2016-05-28 07:31:00

Wakumbukwa wahamiaji na wakimbizi wanaokufa maji kila siku!


Maadhimisho ya Sherehe ya Ekaristi Takatifu wakati huu Mama Kanisa anapoadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu ni changamoto na mwaliko kwa waamini kuhakikisha kwamba, wanakuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vinavyoendeleza adhimisho la Fumbo la Ekaristi katika uhalisia wa maisha yao, kama kielelezo endelevu cha uwepo wa Kristo kati yao. Ni mwaliko wa kuwa ni mkate unaomegwa kwa ajili ya huruma na upendo kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. 

Hapa kwa namna ya pekee, wanakumbukwa wakimbizi na wahamiaji ambao kwa sasa ni changamoto kubwa kwa Jumuiya ya Kimataifa, kwani kuna makundi makubwa ya wakimbizi na wahamiaji wanaoendelea kufa maji na wengine kuteseka kutokana na hali ngumu ya maisha, wote hawa wanapaswa kuonjeshwa ukarimu wa Kanisa unaobubujika kutoka katika Fumbo la Ekaristi Takatifu.

Wale wote wasioguswa na mahangaiko ya wakimbizi na wahamiaji na kuwaacha kuendelea kufa maji kwenye tumbo la Bahari ya Mediterrania ni sawa na kumwacha Mwenyezi Mungu azame na kufa maji, kwani wahamiaji na wakimbizi wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Ni maneno ya uchungu yaliyotolewa na Kardinali Rainer Maria Woelki, Askofu mkuu wa Jimbo kuu Colon, nchini Ujerumani, wakati wa maadhimisho ya Sherehe ya Ekaristi Takatifu.

Kardinali Woelk alitumia mtumbwi wa wakimbizi na wahamiaji waliokolewa kutoka kwenye Bahari ya Mediterrania kama Altare ya maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu. Lengo ni kuendeleza mchakato wa uragibishaji wa upendo, mshikamano na ukarimu kwa wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta hifadhi na usalama wa maisha Barani Ulaya, ambako kwa sasa wanakumbana na pazia la chuma. Waamini wanaalikwa kuona sura na mfano wa Mungu kati ya wakimbizi na wahamiaji wanaokutana nao kila siku.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican








All the contents on this site are copyrighted ©.