2016-05-11 08:06:00

Baba Mtakatifu atuma barua kwa Patriaki wa Kanisa la Kikoptuki juu ya Siku ya Urafiki


Baba Mtakatifu Francisko siku ya Jumanne 10 Mei, alifanya kumbukumbu ya  kukutana kwa  mara ya kwanza kwa   Papa Paulo VI, Askofu wa Roma, na Mkuu wa Kanisa la Kikoputiki la Kiotodosi,  Papa Shenouda III, tukio lililofanyika miaka 43 iliyopita.  Kwa ajili ya kumbukumbu  hii iliyoitwa “Siku ya Urafiki kati ya Wakoptiki Waotodosi wa Misri na  Wakatoliki wa Roma,  Papa Francisko  ameandika barua kwa Mtakatifu Sana  Tawadros II, Papa wa  Upatriaki wa Alexandria  wa  Mtakatifu Marko.

Katika barua hiyo,, Papa Francisko ameonyesha  kufurahia muungano wa kina wa kiroho kati ya  Wakatoliki na Wakoptiki Waotodosi , akimshukuru  Mungu kwa hatua za pamoja mpaka sasa kwenye njia hii ya maridhiano na urafiki.  Amesema  kuwa , ingawa  bado ni safari ndefu kufikia  muungano kamili wa kukusanyika  wote katika meza moja ya Bwana,  yaani Ekaristi, kuna hatua za kuonekana zilizopigwa zenye kuwaunganisha mpaka sasa.  

Barua hiyo ya Papa Francisko inatoa mwaliko kwa Wakatoliki na Wakoptiki , kutoa jibu la ukarimu katika ujenzi  wa  moja kamili  uliojengwa  juu ya msingi wa Injili ya Kristo , na katika kupambana na changamoto za  nyakati hizi,  hasa  Mashariki ya Kati, ambapo Wakristo wanaendelea kukabiliwa na mateso ya kila siku.  Kwa ajili yao, amemwomba Mungu Baba  Mwenyezi , awajalie  faraja  za matumaini katika  Kristo  wale wote wanaopita katika mateso haya, na pia jumuiya ya  kimataifa ivuviwe jibu lenye  busara na hekima, katika kukiabiliana na uovu huu. .

Baba Mtakatifu ameonyesha hamu yake kwamba,  katika wakati huu, wanapoendelea na hija ya maisha hapa duniani ,waweze kujifunza kuvumiliana mmoja kwa mwingine na kubadilishana urithi  wa utajiri wa mila za mapokeo , na hivyo waweze kuona wazi kwamba,  kile kinacho waunganisha ni kikubwa kuliko vile vinavyowatenganisha.   

Papa ameeleza pia  akikumbuka mwaka huu ni wa tatu tangu alipokutana naye kwa mara kwa kwanza na Kiongozi wa Kanisa la Kikoptiki la Misri,  mkutano wa udugu uliofanyika hapa Roma May 2013, baada ya ukimya wa miaka mingi katika njia hii ya maridhiano na urafiki . 








All the contents on this site are copyrighted ©.