2016-05-26 15:27:00

Papa :kudumu katika sala na maombi huimarisha imani kwa Mungu


Baba Mtakatifu Francisko katika Katekesi yake kwa mahujaji na wageni , aliendelea kutafakari juu ya Mwaka Mtakatifu wa Huruma , safari hii akirejea mfano wa Hakimu dhalimu na Mjane kama ilivyoandikwa katika Injili ya Luka 18:8. Alisema, katika mfano huu, mna fundisho muhimu la kusali daima bila kuchoka. Na kwamba mfano huu nimwaliko unaotutaka kuwa watu wa sala na kuomba wakati wote kama wajibu na si hiari ya kuchagua.

Papa aliendelea kutoa mafundisho juu ya mfano huu , wa hakimu dhalimu , asiyemcha Mungu, mtu mwenye moyo mgumu , asiyeheshimu   wengine , wala kuwa na aibu ya kufanya kama anavyotaka kwa kuziweka sheria mkononi mwake , kwa manufaa yake mwenyewe ,  akiwmeleza kwamba, anawakilisha kundi la watu kama hao waliopo hata leo hii , watu wenye mamlaka wanaotenda kama wanavyotaka kwa manufaa yao bila kuhurumia wengine.   Na  alimrejea mwanamke mjane Mcha Mungu anayetafuta haki yake , akimtaja kwamba, anawakilisha kundi la watu dhaifu wanaotafuta kutendewa haki , kama ilivyo hata leo hii kwa wajane wengine, watoto yatima, wahamiaji na wakimbizi na makundi mengine yanayoishi katika mazingira magumu zaidi katika jamii wanaotafuta kulindwa na sheria , ili maisha yao yawe ya kawaida kama watu wengine au katika  kuondokana na dimbwi la umaskini, unyonge na upweke.

Alieleza  bidii ya  mjane huyo, mtu wa haki lakini myonge ambaye  hakuchoka  kuomba  haki yake kwa  hakimu dhalimu, aliendelea kuomba haki hadi usugu wa hakimu dhalimu kulainishwa na ombi lake la siku, na kupata  haki yake. Papa alisema ,  Hakimu huyo dhalimu hakumpa haki mjane huyo kwa sababu alimwonea huruma,  au kutoa hukumu kwa kuwa dhamiri yake ilimtuma kufanya hivyo, lakini hasa kwa sababu alitaka kujiepusha na kile alichokiona kama ni usumbufu na kusema” nitampa haki yake ili asiendelee kunisumbua”.  

Papa aliutazama kwa makini mfano huu ambamo Yesu anasema , ikiwa mjane alidumu katika kumwomba hakimu dhalimu mara kwa mara hadi madai yake kusikilizwa , je si zaidi kwa Mungu ambaye ni mwema na Baba wa haki kwa watu wake wateule wanaomlilia mchana kutwa na usiku. Baba Mwema ambaye hawafanyi watu wake wasubiri kwa muda mrefu , ambaye mara huwapa jibu la kweli  mara moja kama ilivyoandikwa katika aya ya 7,8. Hiyo ndiyo sababu Yesu anatuhimiza kuomba bila kukoma.

 Kwa maelezo hayo, Papa alitoa wito kwa watu wote kujitahidi  kusali bila kuchoka na bila  kuvunjika moyo na hasa pale  inapoonekana  kama vile maombi hayasikilizwi. Kupitia Maandiko MatakatifuYesu anatuhakikisha kwamba Mungu si kama hakimu dhalimu, Mungu hutoa jibu la haraka kwa watoto wake , ingawa hii haina maana kwamba Mungu atoe jibu katika muda tunaotaka sisi , lakini Yeye hutoa jibu katika wakati anaoona inatufaa.

Aidha Papa Francisko alionya kwamba,  kuwa mtu wa sala na maombi si kuwa mshirikina au mchawi, lakini maombi huimarisha imani yetu kwa Mungu na kutuweka karibu zaidi nae. Hutusaidia kujiweka chini ya miguu yake hata kama hatuelewi mapenzi yake yatakavyokuwa.  Papa alieleza na kutoa mwaliko wa kuutazama mfano wa Yesu kuwa mtu wa maombi. Alisema , Yesu mwenyewe daima alidumu kwenye maombi. Yesu aliomba sana , tena wakati mwingine kwa kilio cha  machozi , ili Mungu amwokoe na kifo , lakini alisema “si kama nitaka mimi lakini katika utimilifu wa mapenzi yako” . Mapenzi ya Mungu ilikuwa Kristo amwage damu yake Msalabani kwa ajili ya kuleta wokovu kwa watu wote. Na ndivyo ilivyosali Yesu akiwa  msalabani ( Matayo 26:39).

Papa alikamilisha maelezo yake na swali lililotaka kujua lini  mwana wa Mtu atakuja tena dunani, akisema swali hili , linatoa onyo kwetu sote, kudumu katika  maombi. Kukesha ktika maombi  si kwa manufaa ya mwili lakini kwa ajili ya kudumisha imani. Imani yenye kulishwa na hamu ya kuja kurudi kwa mwana wa Mtu. Na kwamba, katika sala na maombi tunapata hisia za huruma ya Mungu , kama vile Baba anayekutana na watoto wake kwa upendo kamili , upendo wenye huruma . 








All the contents on this site are copyrighted ©.