2016-05-23 14:35:00

Wakuu wa nchi wanakutaka Lusaka, kujadili nishati na mabadiliko ya tabianchi!


Waziri mkuu Kassim Majaliwa ameondoka nchini Tanzania Jumatatu, Mei 23, 2016 kwenda Lusaka, Zambia kuhudhuria Mkutano wa 51 wa Mwaka wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (51stAnnual Meeting of the Board of Governors of the African Development Bank - AfDB) utakaofanyika, Jumanne, Mei 24, 2016. Waziri Mkuu anahudhuria mkutano huo kwa niaba ya Mheshimiwa Rais, Dk. John Pombe Magufuli.

Mkutano huo ambao utafunguliwa na Rais wa Zambia, Edgar Lungu utajadili masuala ya Nishati na Mabadiliko ya Tabianchi. Pia utahudhuriwa na Marais Idriss Deby wa Chad, Paul Kagame wa Rwanda na Uhuru Kenyatta wa Kenya. Nigeria itawakilishwa na Makamu wake wa Rais, Yemi Osinbajo huku Msumbiji ikiwazilishwa na Waziri wake Mkuu, Carlos Agostinho do Rosário. Watu maarufu waliothibitisha kuhudhuria mkutano huo ni pamoja na Kofi Annan, Ashish Thakkar, John Kufuor, Mary Robinson, Mo Ibrahim, Nancy Lee, Ngozi Okonjo-Iweala na Tony Elumelu.

Mkutano huo utakaofanyika kwenye kituo cha mikutano cha kimataifa cha Mulungushi (Mulungushi International Conference Centre) utahudhuriwa na washiriki zaidi ya 5,000 kutoka nchi 54 ambao ni wanachama wa benki hiyo, washiriki kutoka nchi 26 ambazo si za bara la Afrika (non-regional member countries), wawakilishi wa mashirika ya kimataifa, wadau wa maendeleo na wawakilishi wa asasi za kiraia. Wengine ni Mawaziri wa fedha, biashara na uchumi na wataalamu kutoka vyuo vikuu.

Waziri Mkuu wa Tanzania amefuatana na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Asantu Kijaji, wachumi kadhaa pamoja na wataalamu wa sekta ya fedha.

Na Ofisi ya Waziri mkuu wa Tanzania.








All the contents on this site are copyrighted ©.