2016-05-15 07:38:00

Nguvu ya Roho Mtakatifu!


Mara nyingi wanafunzi wanapohitimu masomo yao hufanyiwa dhifa au mahafari. Katika mazingira hayo hualikwa mgeni rasmi anayetegemewa kugawa vyeti kwa wahitimu. Kadhalika anatazamiwa kutoa zawadi yake nono kwa wahitimu au hata kwa shule kijumla.  Fasuli ya Injili ya leo inaonesha Yesu yuko katika mahafari ya mwisho ya kuuaga ulimwengu huu. Tunaweza hata kudhani labda angetegemea kupongezwa na wafuasi wake hadi hapo alipowafikisha.

Ama kweli alistahili kwani Yesu aliukuta ulimwengu umefikia pabaya sana, ulikuwa umechakaa kama kiatu cha raba! Yaani we acha tu! Binadamu walikuwa wanatawaliwa kinyama na viongozi waliostahili kuitwa wanyama. Yesu akaingiza roho na nguvu mpya ya upendo wa kweli wa Mungu. Kwa hiyo katika dhifa hiyo, Yesu hapendi mapozi mengine, bali anawataka wafuasi wake waendeleze sera zake anaposema: “Mkinipenda mtashika amri zangu.”

Upendo anaodai Yesu ni kama ule wa msichana anayetaka kuolewa anavyomhoji mchumba wake: “Kama unanipenda basi unganisha maisha yako na yangu ili kwa pamoja tufanyie mradi mmoja wa maisha.” Kwa hiyo, Yesu tutoe ushirikiano. Kwa vyovyote yabidi tusifanye mzaha, kwani Yesu anataka tutoe ushirikiano bila woga wowote, tena utoke ndani ya mtu. Kama vile kuwa na nguvu ya kumsamehe mbaya wako, au kuwatumikia watu wa baki kama wanavyofanya baadhi ya watawa wa kike au wa kiume, wanaohudumia wakoma, wagonjwa wa ukimwi, wenye vifua vikuu tunaoshindwa kuwakaribia tukichelea kuambukizwa, au wafanyavyo mapadre kuwahudumia wafungwa ambao wengine tunawaogopa.

Nguvu hiyo ya Yesu, tunaipata katika dhifa ya leo. Mtume Paulo anapambanua nguvu aina mbili zinazomsukuma binadamu kutenda mambo fulani na kuacha mengine. Mosi kuna matendo ya mwili yanayosukumwa na nguvu za kibinadamu (kibaolojia) nayo ni: “Uasherati, uchafu, ufisadi, ibada ya sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi, husuda, ulevi, ulafi, na mambo yanayofanana na hayo.” (Wagal. 5:19-21). Pili kuna matendo ya kiroho yatokanayo na nguvu za kiroho anazotupatia Yesu nayo ni: “Upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole, kiasi; juu ya mambo hayo hayo hakuna sheria” (Wagal. 5:22-23). Kinachofanya tabia ya utu siyo kuwa na akili, bali ni kuvuvumka (evolution) kutoka matendo ya unyama hadi kilele cha mwisho cha utu ambacho ni cha kupenda kama Mungu anavyopenda.

Kwa hiyo moja ya ahadi za Mungu tunayopata leo ni zawadi ya maisha ya Yesu mwenyewe, nayo ni roho au nguvu mpya inayotusukuma kupenda toka ndani kama alivyopenda yeye. Huo ndiyo urithi bora na pekee aliotuachia Yesu anaposema: “Nitamwomba Baba, naye atawapa Msaidizi mwingine, ili akae nanyi hata milele.” Huyo msaidizi mwingine (Roho) tutampata tukisali: “Basi, ikiwa ninyi mlio waovu mnajua kuwapa watoto wenu vipawa vyema, je, Baba aliye mbinguni hatazidi sana kuwapa Roho Mtakatifu hao wamwombao?” (Lk 11:11-13) Kwa hiyo sala inatupatia Roho mtakatifu na tunakuwa na kipaji cha sala.

Kwa kawaida Siku kuu ya Pentekoste Wayahudi walisherehekea zawadi ya Tora yaani kupewa kwa Amri kumi mlimani Sinai. Wakafanya agano na Mungu, lakini wakawa daima wanalivunja agano hilo. Nabii Yeremia akatoa mwongozo wa agano jipya lenye sheria zinazomgusa mtu ndani kabisa ya moyo wake. Nguvu hiyo inalinganishwa na upendo wa mwanamke, ambao kabla ya kuwa na mtoto wake mwenyewe, anakuwa na upendo mkubwa kwa watoto wengine. Lakini anapokuwa na mtoto wake mwenyewe, mwanamke huyo anakuwa na nguvu na msukumo wa ndani wa kufanya mambo kama mama. Ndivyo anavyotabiri nabii Yeremia: “Nitatia sheria yangu ndani yao, na katika mioyo yao nitaiandika. Nami nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu.” (Yer 31:33. Hapo moyo wa mtu unakuwa kama mashine ya dira (navigator), inayoonesha njia ya kufuata.

