2016-05-23 09:31:00

Papa: Utatu Mtakatifu,unashuhudia ambapo kuna upendo kuna Mungu


(Vatican Radio) Jumapili iliyopita, nyakati za adhuhuri, mbele ya maelfu kwa maelfu ya waamini Baba Mtakatifu Francisko alisema , ”Sikukuu ya Utatu Mtakatifu, inatoa mwaliko kwamba, maisha yetu ya  kila siku, yawe  chachu ya umoja, faraja na huruma.  Baba Mtakatifu Francisko, alileleza katika hotuba yake fupi  kabla ya sala ya Malaika wa Bwana, akilenga katika adhimisho la  Jumapili  ya Utatu Mtakatifu.  Maelfu kwa maelfu ya waamini walikusanyika katika uwanja wa Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro Vatican, kusali sala ya Malaika wa Bwana pamoja na Papa .

Akivuviwa na  somo la Injili, Papa alisema, Utatu Mtakatifu,  unatualika kuishi  roho wa ushirika, huduma  na huruma , kama dawa kwa ubinadamu uliojeruhiwa na ukosefu wa haki ,ufisadi,  chuki na choyo .   Aidha Papa  kwa namna ya kipekee , aliutaja Mkutano wa Dunia juu ya ubinadamu unaofanyika Istanbul Uturuki , ambamo Jimbo la Papa linawakilishwa na Kardinali Pietro Parolin.  Na pia aliwakumbuka Wakatoliki nchini China ambao Jumanne ya 24 Mei wanaadhimisha  , Sikukuu ya Mama Bikira Maria  Msaada wa Wakristo.

Papa aliendelea  kueleza juu ya  mahusiano haya ya nafsi tatu za Mungu katika mpango wake wa ukombozi akisema , hatuwezi kuzitenganisha nafsi hizi katika mpango wa ukombozi  katika maana kwamba , Mungu alimtuma mwanae nafsi ya pili kuja dunia kumkomboa binadamu kwa kifo chake na baada ya ufufuko wake anawahakikishia wanafunzi wake kwamba hawatabaki peke yao lakini atawaacha na Roho Mtakatifu. Kumbe Roho Mtakatifu anakuwa ni kiongozi wetu mpya katika hali mpya ya kuelekea Uzima wa milele ambako kuna Mungu Baba na Mungu mwana aliyechukua huduma ya mwili  wa ubinadamu uliojeruhiwa na udhalimu, uonevu , chuki na choyo.

Kisha Papa aliutaja Utatu  Mtakatifu  kuwa ni familia yenye  nafsi tatu, Baba, Mwana na Roho Mtakatifu,  ambazo hazijikufungia kipekeepekee,  lakini  bali ni wazi katika upeo wa usharika wa Utatu, kama mfano wa  moyo  wa  kuishi katika upendo na kugawana kindugu,  na hivyo tunapata kuona kwamba,  ambapo kuna upendo, kuna Mungu.

Baba Mtakatifu aliendelea kueleza kwamba , familia hii ya  Utatu Mtakatifu inakuwa kielelzo wazi , katika kuuelewa wito wa Mungu kwa Binadamu,  kama viumbe kuishi katika uhusiano  wenye  mshikamano na upendo,  mmoja kwa mwingine.  Maisha ya mshikamano na Umoja na hasa jumuiya za Kikristo na jamii kwa ujumla.

Baada ya Sala ya Malaika wa Bwana, Baba Mtakatifu alielekeza mawazo yake katika Mkutano wa Dunia wa juu ya Ubinadamu, ulioitishwa na Umoja wa Mataifa huko Istanbul , kwa ajili ya kutafakari hali  halisi za ubinadamu katika ulimwengu wa leo. Papa alitolea sala ili washiriki waweze kutoa jibu linalo faa kuokoa maisha ya kila binadamu bila ubaguzi, hasa kwa wale ambao hawana hatia na wasioweza kujitetea .

Aidha Papa aliwakumbuka waamini wa Kanisa Katoliki nchini China ambao siku ya Jumanne, wanaadhimisha   Ibada maalum kwa Bikira Maria "Msaada wa Wakristo", katika madhabahu yanayoheshimwa sana ya Sheshani  Shanghai.  Alimwomba Mama Maria awawezeshe Wakristo wa China, kupambanua wakati wote,  dalili za uwepo wa upendo wa Mungu,wenye kupokea na kusamehe. Na pia Papa alimtaja Mwenye Heri Mpya Padre Francesko Maria Greco, Padre wa Jimbo la Calabria aliyetangazwa kuwa mwenye Heri Jumamosi iliyopita, akisema ni mfano bora kwa Mapadre wote.

Kati ya Umati huu mkubwa wa watu waliofika kumsikiliza Papa , walikuwepo pia kundi kubwa la waamini Waotodosi kutoka Jimbo Kuu la Bera Almania, aliowataja kuwa mashahidi hai wa  uekumene.  








All the contents on this site are copyrighted ©.