2016-06-01 07:19:00

Huruma na upendo wa Mungu miongoni mwa wavuvi Jimboni Musoma!


Askofu Michael Msonganzila wa Jimbo Katoliki la Musoma, Tanzania hivi karibuni amezindua kigango kipya kwenye kisiwa cha Kwirugwa, Parokia ya Nyegina, matunda ya Jubilei ya miaka mia moja ya uwepo wa Ukristo Jimbo Katoliki Musoma sanjari na maadhimisho ya Sinodi ya Jimbo la Musoma iliyojikita katika imani na matendo! Kimsingi huduma ya kichungaji kwa ajili ya wavuvi wa Kisiwa cha Kwirugwa imekuja kwa wakati muafaka, kwani mara nyingi wavuvi ni watu ambao hawapewi kipaumbele cha kutosha katika sera na mikakati ya huduma makini kiroho na kimwili!

Haya ni mageuzi makubwa hasa wakati huu Mama Kanisa anapoadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Hata wavuvu wanapaswa kuonjeshwa huruma na upendo wa Mungu kwa wakati muafaka! Askofu Michael Msonganzila aliweza kubariki nyumba ya Mapadre watakaokuwa wanatoa huduma ya Neno, Sakramenti na Matendo ya huruma, ili watu wengi zaidi waweze kukutana na Kristo Mkombozi wa ulimwengu.

Vita ya Ukimwi ni mapambano endelevu na vinapaswa kuvaliwa njuga na kila mtu, sanjari na kuwahudumia kwa upendo wale walioathirika kutokana na Virusi vya Ukimwi. Askofu Msonganzila amewakumbusha wavuvi kwamba, Ukimwi upo na unaendelea kupukutisha maisha ya watu wengi hasa Visiwani ambako takwimu zilizotolewa ni za kutisha na kusikitisha sana. Kuna idadi kubwa ya wavuvi kutoka sehemu mbali mbali wanaotekeleza shughuli zao Kisiwani hapo ili kujipatia riziki yao ya kila siku. Kwa bahati mbaya, wavuvi hawa wamekuwa wakitelekeza familia zao na hivyo kujikuta wakitumbukia katika anasa na ulevi wa kupindukia, hali ambayo inawapelekea kuanguka katika kishawishi cha ngono nje ya familia zao.

Askofu Msonganzila amewakumbusha wavuvi hawa kwamba, bado wanategemewa kwa kiasi kikubwa na familia zao, kumbe wanapaswa kujikita katika kanuni maadili, uaminifu kwa wake zao pamoja na kudumisha utu wema. Fedha ya chapu chapu isiwafanye kusahau familia zao zinazoteseka sana pale wanapokumbwa na Ukimwi, wakiwa kwenye shughuli za uvuvi. Wavuvi wajenge utamaduni wa kuwa waaminifu kwa wake zao, ili waweze kufurahia matunda ya jasho na ugumu wa kazi ya uvuvi ambao una mchango mkubwa katika mchakato wa kukuza uchumi kuanzia katika ngazi ya kifamilia.

Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Kisiwa hiki Bwana Emmanuel Kigwa amewakumbusha wavuvi kwamba, kamwe serikali haitawavumilia watu wenye tabia chafu wanaoweza kuambukizwa ugonjwa wa Ukimwi. Watu wa namna hiyo wakigundulika watarudishwa mahali walipotoka. Wananchi kwa kutambua changamoto za maisha wameanza kujikita katika kanuni maadili na utu wema; kwa kuwa waaminifu kwenye ndoa na wenzi wao, kwani wengi wao wameguswa na kutikiswa na ugonjwa wa Ukimwi. Kisiwani hapo wananchi wanaendelea kuhamasishwa kutunza mazingira nyumba ya wote ili kuepuka magonjwa ya milipuko ambayo kimsingi yanaharibu mchakato wa maendeleo endelevu ya watu.

Familia ya Mungu Jimbo Katoliki Musoma imempongeza sana Askofu Msonganzila kwa kuonesha moyo na ujasiri wa kibaba kwa kuthubu kuwa ni Askofu wa kwanza kutembelea Kisiwani hapo ili kutangaza na kushuhudia Neno la Mungu linalojikita katika huruma na upendo. Waamini wameahidi kumuunga mkono Askofu kwa kitendo hiki cha ujasiri, ili kweli hata wao waweze kuwa ni mashuhuda na vyombo vya Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Wavuvi wengi walishikwa na bumbuwazi kumwona Askofu Michael Msonganzila, akiwa miongoni mwao, kielelezo cha Baba mwenye huruma na mapendo!

Na Veronica Modest,

Jimbo Katoliki Musoma. 








All the contents on this site are copyrighted ©.