2016-05-25 10:08:00

Ekaristi Takatifu: kifungo cha umoja, upendo na udugu!


Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu anawakumbusha waamini kwamba, Yesu aliguswa kwa namna ya pekee na mahangaiko na uchovu wa makundi ya watu waliomfuata kusikiliza Habari Njema ya Wokovu, akawaonea huruma na kuwaponya magonjwa yao! Na kwa mikate michache na samaki wawili, akawashibisha njaa yao: kiroho na kimwili. Huruma ni uhai thabiti wa maisha na utume wa Kanisa.

Katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, Mama Kanisa anatumwa kusikiliza kilio cha maskini na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii; kuganga na kuponya majeraha ya maisha ya mwanadamu kiroho na kimwili kwa kwa mafuta ya faraja na huruma; kwa mshikamano na kujali zaidi; mambo yanayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Kwa njia hii, Wakristo watakuwa kweli ni Ekaristi kwa jirani zao, Fumbo ambalo ni chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Ekaristi Takatifu ni Sakramenti ya Upendo, chakula cha kweli kilichoshuka kutoka mbinguni!

Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Siku kuu ya Ekaristi Takatifu “Corpus Domini”, Alhamisi, tarehe 26 Mei 2016 majira ya jioni, anatarajiwa kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane wa Laterano na baadaye kuongoza maandamo ya Ekaristi Takatifu kuelekea kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria mkuu, lililoko mjini Roma. Huu ni mwaliko kwa waamini kuungama na kushuhudia imani ya Kanisa katika Fumbo la Ekaristi Takatifu. Hapa Kanisa linamwamini na kumwabudu Yesu Kristo mwanakondoo wa Mungu na sadaka ya kweli!

Mama Kanisa anatukumbusha kwamba, Ekaristi Takatifu ni chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Kwa njia ya Roho Mtakatifu waamini wanafanywa kuwa jamaa moja wale wote wanaoshiriki Mwili na Damu ya Kristo! Ekaristi Takatifu ni chakula cha njiani katika maisha ya Kikristo. Ikumbukwe kwamba, Ekaristi Takatifu na Sakramenti ya Upatanisho ni Sakramenti pacha zinazomwezesha mwamini kuchuchumilia na kuambata upendo na huruma ya Mungu. Ekaristi Takatifu ina uhusiano wa dhati na Sakramenti nyingine za Kanisa. Kumbe, hili ni Fumbo linalopaswa kuadhimishwa kwa ushiriki mkamilifu na heshima kuu kwa kutambua kwamba, Kristo ndiye mhusika mkuu.

Maadhimisho ya Sherehe ya Ekaristi Takatifu yanaambatana na Ibada ya Kuabudu na Maandamano ya Ekaristi, ushuhuda unaoonesha uwepo endelevu wa Kristo kati ya watu wake. Ekaristi Takatifu ni Fumbo linalopaswa kumwilishwa katika uhalisia wa maisha ya waamini, kielelezo makini cha imani tendaji! Maadhimisho ya Sherehe ya Ekaristi katika Mwaka wa huruma ya Mungu, iwe ni fursa kwa waamini kuwa kwelini mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu; tayari kutoka kimasomaso kuinjilisha kwa njia utakatifu wa maisha; kwa kujikita katika ari na mwamko wa kimissionari, kwani Ekaristi Takatifu ni mkate wa uzima wa milele hata kwa walimwengu. Wakristo watambulikane katika kuumega mkate, changamoto ya kuadhimisha, kuabudu na kulitafakari Fumbo hili kubwa katika maisha na utume wa Kanisa; kielelezo cha huduma na mshikamano kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii! Maadhimisho ya Sherehe ya Ekaristi kwa mwaka huu, yalete chachu ya huruma, mapendo, uadilifu na utakatifu wa maisha!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.