2016-05-25 11:17:00

Ekaristi Takatifu chemchemi ya huruma na upendo wa Mungu!


Ekaristi Takatifu ni Mwili na Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mungu kweli na mtu kweli katika maumbo ya mkate na divai. “Mwokozi wetu, katika Karamu ya mwisho, usiku ule alipotolewa, aliweka sadaka ya Ekaristi ya Mwili wake na Damu yake. Alifanya hivyo ili kuendeleza sadaka ya msalaba siku zote mpaka atakaporudi, kusudi amwachie Bibi Arusi mpendwa, yaani Kanisa, ukumbusho wa kifo chake na ufufuko wake: sakramenti ya upendo, umoja, kifungo cha mapendo, karamu ya Pasaka ambamo Kristo huliwa, na roho hujazwa neema, na ambamo tunapewa amana ya uzima wa milele” (KKK 1323).

Pedagogia ya kibiblia inatuandaa taratibu kulielewa fumbo hili linaloanza kuaguliwa kuanzia katika Agano la Kale hadi linapoonekana kwa uhalisia katika Agano Jipya kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, Yeye aliye mzima katika mafumbo haya ya mkate na divai. Ekaristi Takatifu ni mlo wa kipasaka. Wakati wa adhimisho la Ekaristi na kwa namna ya pekee wakati wa Sala ya Utangulizi ama prefasio Kanisa zima linafanya ukumbusho ‘anamnesis’ wa mateso, ufufuko na kurudi kwake mbinguni kwa utukufu ( Rej KKK 1354). Ukumbusho huu unaturudisha nyuma na kutafakari Pasaka ya Wayahudi ambapo ilikuwa ni kumbukumbu ya kukombolewa kutoka katika utumwa wa Misri.

Wakati wa adhimisho hili Wayahudi walikula mikate isiyotiwa chachu, mkate ambao ulitengenezwa kwa ngano mpya isiyotiwa chachu, yaani bila kitu chochote kinachotokana na mavuno ya mwaka uliotangulia na hivyo ni ishara ya maisha mapya yanayoanza (Rej Kut 12:1nk). Mkate uliendelea kuwa ndicho chakula chao wakiwa safarini hadi walipofika katika nchi ya Ahadi. Wakiwa Jangwani walishushiwa mkate kutoka mbinguni, ni Mungu mwenyewe ndiye aliwalisha kama anavyothibitisha Mzaburi akisema “Nimewalisha kwa unono wa ngano na kuwashibisha kwa asali itokayo mwambani” (Zab 80:17).

Katika Agano Jipya Kristo anaendeleleza ukarimu huo wa kimbingu kwa kuwalisha watu wengi kwa mikate na samaki wachache. Kitendo hiki cha Kristo kilimpatia fursa ya kuwaingiza taratibu katika kukielewa chakula cha kiroho ambacho ni Mwili na Damu yake. Sura ya sita ya Injili ya Yohane inaliweka vizuri fundisho hilo. Kristo anaanza fundisho hili kwa kuwaonya kutotegemea tu chakula cha kidunia akiwaambia msikitendee kazi chakula chenye kuharibika, bali chakula kidumucho hata uzima wa milele, ambacho Mwana wa Adamu atawapa” (Yoh 6:27). Kristo anaendelea kuonesha kuwa chakula hicho ni kutoka mbinguni kwa ajili ya uzima wa ulimwengu tofauti na ngano ile au mana ile waliyoila Baba zao Jangwani wakafa (Rej Yoh 6: 29 – 34). Baada ya hapo ndipo anajitambulisha Yeye mwenyewe kuwa ndiye chakula hicho kitokacho mbinguni (Rej Yoh 6:35 – 51) na hivyo kila aulaye mwili wake na kuinywa damu yake ataishi milele (Rej Yoh 6: 51 – 58).

Sehemu hii ya Injili ya Yohane imetuandaa kuingia katika Fumbo la Pasaka ambalo ndani mwake Kristo anaiweka Ekaristi Takatifu kuwa Sakramenti ya Mwili na Damu yake na hivyo mkate huu tunaouona katika macho yetu ya kibinadamu unageuzwa kuwa mwili wake Mtakatifu sana. Yeye mwenyewe alitwaa mkate akasema “Huu ndio mwili wangu unaotolewa kwa ajili yenu” (Lk 22:19) na hivyo hivyo kwa kikombe akasema “kikombe hiki ni agano jipya katika damu yangu inayomwagika kwa ajili yenu” (Lk 22:20). Chakula hicho cha kibinadamu kinapata hadhi ya kuwa chakula cha kimbingu kwani kinageuka kuwa Mwili na Damu ya Kristo anayejitoa kwa ajili ya upendo wetu sisi.

