2016-05-24 13:56:00

Uchaguzi umekwisha, sasa jengeni umoja wa kitaifa!


Kardinali Christoph Schonborn, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Austria amemtumia salam za pongezi Rais Alexander Van der Bellen aliyeshinda kwa kishindo katika uchaguzi mkuu uliohitimishwa Jumapili iliyopita, tarehe 22 Mei 2016. Katika ujumbe wake, Kardinali Schonborn anakaza kusema, kampeni na uchaguzi umekwisha, sasa Rais anapaswa kuwaunganisha wananchi wote wa Austria ili kuwa kitu kimoja. Ni matumaini yake kwamba, wananchi wa Austria wataonesha ukomavu mkubwa wa kidemokrasi, tayari kushirikiana na wote ili kujenga nchi yao! Hii ndiyo changamoto ya kwanza kwa Rais mpya.

Kardinali Schonborn anasema, Familia ya Mungu nchini Austria inapaswa kutafuta, kujenga na kudumisha heshima na uwajibikaji; wanasiasa wajenge utamaduni wa kuwaheshimu wananchi na kwamba, ushiriki mkubwa ulioneshwa na wananchi wa Austria katika mchakato wa kampeni na upigaji kura ni kielelezo makini kwamba, wanaheshimu dhamana ya Rais katika ustawi na maendeleo ya nchi yao. Ni wajibu wa wanasiasa kuonesha pia ukomavu kwa kushirikiana na wote pasi na ubaguzi kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya nchi.

Kardinali Schonborn anakumbusha kwamba, Rais ameshinda kwa kura chache, hali inayohitaji ukomavu wa kisiasa ili kuweza kushirikiana na wanasiasa wengine kwa ajili ya kuendeleza nchi yao, kwa kutafuta na kuendeleza yale mambo yanayowaunganisha zaidi kuliko yale yanayowatenganisha kama nchi. Kardinali Schonborn anamwombea Rais mpya heri, baraka na neema katika maisha na utume wake, katika mchakato wa kuiendeleza Austria katika ustawi, uhuru, maendeleo pamoja na kutekeleza dhamana na utume wake katika Umoja wa Ulaya na ulimwengu katika ujumla wake!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.