2016-05-26 08:06:00

Yakhe huo si mchapo wa kuganga njaa! Ni Fumbo la Imani!


Maelezo ya utangulizi ya Injili ya leo katika Misale ya Waamini yanasema: “ Muujiza wa kuongeza mikate.” Maelezo hayo yanapotosha ujumbe halisi wa Injili. Kuna masimulizi sita katika Injili zote kuhusu kulishwa watu mikate – Mt 14:13-21; Mt 15:32-38; Mk. 6:30-44, Mk 8:1-10; Lk 9:10-17; Yoh 6:1-13, katika fasuli hizo hutaona pahala popote palipoandikwa kuwa Yesu aliongeza mikate. Bali yasemwa kuwa Yesu akaitwaa mikate waliyompa, akawakabidhi mitume wake  kuwagawia watu nao wakala, wakashiba na kusaza! Maneno hayo!

Suala la kuongeza mikate linaalika maswali mengi yasiyo na majibu. Mathalani mwinjili mmoja anasema kituko hiki kilikuwa jangwani, na mwingine anasema kilikuwa kwenye uwanda wa nyasi. Halafu yasemwa ilikuwa mikate saba na visamaki vichache, wengine ilikuwa mikate mitano na samaki wawili. Kisha baada ya kula walikusanya vikapu kumi na viwili vya mabaki, na pahala pengine vilikuwa vikapu saba tu. Idadi ya wau waliokula ni elfu tano na pengine watu elfu nne. Kwa hiyo takwimu hizi zinachanganya akili. Aidha tunaweza pia kujihoji, endapo Yesu aliongeza mikate kwa nini basi asiwarithishe mitume na wafuasi wake huo ujuzi kusudi waendelee kuwalisha watu fukara wanaokufa kwa njaa kila siku duniani? Kwa  hiyo tunaweza kusema kuwa lengo la masimulizi haya sita siyo kuongeza mikate.

Kumbe, lengo la masimulizi haya ni kutupatia mafundisho tofauti ya kitaalimungu, yenye kuhusiana na adhimisho la Fumbo la Ekaristi Takatifu. Sikukuu ya leo inatusaidia kuelewa masharti yaliyoko katika maisha ya kila siku, katika kuadhimisha Ekaristi na mwelekeo wa maisha yetu dhidi ya ulimwengu mamboleo. Aidha tunashirikishwa ujumbe unaohusu kugawana rasilimali ya ulimwengu huu kwa haki, upendo na mshikamano.

Ndugu zangu, lengo la Mungu kuweka raslimali katika ulimwengu huu ni kumfanya binadamu aishi maisha ya utu unaomstahili kiumbe wake. Kwa hiyo, Yesu anataka kutufundisha jinsi ya kugawanya vyema raslimali hii ili iwatoshee wote. Pazia la Injili ya leo linapofunguliwa unamkuta Yesu akihubiri juu ya Ufalme wa Mungu na anafanya kazi ya kuponya, kusamehe na kuwatekelezea wahitaji mahitaji yao msingi. “Na makutano walipojua walimfuata; akawakaribisha, akawa akisema nao habari za ufalme wa Mungu, akawaponya wale wenye haja ya kuponywa.” Ufalme huo unataka kuunda maisha bora kwa kila mwana ulimwengu. Aidha, maisha hayo hayanyesha kama mvua toka juu bali Yesu anataka kutufundisha sisi wenyewe kujijengea hayo maisha.

Fasuli inaendelea kusema: “Na jua likaanza kushuka” yaani ilikuwa jioni. Hapa tunaelezwa ratiba au mpangilio wa maisha ya wakristo wa kwanza. Kwamba jioni walifunga kazi ya siku na kukusanyika pamoja kuadhimisha Ekaristi. Siku hizi kwa kawaida, muda huo watawa hufunga kazi na kwenda kusali masifu ya jioni wanayoita Vespere, au kuadhimisha Misa takatifu. Basi jua lilipoanza kutua, mitume kumi na wawili walimkaribia Yesu aliyekuwa amezungumza siku mzima juu ya ufalme wa Mungu, ilikuwa kama vile wanamtaarifu kuwa muda umepita na afunge mazungumzo.