Imani yetu juu ya asili ya Kristo kwamba yeye ni Mungu kweli na mtu kweli ndiyo inatupatia uhakika juu ya uhalali na mamlaka yake katika kugeuza mkate kuwa Mwili wake na divai kuwa Damu yake. Kama Kristo Mwenyewe amesema ‘huu ni mwili wangu’ nani atakayethubutu kutilia shaka kwamba ni mwili wake? Imani yetu katika Ekaristi Takatifu inajengeka katika maneno ya Kristo mweyewe wakati wa karamu ya mwisho. Mmoja anapotoka nje ya imani hiyo ni vigumu sana kuweza kuonja utamu na maana yake. Tangu kale Mababa wa Kanisa walionya juu ya umuhimu huo wa imani. Mtakatifu Ireneo wa Lyon alionesha waziwazi kuwa wazushi wa kignostiki wasingeweza kuwa na imani katika Ekaristi Takatifu akisema: “wangeweza vipi kuwa na hakika kwamba mkate wa shukrani uliotolewa ni Mwili wa Bwana na kikombe Damu yake wakati hawakutaka kumthibitisha Yeye kuwa ni Mwana wa Muumba?”

Mwinjili Luka ambaye ametupatia simulizi la tukio hilo la kuwekwa kwa Ekaristi Takatifu  anaendelea kutuonesha udumifu wa chakula hiki kwa maneno ya Kristo mwenyewe ambaye anasema “fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu” (Lk 22:19b). Pengine maswali kadhaa yanaweza kutujia kichwani mwa kila mmoja wetu: Kwa nini tumkumbuke? Ukumbusho wake huo utatusaidia nini? Je, Ekaristi Takatifu inao mchango wowote katika maisha ya mkristo? Bila shaka Sakramenti hii kama tunavyofundishwa na Katekisimu ya Kanisa kuwa ni “chemchemi na kilele cha maisha yote ya kikristo ... kwani ndani ya Ekaristi takatifu mna kila hazina ya kiroho ya Kanisa, yaani Kristo mwenyewe, Pasaka wetu” (KKK 1324). Kwa mantiki hiyo uhai na ustawi wa Kanisa unajikita katika maadhimisho ya daima ya Sakramenti hii ambamo kwa hilo tunaendelea kuufanya uwepo wake kuwa hai katikati yetu na kuendelea kutufunulia upendo wa Mungu.

Katika mwaka huu wa Jubilei ya Huruma ya Mungu ufunuo huo wa Upendo wa Mungu tunauonja zaidi katika huruma yake ambayo tumeipokea kwa kupitia fumbo la Pasaka, yaani mateso, kifo na ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo. Ekaristi Takatifu ni Chemchemi ya huruma hii ya Mungu. Chakula hiki cha kimbingu ni nyenzo muhimu ya kutuunganisha na uso wa Mungu mwenye huruma. Inatosha kurejea katika aya chache za Bola la Baba Mtakatifu Misericordiae Vultus kuona jinsi Askofu huyu mkuu wa Roma na Halifa wa Petro anavyotuonesha muunganiko wa Ekaristi Takatifu Huruma ya Mungu na zaidi hitajiko lake katika jamii yetu leo hii na kwa vizazi vyote. Waraka huo unaanza kwa kusema kwamba Yesu “Kristo ni uso wa huruma ya Baba. Katika neno hili upo ufupisho sahihi wa fumbo zima la imani ya kikristo. Huruma imepata kuwa hai na yenye kuonekana katika Yesu Mnazareti, na hata ikafikia kilele chake katika Yeye” (MV 1).  Ekaristi Takatifu inafunua kwa namna iliyotukuka zaidi huruma hii. Kristo “alipokuwa akisimika Ekaristi kama ukumbusho wake wa milele na sadaka yake ya Pasaka, aliweka hili tendo kuu la ufunuo kama alama ya huruma yake. Ndani ya kifungu hikihiki cha huruma, Yesu aliingia katika mateso na kifo chake, kwa kudhamiria lile fumbo kuu la upendo ambalo angelikamilisha msalabani” (MV 7).

