2016-06-03 10:38:00

Papa Francisko kutembelea Makao Makuu ya WFP 13 Juni 2016


Shirika la Mpango wa Chakula Duniani, WFP, katika taarifa yake kwa vyombo vya habari linasema kwamba, Baba Mtakatifu Francisko, hapo tarehe 13 Juni 2016 anatarajiwa kutembelea na kuzungumza na wajumbe wa mkutano mkuu wa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani, kwenye Makao yake makuu yaliyoko mjini Roma. Hili litakuwa ni tukio la kihistoria kwa Baba Mtakatifu Francisko kuwa Papa wa kwanza kutembelea na kuzungumza na wajumbe wa  Shirika hili, hawa wakati huu Jumuiya ya Kimataifa inapoanza kutekeleza Malengo ya Maendeleo Endelevu.

Wanachama wa Umoja wa Mataifa wamekubaliana kimsingi na Malengo ya Maendeleo Endelevu 17 yaliyobainishwa ili kujifunga kibwebwe kupambana na mambo yanayosababisha umaskini na baa la njaa linaloendelea kutesa na kunyanyasa utu na heshima ya binadamu. Mkutano mkuu unataka kuibua mbinu mkakati utakaoiwezesha Jumuiya ya Kimataifa kuwa na Baa la Njaa Zero ifikapo mwaka 2030.

Wakati wa tukio hili, Baba Mtakatifu Francisko atawahutubia wajumbe wa Baraza la Shirika la Mpango wa Chakula Duniani; ambao wajumbe wake pia ni wajumbe wa Umoja wa Mataifa. Kama kawaida, Baba Mtakatifu Francisko atapata pia nafasi ya kuzungumza na wafanyakazi wa WFP na familia zao, tukio ambalo litarushwa moja kwa moja kutoka kwenye Ofisi hizi hapa mjini Roma.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.