2016-05-23 12:15:00

Mapambano dhidi ya matumizi haramu ya dawa za kulevya!


Mshikamano wa dhati sanjari na ukuaji wa biashara unaendelea kuoneshwa sehemu mbali mbali za dunia kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia ya mawasiliano, mambo ambayo pia yanachangia kwa kiasi kikubwa uhalifu, biashara haramu ya dawa za kulevya na matumizi yake yanayoendelea kuongezeka siku hadi siku. Hii ni changamoto inayopaswa kuvaliwa njuga na Jumuiya ya Kimataifa kwani wafanyabiashara wa dawa za kulevya ni watu wenye nguvu ya kiuchumi na wanatishia pia usalama na maisha ya wengi.

Biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya yanakwenda sanjari na biashara haramu ya binadamu inayoendelea kudhalilisha utu na heshima ya binadamu; biashara haramu ya silaha, vitendo vya kigaidi sanjari na uhalifu wa magenge. Madhara ya  vitendo vyote hivi ni makubwa kwa watu na jamii ya binadamu katika ujumla wake. Ni vitendo vinavyoathiri maendeleo katika masuala ya kiuchumi, kisiasa na kijamii na matokeo yake ni ongezeko la umaskini na maafa kwa watu wasiokuwa na hatia!

Hii ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na Monsinyo Janusz S. Urbanczyk, mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Umoja wa Mataifa wakati wa mkutano wa 59 wa Tume ya Umoja wa Mataifa inayodhibiti Dawa za Kulevya, kama sehemu ya maandalizi ya mkutano wa Baraza la Umoja wa Mataifa kuhusu madhara ya Dawa za Kulevya Duniani. Kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kudhibiti biashara haramu ya dawa za kulevya pamoja na kuendelea kuwasaidia waathirika ili waweze kuanza upya na kuwajibika zaidi katika jamii.

Sheria ichukue mkondo wake pamoja na kuthamini mchango unaotolewa na Jumuiya za kidini katika kuwasaidia waathirika wa matumizi haramu ya dawa za kulevya. Kanisa Katoliki ni mdau mkubwa katika huduma ya afya sehemu mbali mbali za dunia. Ujumbe wa Vatican ungependa kuona Jumuiya ya Kimataifa ikibainisha sera na mikakati ya kupambana na biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya duniani. Kipaumbele cha kwanza kiwe ni kudhibiti pamoja na kuwasaidia waathirika wa matumizi haramu ya dawa za kulevya, ili kuwarejeshea tena afya bora, tayari kuchangia mchakato wa ustawi na maendeleo ya jamii husika.

Monsinyo Janusz S. Urbanczyk anakaza kusema, hapa kuna haja ya kujenga na kuimarisha mshikamano wa kimataifa, ili kupambana kikamilifu katika kuzuia na kudhibiti biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya duniani, bila kusahau kanuni maadili inayojikita katika mshikamano. Waathirika wa dawa za kulevya ni mzigo mkubwa kwa familia na jamii husika, kwani unagusa na kutikisa utu na heshima yao kama binadamu. Madhara yake ni makubwa katika mshikamano na utengamano wa kifamilia.

Familia iwe ni shule ya kwanza kwa watoto dhidi ya biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya. Familia isaidie kukinga, kuwatibu na kuwasaidia wanafamilia walioathirika na matumizi haramu ya dawa za kulevya. Hili ni tatizo mtambuka linalohitaji nguvu, sera na mikakati ya pamoja sanjari na kuhakikisha kwamba, mikataba na itifaki za kimataifa zinatekelezwa kikamilifu. Jumuiya ya Kimataifa itafute sababu msingi ya biashara hii na matumizi yake, ili kwa pamoja, iweze kutoa jibu muafaka.

Ujumbe wa Vatican unapendekeza kwamba, sera na mikakati itakayoibuliwa na Jumuiya ya Kimataifa, kwanza kabisa itoe kipaumbele kwa: maisha, utu na heshima ya binadamu. Adhabu ya kifo imekuwa ikutumiwa na nchi nyingi kama njia ya kupambana na biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya, lakini bado haijafua dafu! Kanuni maadili, haki msingi za binadamu na maisha yake, vipewe msukumo wa pekee!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.