2016-05-26 13:56:00

Viongozi wakuu wa G7 wakacha mkutano wa UN huko Istanbul!


Umoja wa Mataifa umeridhishwa na mafanikio yaliyopatikana kwenye mkutano wa kwanza kimataifa wa msaada wa kibinadamu uliohitimishwa hivi karibuni huko Istanbul, Uturuki, ingawa haukuhudhuriwa na viongozi wengi wakuu kutoka kwenye kundi la Nchi saba Tajiri duniani, maarufu kama G7. Kunahitajika kiasi cha dolla za kimarekani millioni 240 kila mwaka ili kukabiliana na majanga yanayowakabili watu wengi duniani.

Kiasi hiki cha fedha kinaweza kupatikana ikizingatiwa kwamba ni kiasi tu cha asilimia 1% ya gharama zote za ununuzi wa silaha za kijeshi duniani. Asilimia 80% ya matukio yanayosababisha majanga duniani ni yale ambayo yanasababishwa na binadamu mwenyewe! Hapa kuna vita, kinzani na mipasuko ya kijamii, kisiasa na kidini. Hata wale viongozi ambao hawakuhudhuria mkutano huu, wanawajibika kikamilifu katika kusaidia kupambana na majanga yanayomwandama mwanadamu katika ulimwengu mamboleo na hapa hakuna kiongozi anayeweza kukwepa uwajibikaji huu.

Mwezi Septemba, Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa atatoa taarifa kwenye Baraza kuu la Umoja wa Mataifa. Jumla ya wajumbe kutoka katika nchi 173 wameshiriki kati yao kulikwepo wakuu wa nchi na serikali 55, idadi kubwa ya wajumbe kuwahi kuhudhuria katika mkutano wa Umoja wa Mataifa ambao kwa mara ya kwanza umepembua kwa kina na mapana misaada ya kiutu kwa watu wanaoteseka kutokana na vita, majanga asilia pamoja na kinzani za kijamii, kisiasa na kidini.

Jumuiya ya Kimataifa imeweza kuchambua sababu msingi zinazopelekea mateso na mahangaiko kwa mamillioni ya watu duniani kwa wakati huu, ili kujiwekea mbinu mkakati wa kupambana na changamoto hizi ili kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu. Mkazo ni kulinda, kuheshimu na kutekeleza sheria za kimataifa katika masuala ya vita na kinzani za kijamii. Mkutano huu umekuwa ni fursa ya kuwakutanisha wadau mbali mbali ili kujadiliana na hatimaye, kuibua mbinu mkakati wa kuwahudumia wahanga wa maafa mbali mbali duniani.

Wajumbe wamesikiliza shuhuda za mateso na mahangaiko ya watu duniani na sasa ni wakati wa kutekeleza maazimio yaliyofikiwa kwa njia ya vitendo; kwa kuchangia gharama za misaada inayotakiwa ili kusikiliza na kujibu kikamilifu kilio cha mateso na mahangaiko ya watu duniani, kwa kuheshimu, kulinda na kudumisha utu na heshima yao kama binadamu sanjari na haki zao msingi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.