2016-05-30 14:30:00

Wakurugenzi wa PMS Kitaifa wako Roma kwa mkutano mkuu!


Mashirika ya Kipapa ya Kazi za Kimissionari yameanza mkutano wake wa mwaka unaowakusanya wakurugenzi wa mashirika haya kitaifa pamoja na viongozi wakuu kutoka katika Mashirika haya hapa Vatican. Mkutano huu unaongozwa pamoja na mambo mengine, unajadili kuhusu “Siku za kichungaji” tema inayojadiliwa kuanzia tarehe 30- 31 Mei, 2016.

Tema ya pili ni kuamsha dhamiri ya utume kwa nyakati hizi. Tema ya tatu Mashirika ya Kipapa ya Kazi za Kimissionari kwa ajili ya huduma kwa Makanisa changa. Kutakuwa na tema inayojadili Jubilei ya miaka 100 tangu kuanzishwa kwa Umoja wa Mashirika ya Kipapa Kimissionari na hatimaye, mkutano wa kawaida wa Masahirika haya utakaotimua vumbi kati ya tarehe 2 hadi 4 na kufungwa kwa kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko.

Mkutano huu umefunguliwa na Askofu mkuu Protase Rugambwa, Katibu mwambata na Rais wa Mashirika ya Kipapa ya Kazi za Kimissionari. Wajumbe wametoa shuhuda zao pamoja na kusikiliza changamoto kutoka kwa viongozi wakuu wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu na Mashirika ya Kipapa ya Kazi za Kimissionari. Mkutano huu ni wakati muafaka wa kusali, kutafakari na kushirikishana fursa, matatizo na changamoto zilizoko katika maisha na utume wa Makanisa mahalia. Wajumbe watawasilisha miradi kutoka kwenye Makanisa mahalia, ili iweze kupitishwa na hatimaye, kufadhiliwa na Kanisa. Askofu mkuu Protase Rugambwa siku ya Ijumaa, tarehe 3 Juni atafunga mkutano na Jumamosi, tarehe 4 Juni 2016 wajumbe watakutana na Baba Mtakatifu Francisko.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.