2016-06-01 08:24:00

Wafungwa fungueni malango ya nyoyo zenu ili mpokee huruma ya Mungu!


Baba Mtakatifu Francisko anawapongeza na kuwashukuru wale wote wanaojisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kuwahudumia wafungwa magerezani; kwa kusimama kidete kulinda na kutetea utu na heshima yao bila kusahau haki zao msingi. Baba Mtakatifu anasema, yupo pamoja nao katika sala, mshikamano wa kidugu na sadaka yake anayomtolea Mwenyezi Mungu kila siku. Haya yamo kwenye ujumbe wa Baba Mtakatifu ulioandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kwenye mkutano wa wahudumu wa maisha ya kiroho kutoka katika Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Umoja wa Ulaya.

Mkutano huu ulifunguliwa hapo tarehe 30 Mei na kuhitimishwa tarehe 1 Juni 2016 huko Strasbourg. Huu ni mkutano wa Tume ya Kikatoliki Kimataifa kwa ajili ya Huduma za Kichungaji kwa Wafungwa Magerezani, ambao umeandaliwa pia kwa ushirikiano na Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Umoja wa Ulaya. Baba Mtakatifu anawashukuru wahudumu wa maisha ya kiroho magerezani kwa kuwasaidia wafungwa kuweza kuadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu hata wakiwa magerezani, kwani jambo la msingi hapa ni kwa wafungwa wenyewe kumfungulia malango ya mioyo yao ili kuonja huruma na upendo wa Mungu kila wakati wanapopita katika malango ya magereza. Anawakumbusha kwamba, neema ya Mungu ina uwezo wa kuleta mageuzi katika nyoyo na maisha ya watu na hivyo kuwakirimia uhuru na amani ya ndani. Baba Mtakatifu Francisko anahitimisha ujumbe wake kwa kuwatakia wajumbe wote neema na baraka zake za kitume.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.