2016-05-30 07:42:00

Msiadhimishe na kupokea Mafumbo ya Kanisa kwa mazoea!


Ekaristi takatifu ni chakula cha kweli kinachoshibisha roho za waamini. Hili ni fumbo ambalo linapaswa kuadhimishwa kwa ibada, uchaji na moyo mkuu na wala si kwa mazoea au kufuata mkumbo. Sakramenti ya Ekaristi inafumbata utajiri wote wa kiroho wa Kanisa, yaani Ekaristi Takatifu ni Kristo mwenyewe. Ekaristi Takatifu na Sakramenti ya Upatanisho ni chanda na pete hasa kwa nyakati hizi ambamo dhana ya dhambi na madhara yake inaanza kufutika taratibu katika akili na maisha ya watu.

Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwaichi wa Jimbo kuu la Mwanza katika mahojiano maalum na Radio Vatican anazungumzia umuhimu wa Sakramenti ya Ekaristi Takatifu na Upatanisho katika maisha ya mwamini. Kwani hizi ni Sakramenti zinazowaonjesha waamini upendo, huruma na msamaha unaobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu na Kanisa lake. Sakramenti hizi pacha zinapewa msukumo wa pekee wakati huu wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu.

Lakini, Askofu Mkuu Ruwaichi anakaza kusema waamini wanapaswa kuelewa kwa kina mafumbo wanayoadhimisha, ili waweze kujiandaa kikamilifu badala ya kuadhimisha mafumbo ya Kanisa kwa mazoea au kuyafanya kuwa jambo la kijamii. Hapa kwa namna ya pekee anazungumzia Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, kamwe waamini wasiipokee kwa mazoea. Waamini wajitaabishe kuungama dhambi zao kabla ya kujongea kumpokea Kristo katika Sakramenti ya Ekaristi Takatifu. Waamini watambue kwamba, Sakramenti ya Upatanisho inawaganga kiroho, kumbe, dhamiri nyofu iwasukume kupokea Ekaristi Takatifu kwa moyo mweupe.

Askofu mkuu Ruwaichi anafafanua kwamba, kuna hatari kubwa ambayo inaendelea kujionesha katika ulimwengu mamboleo kwani kuna watu wenye dhamiri zilizojeruhiwa; dhamiri zilizodhohofika pamoja na dhamiri mfu zinazowapekelea watu kutenda kwa mazoea bila kuguswa na mafumbo wanayoadhimisha na kuyashiriki. Waamini wanapaswa kutambua kwamba wanapaswa kumwilisha imani katika uhalisia wa maisha yao, ili kweli imani hii iweze kugusa maisha yao: kiroho, kimwili na kidhamiri.

Waamini wanapaswa kuthamini Sakramenti ya Upatanisho katika hija ya maisha yao ya kiroho. Ili kufikia lengo hili, wachungaji wanapaswa kujitosa zaidi katika kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa kwa moyo wa Ibada, Uchaji na Heshima sanjari na kutoa mafundisho ya kina kuhusu maadhimisho haya. Pili, waamini wanapaswa kupewa katekesi ya kina na endelevu kuhusu dhana, ukweli na madhara ya dhambi katika maisha ya mtu mmoja mmoja na katika jamii.

Tatu, kuna haja ya kuwa na katekesi endelevu na ya kina na kwamba, wachungaji wanapaswa kujisadaka zaidi kuwafundisha waamini umuhimu wa kukimbilia kiti cha huruma ya Mungu, kila wakati wanapojikuta katika uhitaji. Mapadre ambao kimsingi ni wahudumu na mashuhuda wa huruma ya Mungu wanapaswa kujisadaka kwa kuwahudumia waamini wakati wote bila ya kufungwa na ratiba ambazo kwa sasa zinapelekea utamaduni wa kutothamini sana Sakramenti ya Upatanisho. Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu iwe ni fursa ya kupata katekesi ya kina kuhusu Sakramenti za huruma ya Mungu, ili kweli waamini waweze kufaidika na maadhimisho haya katika maisha yao kiroho na kimwili.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.