2016-05-27 14:40:00

Papa na Rais wa Costa Rica wateta kuhusu: maisha, wakimbizi na dawa za kulevya


Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa tarehe 27 Mei 2016 amekutana na kuzungumza na Rais Luis Guillermo Solis Rivera wa Jamhuri ya Costa Rica, ambaye baadaye amekutana pia na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican aliyekuwa ameambatana na Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican.

Katika mazungumzo ya Baba Mtakatifu na mgeni wake, kwa pamoja wamepongeza uhusiano mzuri uliopo kati ya Vatican na Jamhuri ya Costa Rica sanjari na mchanago mkubwa unaotolewa na Kanisa Katoliki katika ustawi na maendeleo ya wengi, hususan katika sekta ya elimu, afya pamoja na majiundo makini yanayojikita katika tunu msingi za kibinadamu na kiroho, bila kusahau huduma ya upendo, kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Viongozi hawa wawili, baadaye wamejikita zaidi katika masuala msingi, hasa kuhusu umuhimu wa kulinda maisha ya binadamu bila kusahau changamoto ya wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji kwa wakati huu. Wamejadili pia kuhusu athari za biashara na matumizi ya dawa za kulevya. Mwishoni, wamegusia masuala ya kikanda pamoja na Jumuiya ya Kimataifa katika ujumla wake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.