2016-06-02 13:16:00

Dhana ya huruma ya Mungu!


Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu kwa Wakleri na Majandokasisi, ametoa tafakari tatu zitakazowasaidia Wakleri na Majandokasisi katika maisha na utume wao katika: kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Katika tafakari yake ya kwanza, aliyoitoa kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane wa Laterano, Alhamisi, tarehe 2 Juni 2016 amezungumzia huruma inayojikita katika mwelekeo wa kimama.

Baba Mtakatifu ametoa ushauri wa mambo makuu matatu yanayopaswa kuzingatiwa na mapadre: umuhimu wa maisha ya sala ili kuzima kiu ya maisha ya ndani; umuhimu wa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu pamoja na kuomba neema ya kuwa kweli ni Mapadre wenye uwezo wa kuomba na kutoa huruma. Huruma kwa namna ya pekee inaguswa na udhaifu pamoja na mahangaiko ya watu ili kuweza kukua na kuishi.

Huu ndio mwelekeo wa huruma mintarafu mwono wa kimama. Kwa upande mwingine huruma inayoshuhudiwa na mababa inaonesha uaminifu, msamaha, dira na kwamba, msamaha ni matunda ya agano. Katika maana mapana zaidi, huruma inajikita katika huduma ya upendo kwa wale wanaoteseka, kwa watu wanaokosa haki zao msingi, tayari kutoa suluhu ya amani kwenye hali na mazingira kama haya. Huu ndio mwelekeo ambao Kristo Yesu amependa kuwafunulia waja wake kwamba, jina la Mungu ni huruma.

Kumbe, mwamini daima anapaswa kujikita katika wongofu, tafakari na upendo uliopyaishwa, tayari kuambatana na Mungu anayesamehe dhambi za waja wake na kuwapatia neema ya kuwa ni vyombo na mashuhuda wa matendo ya huruma, kielelezo cha imani tendaji. Yesu kwa muhtasari anakaza kusema, heri wenye rehema maana hao watapata rehema ili kuweza kutekeleza dhamana na wajibu wao mbele ya Mwenyezi Mungu, kwa kuwa kweli ni vyombo vya huruma ya Mungu kwa waja wake, tayari kushiriki katika furaha ya Mungu kama inavyojionesha kwenye mfano wa Baba mwenye huruma, tayari kutoka katika mwelekeo wa mtu binafsi na kuambata jumuiya, ili kuonjeshana upendo kama alivyofanya Yesu kwa muujiza wa kuwalisha watu elfu tano kwa mikate mitano na samaki wawili, mwaliko wa kushirikishana neema na baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Baba Mtakatifu Francisko anatoa ushauri unaojikita katika kifungo cha upendo kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa ufalme wa Mungu hapa duniani. Kwanza kabisa ni umuhimu wa kujikita katika maisha ya sala ili kujipatia mambo msingi yatakayoweza kuzima kiu ya maisha ya kiroho kama anavyosema Mtakatifu Inyasi wa Loyola. Kwa kutafakari kuhusu upendo wa Mungu aliyewaumba, akawakomboa na anayeendelea kuwategemeza katika maisha na utume wao, Mapadre wanaweza kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu, kama kielelezo cha moyo wa shukrani. Mapadre waoneshe moyo wa upendo kwa maskini, ili wao pia waweze kuonesha ile kiu ya kutaka kupata huruma ya Mungu.

Pili, waamini wajifunze kutoa na kupokea huruma, kwa kuonja na kuguswa na mahangaiko ya binadamu kutoka katika undani wa mioyo yao. Sala iwasaidie waamini kuzungumza na Mwenyezi Mungu, ili kuangalia udhaifu wao, tayari kuomba huruma na msamaha wa Mungu, tayari pia kuzima kiu na njaa ya watu kukutana na Mungu. Kwa namna ya pekee, huruma inamwambata mtu mzima: kiroho na kimwili; inawaambata watu wote pasi na ubaguzi.

