2016-05-30 08:54:00

Jengeni utamaduni wa majadiliano na kusikilizana katika ukweli na uwazi!


Vijana wanafunzi mia nne kutoka katika vyuo vikuu zaidi ya arobaini kutoka katika nchi 190 waliokuwa wanashiriki katika kongamano la sita la kimataifa la Taasisi ya Kipapa ya “Scholas Occurrentes” wamehitimisha kogamano hili kwa kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili tarehe 29 Mei 2016. Lengo lilikuwa ni kuendeleza mchakato wa kubomoa kuta za utengano kati ya watu ili kujenga na kuimarisha madaraja ya kuwakutanisha watu yanayojikita kwa namna ya pekee katika elimu mashuleni. Kongamano limewashirikisha wadau kutoka katika sekta ya mawasiliano ya jamii; sanaa na michezo; sayansi na teknolojia.

Kauli mbiu ya maadhimisho haya ilikuwa ni “Chuo kikuu na shule: ni ukuta au daraja?”. Hii ilikuwa ni fursa muafaka kwa washiriki wa kongamano hili kuweza kupembua kwa kina na mapana dhana ya taasisi za elimu ya juu na shule mintarafu mwono wa Baba Mtakatifu Francisko, dhana aliyoifanyia kazi takribani miaka kumi na mitano iliyopita.

Baba Mtakatifu Francisko akizungumza na wajumbe hawa amekazia kwa namna ya pekee umuhimu wa ujenzi wa utamaduni wa watu kukutana na kujadiliana pamoja na kupongeza maendeleo makubwa yaliyokwisha kupatikana katika nyanja za mawasiliano ya jamii, changamoto pevu katika ulimwengu mamboleo. Mintafaruku na kinzani katika ngazi mbali mbali ni mwanzo wa ujenzi wa uadui, chuki na uhasama. Pale ambapo jamii inaweza kujenga urafiki na mafungamano ya kijamii, hapo udugu na utamaduni wa watu kukutana unashamiri na kustawi kama mtende wa Lebanoni.

Baba Mtakatifu amewapongeza na kuwashukuru wajumbe wote kwa kuchangia kwa hali na mali katika mchakato wa ujenzi wa utamaduni wa watu kukutana. Baba Mtakatifu anakaza kusema, katika maisha yake, hakuwahi hata siku moja kuwaza kwamba, iko siku angeweza kuchaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Kuchaguliwa kwake, limekuwa ni tukio la kushangaza sana katika maisha yake na tangu wakati huo, Mwenyezi Mungu amemkirimia amani na utulivu wa ndani ambao unaendelea kudumu hadi leo; neema na baraka kutoka kwa Mungu.

Hii imekuwa pia ni fursa ya kusikiliza shuhuda mbali mbali na hatimaye kuwatunuku watu ambao wamejitokeza kwa namna ya pekee katika mchakato wa ujenzi wa amani duniani, kati yao ni: Richard Gere, Salma Hayek pamoja na George Clooney. Wasanii hawa wamepewa tuzo hii kutokana na mchango wao unaopania kuwajengea uwezo vijana wanaotoka pembezoni mwa jamii. Hapa Baba Mtakatifu Francisko amekazia umuhimu wa kuwapatia watu utambulisho kwa njia ya elimu makini, ili watu waweze kweli kujisikia kuwa ni sehemu ya familia na jamii fulani.

Baba Mtakatifu amewataka wajumbe kujifunga kibwebwe ili kuhakikisha kwamba, wanasaidia kung’oa mateso na nyanyaso dhidi ya wanafunzi vyuoni na mashuleni. Hivi ni vitendo vinavyoficha ukatili duniani kama ilivyo pia kwa vita, mambo yanayowatendea hata watoto wadogo. Watu wajitahidi kung’oa ukatili na hatimaye, kujenga utamaduni wa kusikilizana katika uhuru, ukweli na uwazi.

Katika mchakato wa majadiliano kila mtu ni mshindi na hakuna mtu anayeweza kupoteza kitu na matunda yake ni msamaha wa kweli. Majadiliano ni kielelezo cha utashi wa kutaka kumsikiliza mwingine, tayari kujenga madaraja ya watu kukutana. Hapa kuna haja ya kuondokana na kiburi pamoja na majivuno, kaburi la maisha na utu wa binadamu. Walimwengu wajifunze zaidi unyenyekevu wa moyo, utamaduni wa kujadiliana ili waweze kutembea kwa pamoja.

Katika tukio hili la kufunga kongamano la sita la kimataifa la Taasisi ya Kipapa ya ”Scholas Occurrentes” wajumbe waliweza kushuhudia utajiri unaofumbatwa katika maisha na utume wa taasisi hii katika maisha ya sala; maswali na majibu yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko ambayo yatakusanywa na hatimaye kuchapishwa kitabu kitakachozinduliwa mwishoni mwa mwaka 2016. Kilikuwa ni kipindi cha kusakata rumba, michezo, shuhuda na changamoto zilizotolewa na wasanii katika mchakato wa ujenzi wa haki na amani duniani. Imetangazwa kwamba, mashindano ya mpira wa miguu kwa ajili ya amani, yatafanyika nchini Argentina, hapo tarehe 10 Julai 2016.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.