2016-05-23 11:38:00

Furaha ya upendo ndani ya familia! Mshikamano wa dhati!


Kardinali Christoph Shonborn, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Vienna, Austria ni kati ya viongozi wakuu wa Kanisa walioshiriki katika uzinduzi wa Wosia wa kitume wa Baba Mtakatifu Francisko Furaha ya Upendo ndani ya familia “Amoris Laetitia” kwa kuwataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kujisomea wenyewe wosia huu ili kugundua utajiri mkubwa unaotolewa na Baba Mtakatifu Francisko anayezungumzia furaha ya upendo katika maisha ya familia. Baba Mtakatifu anatumia lugha rahisi inayofahamika na watu wa kawaida kabisa, ikilinganishwa na lugha ambayo imezoeleka katika Nyaraka za Kanisa!

Baba Mtakatifu anazungumzia uhalisia wa maisha pasi na kuzunguka mbuyu! Ni wosia unaowajaza waamini furaha ya Injili ya familia hasa wakati huu Mama Kanisa anapoadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Huu ni wosia unaojikita kwenye maisha ya ndoa na familia katika ukamilifu wake, changamoto na magumu ambayo familia inakumbana nayo katika safari ya maisha yake ya kila siku.

Wosia unalenga kuwaambata waamini wote pasi na ubaguzi, kwani huruma na upendo wa Mungu inawaambata wote, kielelezo na ushuhuda wa Injili ya huruma ya Mungu ambayo ni kiini cha mafundisho ya Baba Mtakatifu Francisko. Ni changamoto kwa familia ya Mungu kutembea kwa pamoja, huku ikiwa imeshikamana kwa dhati, ili kusaidiana, kuhudumiana na kuimarishana; ili kukua na kukomaa kwa kujikita katika hatua mpya zaidi.

Kardinali Shonborn anasema waamini watambue dhambi, vikwazo vya maisha ya ndoa na familia; machungu yake, tayari kujikita katika mchakato wa toba, wongofu wa ndani, msamaha na upatanisho wa kweli; mwanzo mpya wa maisha ya ndoa na familia. Baba Mtakatifu anaichambua familia “kama karanga” huku akiwa na jicho la huruma na upendo wa Mungu, ili kuwatangazia wanandoa Injili ya furaha. Wosia huu hauna nafasi ya kumbeza mtu awaye yote bali unajenga jukwaa la upendo, ukarimu, toba, msamaha na upatanisho, tayari kuandika na kushuhudia Furaha ya upendo ndani ya familia.

Baba Mtakatifu anakazia kwa namna ya pekee: utakatifu wa maisha, utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu na kwamba, watu wote wanahitaji kuonja na kuambata huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao! Wakristo wanapaswa kushuhudia uzuri na utakatifu wa maisha ya ndoa na familia; kwa kuwajibika na kuonesha ukarimu, neema na baraka zinazobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Wanandoa wakristo wawe wanyenyekevu wanaoshuhudia uhalisia wa maisha pasi na unafiki, ili kweli vijana wa kizazi kipya waweze kuvutika kujenga msingi wa maisha bora ya ndoa na familia. Wakristo wafahamu pia kwamba, ndoa si lelemama! Ina utakatifu, uzuri na wema wake, lakini pia ndoa ni sawa na dawa ya mchunguti, inachangamoto na karaha zake zinazopaswa kufafanuliwa ili watu waweze na mwelekeo mpana zaidi wa maisha ya ndoa na familia, changamoto ya wongofu wa kichungaji.

Ndoa ni safari inayowawezesha wanandoa kusaidiana, kutakatifuzana na kutanguzana katika maisha, wakati wa raha na machungu; wakati wa furaha, kicheko na shangwe ya mafanikio ya maisha! Jambo la msingi anakaza kusema Kardinali Shonborn ni kujenga dhamiri nyofu miongoni mwa watu; kwa kujikita katika malezi, elimu na katekesi makini na endelevu kuhusu maisha ya ndoa na familia, tayari kumjengea mtu uwezo wa kuwajibika na kudumu katika maamuzi yake.

Utengano na talaka ni magumu na machungu yasiyovumilika katika maisha ya ndoa! Mchakato wa uhuru na ukomavu ni muhimu sana katika udumifu wa maisha ya ndoa na familia. Dhamiri nyofu inaweza kuanza kutambua nyakati za shida na magumu ya maisha tayari kuzifanyia kazi kwa kutafuta ufumbuzi wa kudumu na ukomavu wa maisha ya Kikristo mchakato unaotekelezwa kwa kumwambata Kristo Yesu.

Hapa wanandoa wanahamasishwa kuwa kweli ni waaminifu kwa Mungu na Kanisa katika maagano yao ya ndoa, kwa kutambua kwamba, wanapaswa kujisadaka na kusaidiana, ili kwa pamoja waweze kufikia utakatifu wa maisha unaojikita katika Furaha ya upendo ndani ya familia, utenzi wa sifa na shukrani kwa Mwenyezi Mungu.

Kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu Francisko katika wosia wake wa kitume anawaalika waamini kutafakari Sura ya kumi na tatu ya Waraka wa kwanza wa Mtume Paulo kwa Wakorinzi, anawahamasisha wanandoa kuwa na ujasiri na tumaini katika fadhila ya upendo inayoweza kukua na kuchanua kama mtende! Lakini pia upendo unaweza kusinyaa na kunyauka kama mboga ya “mgagani iliyoota mbugani” Waamini wajenge na kudumisha upendo wa kweli na wala si hali ya kujisikia tu ili kukidhi tamaa ya mwili!

Katika maisha tete na magumu ndani ya familia; katika mashaka na wasi wasi, Baba Mtakatifu anawataka wanandoa kufanya mang’amuzi ya dhati mbele ya Mwenyezi Mungu, changamoto kwa viongozi wa Kanisa kuwa makini si tu kwa kuzingatia sheria, kanuni na maadili, bali kuonesha huruma na upendo wa Mungu kwa wale wanaoteseka. Waamini wanaalikwa kuzingatia kwa namna ya pekee, wosia uliotolewa na Mtakatifu Yohane Paulo II kuhusu utume wa familia katika ulimwengu mamboleo, “Familiaris Consortio” waamini wawe na ujasiri wa kutafuta majibu kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa kuzingatia mapungufu yao ya kibinadamu, bila kukatishwa tama, bali kuendeleza mchakato wa toba, wongofu wa ndani na utakatifu wa maisha.

Baba Mtakatifu anafafanua kwamba, hakuna njia ya mkato, lakini anawakumbusha Mapadre kwamba, kiti cha huruma ya Mungu si mahali pa hukumu, bali mahali ambapo kweli mwamini anaonja na kushuhudia huruma ya Mungu. Sakramenti ya Ekaristi Takatifu si nishani kwa waamini wakamilifu na watakatifu, bali ni chakula cha wanyonge, wadhambi na wale wanaotubu, tayari kumwambata Kristo Yesu. Hii ni changamoto pevu anasema Kardinali Shonborn kwa viongozi wa Kanisa kuondokana na misimamo mikali ya shughuli za kichungaji, tayari kuambata na kumwilisha huruma na upendo wa Mungu kama njia makini ya kushuhudia huruma ya Mungu ikimwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu!

Baba Mtakatifu anaweka tumaini lake katika Furaha ya upendo ndani ya familia kwani hapa familia zinaweza kupata dira, njia na mwelekeo wa kumwendea Mwenyezi Mungu, ambaye ni asili na kiini cha upendo. Furaha ya upendo ndani ya familia ni changamoto nyeti inayosheheni furaha ya kweli!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.