Baba Mtakatifu Francisko anatoa ushauri wa wa tatu ambao unapaswa kufanyiwa kazi na Wakleri katika maisha na utume wao kama vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu ni kuomba neema itakayowasaidia kuwa kweli ni Mapadre wenye uwezo wa kuomba na kutoa huruma kwa kuguswa na udhaifu, mapungufu na dhambi  za binadamu, ili kuanza mchakato wa kuwa wenye huruma kama Baba yao wa mbinguni alivyo na huruma; dhana inayojikita katika matunda ya wongofu wa ndani ili kupokea  na kutoa huruma ya Mungu, ili kusaidia huruma ya Mungu kuendelea kukua na kuongezeka.

Baba Mtakatifu anawaalika Wakleri kuacha tabia kuwa watazamaji na badala yake kuwa ni wahusika wakuu katika kupokea na kugawa huruma ya Mungu kama inavyojionesha kwenye mfano wa Baba mwenye huruma, ili kuondokana na ubinafsi, utumwa na kijicho uliooneshwa na mwana mpotevu kiasi cha kutamani kurejea nyumbani kwa Baba, kwa kukumbuka wema na uzuri wa nyumbani kwao, kiasi cha kuzama katika tafakari ya kina na kugundua jinsi ambavyo alikosa mbele ya Mbingu na dunia, lakini aliporejea nyumbani, Baba mwenye huruma alimkumbatia na kumfanyia sherehe kubwa.

Baba Mtakatifu anasema, huruma ya Mungu inaendelea kububujika kwa njia ya Damu Azizi ya Yesu inayotolewa kwa ajili ya msamaha na wokovu wa watu; hii ni damu ya Agano Jipya na la Milele; ni Agano la huruma ya Mungu. Hii ni DamuAzizi inayosafisha na kuwapatanisha wote; ni Damu inayosamehe dhambi; kinywaji safi kinachotoa maisha ya uzima wa milele kwa wale waliokufa kutokana na dhambi. Waamini waone aibu inayotunza heshima yao kama alivyofanya yule Mwana mpotevu, wawe na moyo wa unyenyekevu kama alivyokuwa Mtakatifu Petro kwa kuonesha ukuu na mapungufu yake kama binadamu. Alipokuwa anazama, Petro akapiga ukelele kuomba msaada kutoka kwa Kristo, akamshika mkono na kumrudishia utu wake na heshima yake tena! Huruma ya Mungu ikamweka huru; huruma inaweza kukubaliwa au kukataliwa, lakini ikumbukwe kwamba, huruma ya Mungu inamwambata mwanadamu katika maisha yake.

Leo hii mwanadamu anakumbuna na umaskini wa kiroho, kimwili na kimaadili hivyo kuwa na uhitaji wa huruma ya Mungu inayobubujika kutoka katika Moyo Mtakatifu wa Yesu ili kushiriki tena ile furaha ya kurejeshewa huruma ya Mungu inayomkirimia mtu maisha dhidi ya kifo, matokeo ya dhambi. Waamini wafungue nyoyo zao ili kuwasaidia wengine ili nao waweze kusaidiwa na Mwenyezi Mungu. Huruma inapaswa kusambazwa kwa watu kama alivyofanya Yesu katika maisha na utume wake: kwa kuponya magonjwa na udhaifu wa mwili, kwa kusamahe dhambi na kuwalisha na kuwanywesha watu kwa ngano safi na asali itokayo mwambani. Kwa njia hii, Yesu alijishusha ili kuwashirikisha watu huruma ya Mungu na wala si kama mtazamaji. Hiki ndicho kielelezo kinachoshuhudiwa na Bikira Maria katika utenzi wake wa “Magnificati” na Zaburi ya 50 ya Mfalme Daudi anayeomba huruma na msamaha kutokana na dhambi zake.

Na Padre Richard A. Mjigwa. C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.