2016-05-23 08:46:00

Iweni makini msijekuishia kwenye Utata!


Endapo tunaulizwa, zipi ni tabia pekee zinazoitofautisha dini ya Kikristo na dini nyingine, unaweza ukajibu haraka haraka kuwa ni Upendo na huruma kwa jirani. Lakini kuna waamini wa dini nyingine wanahubiri upendo na kutenda matendo ya huruma vizuri zaidi. Labda utajibu kuwa tabia pekee ya wakristu ni kusali. Kumbe, kuna dini nyingine zimebobea sana katika kusali hata unaweza kujisikia aibu kujilinganisha nao. Kwa mfano wenzetu Waislamu, Wayahudi, Wabuda, Wapagani wanasali sana. Hata hatuwezi kusema tabia yetu ya pekee ni kumwabudu Mungu mmoja. Kumbe kila dini ina imani kwa Mungu mmoja tu bali tunatofautiana jinsi tunavyomwita.

Kumbe, tabia pekee inayoweza kututofautisha na dini nyingine inalala katika suala la kuhakiki ni aina gani ya Mungu tunayemsadiki na ni kwa jinsi gani tumfahamu na Mungu huyo anaathiri kivipi maisha yetu. Dini zote zinaamini juu ya Mungu aliye Nafsi. Mathalani Waislamu, wanaamini kuwa Mungu ni nafsi yenye enzi, ni muumbaji pekee, lakini ni Mungu anayeishi mbali mbinguni na kutawala ulimwengu kutoka huko. Mungu huyo ametoa sheria zake ambazo binadamu yambidi kuzishika na kusubiri hukumu siku ya kiama. Kumbe kwa Wayahudi, Mungu huyo ni nafsi, lakini anayependa kukaa na watu. Mungu huyo aliwasiliana na Abrahamu, alienda Misri kuwachukua watu wake na kutanguzana nao jangwani. Alikuwa nao hadi utumwani Babiloni na badaye akarudi na kukaa nao Hekaluni Yerusalemu katika Sanduku la Agano

Kadhalika sisi Wakristo tunamwabudu Mungu aliye nafsi. Lakini ni nafsi hiyo ni ya aina gani na anakaa-kaaje nasi hilo ndilo swali la msingi linalojibiwa katika Sherehe ya Fumbo la Utatu Mtakatifu. Sherehe ya Utatu Mtakatifu ni fursa pekee tuliyo nayo wakristo ya kutathimini nafasi aliyo nayo Mungu katika maisha yetu. Tunaweza kuwa waamini bora, lakini kumbe Mungu hana nafasi yoyote katika maisha yetu, yaani Mungu hapewi kipaumbele cha kwanza katika maisha, badala yake tunamsahau na tunaona maisha yanasonga mbele kama kawaida hata bila ya Mungu. Sikukuu ya leo ni fursa ya mkristo kutathmini mahusiano yake na Mungu.

Aidha hatuna budi kuelewa vyema toka mwanzoni, kwamba msamiati huu wa UTATU Mtakatifu siyo wa kibiblia, bali ni mapato ya tafakari aliyofanya binadamu ya kujaribu kuunda kitaalamu kwa kutumia vigezo vya kifilosofia ukweli ulio katika Biblia. Kwa hiyo yabidi msamiati huo uundwe kwa uangalifu mkubwa sana, unaweza ukabadili maana, badala ya kuwa Utatu Mtakatifu tukapata Utata mtupu, na tukishia kueleweka kwamba tunaabudu miungu watatu. Kumbe kimsingi wakristo kama walivyo waamini wa dini nyingine, tunamwabudu Mungu mmoja ambaye ni Baba, ni Mwana na ni Roho Mtakatifu. Hizi zote ni picha ambazo akili inajaribu kuweka kwa uangalifu ukweli ulioko katika Biblia juu ya Mungu huyo mmoja. Kwa hiyo inatubidi kuutafakari msamiati huu wa UTATU Mtakatifu katika mwanga wa Maandiko Matakatifu yaani Biblia. 

Biblia Takatifu yatuambia kuwa Mungu ni mmoja tu naye ni Bwana. Hiyo ndiyo imani tuliyorithi toka kwa taifa teule la Waisraeli nayo ni kiini cha msingi wa imani yao kinachosema kwamba Mungu ni mmoja tu (Adonai). Aidha, tunapozungumza juu ya Mungu mmoja tunamaanisha kuwa Mungu huyo ni Baba, aliyeumba ulimwengu na anauongoza kwa hekima yake. Hekima yake tunaiona kwa njia ya viumbe vyake pale tunapotumia akili aliyotupatia. Kutokana na maovu yalivyozagaa ulimwenguni wengine wanaweza kudhani kuwa Mungu huyo hakuwa na nia njema na binadamu alipouumba ulimwengu wake.

Kumbe mkristo anamini kwamba Mungu aliumba vyema kabisa ulimwengu huu na alikuwa na malengo nao. Kwa sababu kila siku alipomaliza kuumba inasemwa: “Mungu akaona kila kitu alichoumba kuwa ni chema.” Huyu ndiyo Mungu anayemwamini mkristu. Aidha, Mungu huyo amejiruhusu kuonekana kamili kabisa kama binadamu katika picha ya Yesu aliyejidhihirisha na kuonekana kwa binadamu. Mungu huyo ni upendo. Kwa vyovyote kama tungekuwa na picha ya Mungu kuwa ni dhahabu hapo huyo Mungu angekuwa dhahabu. Kumbe picha ya Mungu wetu ni upendo. Huyo amejionesha kuwa ni upendo na ni upendo tu, na amejionesha hivyo kwani alitaka kujidhihirisha hivyo kwa viumbe vyake.

