2016-06-01 15:36:00

Kanisa Katoliki kuendelea kushirikiana na Taasisi ya "Jainology"


Kardinali Jean Louis Tauran, Rais wa Baraza la Kipapa la majadiliano ya kidini, Jumanne, tarehe 31 Mei 2016 amekutana na kuzungumza na ujumbe wa Taasisi ya Kimataifa ya Jainology iliyokuwa chini ya uongozi wa Bwana Nemu Chandaria, Mwenyekiti wa Taasisi hii kama sehemu ya mwendelezo wa mikutano baina ya Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini na taasisi ya “Jainology” iliyofanyika kunako mwaka 1995 na mwaka 2011, ingawa kumekuwepo pia na mikutano ya kawaida baina ya pande hizi mbili kuanzia mwaka 1986.

Baraza la Kipapa la Majadiliano ya kidini kwa kushirikiana na wajumbe wa Taasisi ya “Jainology” nchini India, Uingereza na Marekani,  waliweza kufanikisha mikutano baina ya pande hizi mbili kunako mwaka 2011, 2013 na mwaka 2015. Mikutano yote hii imeadhimishwa katika hali ya kirafiki na kuheshimiana na kwamba, pande zote mbili zimeridhika kwa ushirikiano kati ya Wakristo na wajumbe kutoka katika taasisi hii hadi sasa. Viongozi hawa katika tamko lao wanapenda kuendeleza ushirikiano katika maeneo mahalia, ili kushiriki kikamilifu katika mchakato wa kuchangia katika ustawi, maendeleo na mafao ya jamii. Wamekazia umuhimu wa elimu kwa vijana wa kizazi kipya, ili kuwasaidia kutambua mapokeo na tamaduni zao, ili waweze pia kuheshimu na kuthamini tamaduni za watu wengine.

Mkutano huu umeongozwa na kauli mbiu “Umuhimu wa kutunza dunia, nyumba ya familia ya binadamu” kwa kukazia ushirikiano na waamini wa dini mbali mbali ili kulinda na kutunza mazingira, hatimaye, dunia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi. Wamekazia umuhimu wa kujikita katika amani na upendo; huduma ya upendo na mshikamano kwa maskini pamoja na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Waamini wote wanahamasishwa kulinda, kutunza na kuendeleza mazingira kwa kujikita katika msingi wa amani, matumizi sahihi ya rasilimali ya dunia, kupunguza uchafuzi wa mazingira, kuheshimu uhai wa viumbe wote pamoja na kujali ustawi na maendeleo ya kizazi kijacho!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.