Huruma hii ya Mungu inatuunganisha na Watakatifu wa mbinguni. Baba Mtakatifu anaendelea kutufundisha kwamba: “Kanisa linaishi ushirika wa Watakatifu. Katika Ekaristi ushirika huo, ulio zawadi ya Mungu, unakuwa kama muungano wa kiroho unaotuunganisha sisi waamini na Watakatifu na Wenye Heri ambao idadi yao haihesabiki (rej. Ufu 7:4). Utakatifu wao unausaidia udhaifu wetu; kwa namna hiyo Mama Kanisa linaweza kwa sala yake na maisha yake kuusaidia udhaifu wa wengine kwa nguvu ya utakatifu wa wengine. Basi, kuiishi rehema katika Mwaka Mtakatifu kunamaanisha kuisogea huruma ya Baba tukiwa na uhakika kwamba msamaha wake unaenea juu ya maisha yote ya mwamini. Rehema ni kufahamu na kufaidi na utakatifu wa Kanisa ambalo linawagawia watu wote manufaa ya ukombozi wa Kristo, ili msamaha ufikie mpaka kilele kinachofikiwa na upendo wa Mungu. Tuiishi kwa dhati kabisa Jubilei tukimwomba Baba atujalie msamaha wa dhambi na uenezaji wa rehema yake yenye huruma” (MV 22).

Kwa kuhitimisha tafakari yetu hii ni vema basi kuangalia matunda yanayotarajiwa na Sakramenti hii katika Kanisa na kwa nafasi ya pekee katika Mwaka huu wa Jubilei ya Huruma ya Mungu. Kwa nafasi ya kwanza ni kuupokea uzima wa kimungu ndani mwetu. Tunayempokea katika Ekaristi ni Kristu mzima, Mungu kweli na mtu kweli. Tunaunganika naye na kwa njia ya chakula hiki na hivyo kuwa mtendaji mkuu wa maisha yetu ya kila siku. Muunganiko huu unatushurikisha kwa nafasi ya kwanza huruma yake kwa kuwa Yeye anakuwa ni ufunuo wa upendo wa Mungu kwetu wanadamu na pia kututia shime katika magumu ya safari tuwapo njiani kuelekea ukamilifu.

Muunganiko wetu na Kristo unaotupatia uzima wa kimungu unatufanya kuwa wamoja. Tunaunganishwa na Mwili wake na Damu yake. Chakula hiki kinatufanya kuwa kaka na dada ndani ya jamii ya kibinadamu. Changamoto inakuja kwetu sisi tunaobahatika kupokea haiba hii hasa pale tunapoonesha tabia mbalimbali zinazoashiria kutengana. Moja ya majukumu makubwa tunayopewa na adhimisho la Jubilei ya Huruma ya Mungu ni kujenga jamii ya wanadamu yenye umoja. Hivyo sisi wanakanisa tunayo changamoto hii ya kuifanya jamii ya mwanadamu ionje maisha ya kiekaristia kwa kuishuhudia huruma ya Mungu ikistawi kati ya watu. Mwanadamu aonje kupendwa, kujaliwa, kusaidiwa, kuonywa kidugu na mengine mwengi ambayo yatasaidia zaidi katika kujenga na si katika kuisambaratisha hadhi ya mwanadamu.

Katekisimu ya Kanisa Katoliki inatupatia jukumu lingine muhimu tunalopokea kama matunda ya Ekaristi Takatifu, Sakramenti ambayo inafunua huruma ya Mungu. Jukumu hilo ni lile la kufungua macho yetu kwa wahitaji. “Ili kupokea katika kweli Mwili wa Kristo na Damu ya Kristo iliyotolewa kwa ajili yetu, lazima kumtamani Kristo ndani ya ndugu zake walio maskini sana na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii: Umeonja Damu ya Bwana na bado humtambui ndugu yako ... unaifedhehesha meza hii” (KKK 1397). Sakramenti hii inatualika kufunua mioyo yetu kwa wahitaji wa kimwili na kiroho. Tunafanywa kuwa kile tunachokipokea, tunaalikwa kuudhirisha upendo tunaoupokea katika Ekaristi kwa watu wengine. Matendo yetu ya huruma kwa wahitaji yanatiwa chachu na Sakramenti hii na hivyo uadhimishaji wetu unakamilishwa na upendo wetu kwa wenzetu.

Imeandaliwa na Padre Joseph Peter Mosha.








All the contents on this site are copyrighted ©.