2016-05-25 08:13:00

Kabla ya kuanzisha Shirika la kitawa ngazi ya Kijimbo: Ushauri unatakiwa!


Baba Mtakatifu Francisko baada ya kuzungumza  kwa kina na mapana na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican hivi karibuni, ameamua kwamba, kuanzia tarehe 1 Juni 2016 kabla ya kuanzisha mchakato wa kuunda Shirika la Kitawa au kazi za kitume kwa ngazi ya kijimbo, itatakiwa kwanza kupata ushauri kutoka Vatican hali kadhalika kufutwa kwa Shirika la kitawa au kazi za kitume, utatakiwa kwanza ushauri kutoka Vatican.

Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na Kazi za kitume linatambua na kukiri kwamba,  kila Shirika la kitawa na kazi za kitume ni zawadi ya Roho Mtakatifu kwa Kanisa zima, ili kuondokana na kishawishi cha kuanzisha Mashirika mapya ya kitawa katika ngazi ya kijimbo, bila ya kuwa na mang’amuzi mapana zaidi yanayokubali uhalisia wa karama mpya ndani ya Kanisa, inayopembua na kubainisha mambo msingi yatakayofumbatwa katika maisha haya kwa njia ya nadhiri za: Utii, Ufukara na Usafi kamili sanjari na kumwendeleza mtawa mwenyewe, imeamriwa kwamba, ni vyema kuzingatia Sheria za Kanisa namba 579 inayosisitizia umuhimu wa kuomba ushauri kabla ya kuanzisha Shirika jipya la kitawa katika ngazi ya Kijimbo.

Ufafanuzi huu umetolewa hivi karibuni na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican baada ya mazungumzo ya kina na Baba Mtakatifu Francisko hapo tarehe 11 Mei 2016.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.