2016-05-30 11:11:00

Papa Francisko: Zingatieni: Kumbukumbu, Unabii na Matumaini!


Mama Kanisa katika hija yake ya imani kama hata ilivyo kwa kila Mkristo anapenda kuacha nafasi ya kufanya kumbukumbu endelevu ya zawadi na karama ambazo amekirimiwa na Mwenyezi Mungu kama sehemu ya mwendelezo wa unabii sanjari na ujenzi wa matumaini. Haya ni mambo makuu yaliyochambuliwa na Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican, Jumatatu, tarehe 30 Mei 2016.

Baba Mtakatifu amewataka waamini kutokuwa na shingo ngumu kwa kufunga mioyo yao kwenye mfumo wa sheria peke yake, mambo ambayo wakati mwingine ni kikwazo cha mwendelezo wa Unabii unaopaswa kuvuka mipaka na kwenda mbali zaidi. Katika maisha ya kiimani, kuna matumaini lakini pia kuna hatari ya kuweza kuzima amana ya kumbu kumbu na mwendelezo kutoka kwa Roho Mtakatifu. Huu ndio ndio mwelekeo uliooneshwa na Wakuu wa Makuhani na waandishi kama inavyosimuliwa na Mwinjili Marko.

Hawa walitaka kumfunga mdomo Kristo kama ilivyojitokeza kwenye mfano wa vibarua wauaji waliowatesa, wakawapiga kwa mawe watumishi wa Bwana mwenye shamba na hatimaye wakamuua hata Mwanaye wa pekee,  ili waweze kurithi shamba lile! Mauaji ya watumishi na Mwana wa pekee ni picha inayotumiwa kwa ajili ya Manabii kwenye Agano la Kale na Yesu kwenye Agano Jipya. Hawa ni watu waliojifunga katika ubinafsi na undani wao, kiasi hata cha kushindwa kujifunua kwa ahadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, hawa ni watu wasiokuwa na kumbu kumbu hai wala matumaini. Wakuu wa Makuhani na waandhishi walitaka kujenga kuta za utengano zinazojikita katika sheria, mfumo wa maisha uliofichika katika ubinafsi. Ni kundi la watu ambalo halikutaka kuwaona Manabii, ili kutokuwa na matumaini na hivyo kushindwa kumpatia nafasi Roho Mtakatifu kutenda kadiri anavyotaka. Viongozi hawa wakashindwa kutambua zawadi ya Mungu kwa njia ya Roho Mtakatifu, kiasi cha kutupilia mbali uwepo wa unabii na matumaini.

Huu ni mfumo ambao Neno la Mungu linauelezea kuwa ni uharibifu uliomo ulimwenguni unaojikita katika tamaa. Wakuu wa Makuhani walitamani kuona Yesu anapoteza kumbu kumbu na Unabii; wakatamani usalama wao badala ya matumaini. Huu ndio utumwa wa Sheria na uhuru unaotajwa na Mtakatifu Paulo katika Nyaraka zake. Kanisa liko huru pale linapojikita katika: Kumbukumbu endelevu, Unabii na Matumaini. Shamba linalotunzwa vyema ni taswira ya Watu wa Mungu, Kanisa na nyoyo za waamini, zinazotunzwa kwa upendo na upole.

Waamini wawe na ujasiri wa kukita maisha yao katika kumbu kumbu endelevu na pale wanapojikwaa na kuanguka, wawe na ujasiri wa kusimama na kurejea tena kwenye msingi wa maisha yao ya kiroho. Wajiulize katika maisha yao, ikiwa kama bado wana kumbu kumbu endelevu ya matendo makuu ya Mungu na karama zake katika maisha yao; ikiwa kama wako tayari kufungua malango ya mioyo yao kwa Manabii katika Ibada au wamejifungia katika sanduku la Sheria, kiasi cha kushindwa hata kuwa na matumaini kama aliyokuwa nayo Ibrahimu, Baba wa imani?

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.