hali ya kibinadamu na kijamii ya waamini walei, taasisi ya familia na maisha ya binadamu katika jamii.

Kitengo cha Walei kitakuwa na wajibu wa kuwahamasisha waamini walei katika wito na utume wao ndani ya Kanisa na ulimwengu katika ujumla wake. Kitaendelea kufanya tafiti mbali mbali ili kukazia mafundisho ya Kanisa kuhusu waamini walei ili watambue dhamana na wajibu wao ndani ya Kanisa, kila mtu kadiri ya karama zake. Kuwajengea uwezo waamini walei ili waweze kushiriki kikamilifu katika mchakato wa Uinjilishaji, tayari kuyatakatifuza malimwengu. Kitengo hiki pamoja na mambo mengine kitakuwa na dhamana ya kuwafundisha na kuwahamasisha waamini walei kushiriki kikamilifu katika Katekesi, Liturujia, Sakramenti; shughuli za Kimissionari na Matendo ya huruma katika juhhudi za kumwendeleza mwanadamu. Kitengo pia kitasimamia na kuratibu Mashirika na Vyama vya Kitume vyenye hadhi ya kimataifa.

Kitengo cha familia kitakuwa na dhamana ya kuendeleza Utume wa Familia; kulinda na kudumisha utu na mafao ya familia kadiri ya Sakramenti ya Ndoa; kwa kulinda haki na wajibu wao ndani ya Kanisa na katika Jamii, ili taasisi ya familia iweze kutekeleza wajibu wake barabara. Kitakuwa na wajibu wa kusoma alama za nyakati ili kulinda na kudumisha tunu msingi za maisha ya familia. Kitaratibu Mashirika na Vyama vya Kitume kwa ajili ya maisha ya ndoa na familia kitaifa na kimataifa kwa ajili ya ustawi wa familia. Kitawajibika kusimamia mafundisho tanzu ya Kanisa kuhusu Ndoa na Familia na kuyasambaza kwa njia ya Katekesi, tasaufi ya ndoa na familia kama sehemu ya mwendelezo wa majiundo makini. Kitasimamia pia ustawi na maendeleo ya watoto na kwamba, kitakuwa na uhusiano wa moja kwa moja na Taasisi ya Papa Yohane Paulo II kwa ajili ya Ndoa na Familia” pamoja na taasisi zote ambazo ziko chini yake.

Kitengo cha Maisha kitakuwa na dhamana ya kulinda, kutetea na kudumisha maisha ya mwanadamu tangu anapotungwa mimba hadi mauti ya kawaida inapomfika kadiri ya mpango wa Mungu pamoja na kuhakikisha kwamba, binadamu anapata mahitaji yake msingi katika hatua zake mbali mbali. Kusimamia na kuratibu vyama na mashirika yanayowasaidia wanawake na familia kulinda, kutetea na kushuhudia Injili ya maisha dhidi ya utamaduni wa kifo.

Kitazingatia mafundisho tanzu ya Kanisa kuhusu kanuni maadili mintarafu matatizo na changamoto zinazoendelea kujitokeza katika masuala ya dawa za binadamu pamoja na haki ya maisha dhidi ya siasa na sera zinazotishia Injili ya uhai. Kitengo hiki kitakuwa na ushirikiano wa karibu sana na Taasisi ya Kipapa ya Maisha kuhusiana na tema zinazohusiana na kitengo hiki kama zilivyobainishwa katika Katiba ya Majaribio ya Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.