Wanamletea matatizo mawili ya msingi katika maisha. Wakamwambia:“Uage mkutano, ili waende katika vijiji na mashamba ya kandokando wapate mahali pa kulala na vyakula, maana hapa tulipo ni nyika tupu.” Matatizo hayo yanahusu chakula na mahali pa kulala. Njaa ya chakula haina maana njaa ya kimwili tu bali kuna njaa ya mambo mengi sana ikiwa ni pamoja na njaa ya kupendwa, njaa ya kutendewa haki, njaa ya  urafiki, njaa ya kueleweka vizuri, njaa ya kujua, njaa ya Mungu nk. Njaa hizo zote zinadai kushibishwa. Mungu ameweka kila aina ya raslimali inayoweza kushibisha aina hizo za njaa.

Hitaji jingine ni kulala. Neno la Kigiriki lililotumika hapa ni Katalysosin, maana yake ni mapumziko, yaani kukaribishwa. Hapa masuala muhimu ya kuyashugulikia ni kula na kukaribishwa au kupokewa. Kwa namna nyingine hapa Wakristo wanahamasishwa kuwa ni wakarimu, watu wanaoguswa na shida na mahangaiko ya jirani zao, changamoto makini inayotolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati huu wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu! Hiki ni kielelezo cha imani tendaji!

Hebu sasa fuatilia mapendekezo yanayotolewa na wafuasi na mawazo ya Yesu jinsi ya kukidhi mahitaji hayo muhimu. Pendekezo la kwanza la mitume hawa kumi na wawili kumhimiza Yesu: “Uage mkutano vijijini na mashambani wakapate chakula na pahala pa kulala” yaani waachie watu ili kila mmoja “akajiju” “Achana nao” Mzee hapa kula pini tu! Wakifika kijijini watajieleza wenyewe hukohuko halafu watajinunulia chakula. Mantiki hii ya kupata mahitaji ni ya masoko au ya maduka na biashara “Hakuna cha bure.” Na wengine wanasema, kula na kulipa ndio mtindo wa kisasa! Kabla ya kupata bidhaa budi kujadiliana bei.

Mfanyabiashara anaweza kuongeza gharama au hata kuficha bidhaa kusudi aongeze gharama na kupata faida. Katika masoko matajiri wanaendelea kuwa matajiri na fukara wanazidi kuwa fukara kiasi cha kukandamizwa chini utadhani ni soli ya kiatu, yaani hapa napata uchunu moyoni! Katika “kujiju” huko kuna patashika nguo kuchanika kati ya mwenye pesa na asiye nayo, kati ya mgonjwa na mzima, kati ya kijana na mzee. Mapato yake watu wa kawaida hawawezi kuijua paradisi hapa duniani bali matatizo tu. Kwa hiyo suala la masoko siyo suluhisho la matatizo ya njaa na ya mahali pa kulala, kwani hakuna anayekukaribisha na hakuna cha bure.

Yesu anawakejeli wafuasi wake kwa kuwadokezea jambo linalodai mchango wao zaidi anawaambia: “Wapeni ninyi chakula.” Hapo mitume wanaona wamegonga mwamba hivi wanadokeza mbinu nyingine ya kugawana raslimali. Wanamjibu Yesu: “Hatuna kitu ziadi ya mikate mitano na samaki wawili.” Idadi hii ya mikate na samaki ukijumlisha pamoja unapata saba iliyo namba kamili. Maana yake vyakula – au raslimali – iliyoko ni hiyo tu huwezi kufanya zaidi. Kwamba hata wao mitume wangependa kufanya tendo la upendo, lakini pembejeo na rasilimali haitoshi kukidhi mahitaji ya watu. Hapa mitume wanasema, “Mzee unga robo, hauwezi kufua dafu”. Aidha wanapendekeza kama mitume wenyewe wangeweza kuchangachanga pesa kidogo kisha kwenda kununua chakula na kuwagawia: “tusipokwenda tukawanunulie watu hawa wote vyakula.” Hapa linaingia wazo la kutoa ufadhili, yaani watu wanaweza wakaendelea na namna yao ya kutatua matatizo kwa njia ya masoko, mradi tu wale matajiri watoe ufadhili. Yesu anapoona kwamba njia hizi zote hazifai katika kuujenga ufalme wa Mungu hapo anaingilia kati na kuwatolea uvivu. Anawapa mitume kazi ya kuwapanga watu anawaambia: “Waketisheni watu kwa safu, kila safu watu hamsini.” Neno hili waketisheni watu kwa kigiriki ni kataklinate lenye maana ya kupumzisha yaani kuwaketisha watu wakae kwa “mkao wa kula.”