Lengo la kujidhihirisha au kujimwilisha ni kuingia katika familia ya kibinadamu ili binadamu aingie katika ulimwengu wa upendo wa kimungu. Binadamu tunaweza kuingia katika ulimwengu huo wa Mungu ulioainishwa katika biblia pale Yesu kwa karibu mara tano anawaahidi Roho mtakatifu. Pale anapoongea na Nikodemo, anasema: “binadamu budi kuzaliwa tena.” Akimaanisha kuzaliwa toka juu, kwa Mungu, kwani kuzaliwa kimwili kutakuwa daima kuzaliwa kimwili. Yesu alifika hapa duniani ii kutupatia uzima wa juu. Pale alipopumua mara ya mwisho, akatukabidhi roho yake yaani, maisha ya upendo wa Mungu na kuuweka ndani ya kila mmoja wetu. Hiyo ndiyo zawadi aliyoileta hapa duniani yaani kutuingizia maisha ya Mungu ambayo ni ya upendo usio na masherti ndani ya mioyo yetu.

Kisha Yesu anasema tena katika Injili: “Ninayo mengi ya kuwaeleza lakini kwa sasa hamwezi kupokea Kutokana na uzito wake.” Siyo kwamba Yesu anayo mengi ya kuongea, lakini kwa vile hana muda anashindwa kuongea yote au roho ataongezea kitu fulani baadaye, la hasha. Yesu anaongea juu ya wafuasi wake kutoweza kupokea uzito wa ujumbe wake kwa vile pale binadamu anaposhindwa kupokea roho hii ya maisha ya Mungu, hapo binadamu hataweza kuishi kikamilifu na kuonesha kikamilifu maisha yaliyo ya juu zaidi ya yale ya kibaolojia au yale ya kibinadamu. Kumbe maisha ya kimungu hutupeleka mbele zaidi ya kuonesha upendo kwa jirani, kuishi maisha ya Kristo.

Kwa hiyo Yesu anasema, “Roho Mtakatifu atatuongoza kwenye ukweli,” yaani siyo ukweli ule wa kutosema uwongo, bali ni ule wa kuwa mtu halisi. Kwani kilele cha juu cha utu wa binadamu ni kuishi maisha ya kimungu. Atakayetuingiza katika maisha hayo ya ukweli ni Roho mtakatifu. Roho hiyo ni nguvu ile ya Yesu ya kuishi maisha ya kimungu kama atakavyo Mungu, yaani kutuwezesha kuwa na nguvu itokayo ndani ya moyo wa mtu ya kuishi na kutenda kimungu. Hiyo ndiyo kazi ya nguvu ya Yesu ambayo ni Roho mtakatifu ya kutuonesha ukweli huo.

Kisha Yesu akasema:  “Atatangaza mambo ya mbele”, ni kwamba itakufanya ujue ni kitu gani kinafaa katika maisha. Aidha, “Roho atamtukuza Baba.” Maisha yote ya Yesu ni kumtukuza Mungu, “Nilimtukuza Mungu” hivi roho aliye katika wafuasi ndiye atakayemtukuza Mungu, yaani nafsi ya Yesu itakuwa katika wafuasi ndiyo watakaomwabudu Mungu. Kwa vile lengo ni kumfanya Yesu ajidhihirishe ndani ya wafuasi.

Neno la lugha ya Kigiriki lililotumika hapa kuhusu kumtukuza au kumtangaza Baba ni anangelei. Maana yake siyo tu kutangaza bali ni kutangaza tena, kuhubiri tena kazi ya Roho. Kwa vile ujumbe wa Yesu umeshasikika masikioni, sasa yabidi kuuchukua ujumbe huo na kuutangaza tena hadi upenye mioyoni mwa watu. Kwa namna ya pekee kabisa katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, Wakristo na watu wote wenye mapenzi mema wanahamasishwa na Mama Kanisa kuwa kweli ni chumvi na mwanga wa mataifa kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko; ushuhuda unaomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya kila siku. Ni changamoto ya kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha, utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu  

Ili ujumbe huu uweze kuingia hadi mioyoni, basi hiyo ni kazi ya Roho Mtakatifu ambayo ni mang’a uzi tunayobidi kuwa nayo sisi sote ya kuishi na kutenda. Tutafanikiwa kufanya hivyo pale tu tunapokuwa na moyo safi, yaani tunaposikia mapendekezo ya Yesu, na roho inapotuambia mioyoni, tupokee na tufuate njia hiyo ya maisha ya kimungu. Tunaposikia sauti hiyo ndani mwetu, roho anayetutangazia tena ujumbe aliotutangazia Yesu na kuuishi. Hii ndiyo maana ya Utatu Mtakatifu vinginevyo ni utata mtupu. Hii ni changamoto ya kujenga na kudumisha umoja, upendo na mshikamano wa dhati kwani Mungu ni upendo unaowakumbatia wote pasi na ubaguzi!

Heri sana kwa Sherehe ya Utatu Mtakatifu.

Na Padre Alcuin Nyirenda OSB.

 








All the contents on this site are copyrighted ©.