Sikukuu ya Pentekoste kwa Wakristo ni kusherekea udhihirisho wa ahadi ya nguvu ya upendo aliyotupatia Yesu, nguvu inayotugusa ndani mwetu. Nguvu hiyo mpya inayotolewa na roho wa Yesu inalinganishwa na alama mbalimbali zinazoelezwa katika Matendo ya mitume. Mosi, roho inatoa nguvu mpya ya Uvumi na matetemeko.  “Kukaja ghafula toka mbinguni uvumi kama uvumi wa upepo wa nguvu ukienda kasi, ukaijaza nyumba yote waliyokwua wameketi.” Uvumi na mtetemeko huo unatoka mbinguni, siyo ulimwengu. Mtetemeko wa kwanza uliotokea alipokufa Yesu Kalvarini, na wa pili ni siku ya Pasaka Yesu alipofufuka, malaika akaja akaliviringisha jiwe la kaburi na kulikalia.

Matetemeko hayo ni ya historia ya kibinadamu iliyotetemesha ulimwengu. Nguvu nyingine ya roho huyo ni upepo kwa kiebrania ni ruah, ulioijaza nyumba nzima. Hiyo ni nguvu ya upepo wa roho mwumbaji. “Nayo nchi ilikuwa ukiwa tena utupu, na giza lilikuwa juu ya uso wa vilindi vya maji; Roho ya Mungu ikatulia juu ya uso wa maji.” (Mwa 1:2). Upepo huo una nguvu ya kusukuma milima, ya kusambaratisha na kupeperusha kila kitu. Upepo ulifungua milango na Mitume wakatoka nje na kuhubiri bila woga.

Leo sisi tunaweza kukatishwa tamaa, kuvunjika moyo na kukosa nguvu ya kuyatatua matatizo ya maisha. Lakini kama tunaamini kwamba kuna nguvu ya roho wa Yesu kutoka mbinguni anayeweza kujenga ulimwengu mpya wa undugu, hapo kila kitu kinawezekana. Nguvu nyingine ya roho wa Yesu ni: “Ndimi za moto zilizowakalia katika kichwa kila mfuasi.” Nguvu hii ya moto ni ya kiapokalipto. Huu ni moto unaonguza. Yesu alisema: Nimekuja kuwasha moto duniani na ninataka uwake. Yesu amefanywa kwa moto wa upendo wa Mungu. Moto huo ni maisha ya Mungu aliye upendo. Ukipata nguvu hiyo, hapo unapata nguvu ya kuongea lugha mpya ya upendo inayofahamika na watu wote ulimwenguni.

Tunaweza kupokea roho hiyo katika mwongozo wa Mwana wa Mungu aliye ndani yetu na siyo katika ubinadamu wa kale na tukaweza kubadili maisha. Hapo tutafanana na Yesu aliyefanana na Baba yake: “Mtu akinipenda, atalishika neno langu, na Baba yangu atampenda, nasi tutakuja kwake na kufanya makao kwake.” Yesu anafanana kabisa na Mungu kwa vile alikuwa na roho ya Mungu katika ukamilifu wake wote. Kwa hiyo, kila anayempokea Yesu aliyekuwa na roho wa Baba wa upendo, ataishi kama mwana wa Mungu.

Yesu anajionesha kwa njia ya sisi tunavyomuishi na siyo kwa njia ya miujiza, kwani miujiza inakuja yenyewe hasa kama sisi tunaishi kama waana wa Mungu. Kama vile muujiza tunaouona kwa watu wanaoacha kufuata mali ya ulimwengu huu na kujitoa kusaidia wengine. Huu ndiyo muujiza, pale watu wanapopokea maisha hayo ya kupenda bila mipaka kama Yesu. Hivi kwa njia yetu, Yesu anajidhihirisha nafsi yake. Kwa hiyo, jumuiya ya kikristu haipo kwa ajili ya kutoa mafundisho fulani, la hasha, bali ipo kwa ajili ya kudhihirisha na kushuhudia uwepo wa Kristo mwana wa Mungu ulimwenguni. Jumuiya ikipokea vyema zawadi hiyo ya Mungu yaani kumpokea Mwanaye Yesu, hapo itadhihirisha maisha ya Yesu. Huyo Roho anatufundisha kila kitu, atatupa mwongozo wa ndani. Tumshukuru Mungu kwa zawadi hii ya mbinguni.

Heri sana kwa Sherehe ya Pentekoste.

Padre Alcuin Nyirenda, OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.