Hivi wanafunzi wa Yesu wanapewa kazi ya kuwakaribisha (kuwapokea) kuwapumzisha ili wajinyoshe vizuri, halafu kuwatumikia. Kisha Yesu “akaitwa ile mikate mitano na wale samaki wawili, akatazama juu mbinguni, akavibariki, akavimega, akawapa wanafunzi wake ili waandikie mkutano.” Kutoa shukrani maana yake ni kutambua kwamba vyakula na mahitaji yote ya binadamu hutoka kwa Mungu. Sisi sote ni wageni na wagawaji tu wa mali hiyo kwa wengine.

Yesu anamega mkate na kuwapa wanafunzi na hapo ndipo kuna muujiza utokanao na tendo la kugawana chakula alichotupa Mungu. Muujiza ni huu kwamba: “Wakala, wakashiba wote.” Huu ndiyo muujiza utokanao na kupokea upendo wa watoto wa Mungu. Yesu ametufundisha kutumia vyema raslimali ya ulimwengu huu na muujiza huo tunaoweza kuufanya sisi wenyewe.  Kuhusu mabaki ya mikate iliyokusanywa yasemwa: “na katika vipande vilivyowabakia walikusanya vikapu kumi na viwili.” Hapa tunafundishwa kutojilimbikizia mali bila kutumia au kutapanya mali ovyo ikiwa ni pamoja na vyakula, nyumba, magari, vitu, simu, fedha nk.

Kwa hiyo tunafundishwa kutumia mali ya ulimwengu huu kwaheshima, huruma na upendo. Maskini ndiye mteja anayetukomboa kwani anatufundisha tuweze kutenda tendo la huruma na upendo. Hapa mkazo ni kumwilisha matendo ya huruma: kiroho na kimwili, ili kushibisha njaa ya kiroho na kiu ya uzima wa milele! Baada ya kupata ujumbe huu tunaweza sasa kulielewa fundisho la Fumbo la Ekaristi Takatifu. Siku ya karamu ya mwisho Yesu “Alichukua mkate akasema huu mkate ni mimi, chukueni kuleni.” Kwamba, Yesu amechagua mkate kuwa ufupisho wa maisha yake ili kuonesha kwamba maisha yake yote yalikuwa mkate hata kipande kidogo aliotolewa kama zawadi kwa binadamu. Anasema msiweke huo mkate pahala fulani, bali kuleni na hivi myapokee maisha yangu na kuyaishi, yaani mnipokee mimi, pokeeni mantiki mapya yanayowapeleka kwenye paradisi mpya ya hapahapa duniani.

Kwa hiyo Yesu ametufundisha kujenga maisha halisi. Anayekula mkate anakaribishwa kuingia katika mantiki hii ya upendo na huruma ya Mungu kwa binadamu; Mantiki ambayo imeoneshwa na kushuhudiwa na Yesu kwa njia ya maneno na matendo yake. Aligusawa zaidi na mahangaiko ya binadamu, akawaganga na kuwaponya magonjwa yao; akawasamehe na kuwaondolea dhambi zao; akawalisha kwa ngano safi na kuwanywesha asali safi itokayo mwambani. Hii ndiyo maana ya Ekaristi, yaani kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma makini ya huruma na upendo kwa jirani! Yaani ni kuwa Ekaristi, mkate unaomegwa kwa ajili ya kuendeleza Injili ya huduma, upendo na maisha.

Na Padre Alcuin Nyirenda, OSB








All the contents on this site are copyrighted ©.