2016-05-09 15:24:00

Mawasiliano daraja la kukutanisha watu


Tarehe 8 Mei, ilikuwa ni Siku ya Mawasiliano Duniani , mwaka huu ikiwa ni adhimisho la   50 tangu kuanzishwa kwake.  Kwa ajili  hii, Baba Mtakatifu katika ujumbe wake, amekazia zaidi mawasiliano kama fursa ya kujenga madaraja ya kuwakutanisha watu,  kupitia njia ya majadiliano na  mazungumzo ya  amani kati ya watu. Na  kwamba huruma ina uwezo wa kuponya uhusiano uliojeruhiwa , kurejesha matumaini na maelewamo kati ya wanafamilia na katika jamii. Ujumbe huu wa Papa, uliwasilishwa siku za nyuma 24 Januari, ili kutoa muda wa kutosha kusomwa, kabla ya adhimisho lenyewe.  Papa aliandika ujumbe wake chini ya jina:  “Mawasiliano na Huruma:  matunda ya kukutana ” .

Papa ametoa ujumbe wake katika mtazamo wa maadhimisho ya  Mwaka  wa Huruma  sanjari na maadhimisho ya kupita miaka 50 tangu adhimisho la  Siku ya Dunia ya Mawasiliano lilipoanzishwa,  akisema, mwaka Mtakatifu, unatoa mwaliko kwetu sote, kutafakari uhusiano  uliopo kati ya mawasiliano na huruma . Kanisa katika muungano wake na Kristo , mwili hai wa Baba wa Huruma , linaitwa  kuiishi huruma kama tabia yake yenye kuonyesha kwamba,  ni Yeye  Baba mwenye huruma anayetenda.  Papa amewahimiza wakristo wote  kuwa na lugha nzuri inayotoa mwangi wa wema na huruma akisama ni lazima kujali tunasema nini na jinsi tunavyosema ,na  kila neno na tendo , ni lazima litoe picha ya  huruma ya Mungu, upendo  na msamaha wake  kwa  wote.Aliongeza,  “Upendo, kwa asili yake, ni mawasiliano yanayoongoza kwa  uwazi na ushirikiano.  Kama mioyo yetu na matendo vinaongozwa na   upendo wa Mungu, basi mawasiliano yetu yatapata nguvu yake kutoka kwa Mungu mwenyewe”.

Hivyo Papa amesisitiza katika ujumbe huo kwamba, wote kama wana wa Mungu, wake kwa waume , tumeitwa kuwasiliana na kila mtu, bila ubaguzi. Na kwa namna ya Kipekee, Kanisa kwa  maneno na matendo yake yote, yanatakiwa kutoa  maana ya huruma  na kuifikisha huruma hiyo kwa watu, ikigusa  mioyo ya watu na kuwadumisha katika safari yao ya  maisha hadi katika ukamilifu wake ambaye ni Yesu Kristo aliyetumwa na Baba, kuwapeleka wote  kwake Mungu.  Hii ina maana kwamba sisi wenyewe lazima kuwa tayari kukubali upendo  huu wa  Mama Kanisa na kuushiriki ili  na wengine pia wapate kujua kwamba, wanapendwa na Yesu. Ni upendo huo wenye kutoa maana ya Neno la Imani , kwa mahubiri na shuhuda , hutoa "cheche" za maisha.

 Ujumbe wa Papa unaendelea kufafanua kwamba, mawasiliano yana uwezo wa  kujenga madaraja, yenye  kuwawezesha kukutana na kushirikiana , na hivyo kuwa na jamii iliyoimarika katika umoja na mshikamano. Papa ameeleza na wakati huohuo akaonya kwamba , wakati wa kuwasiliana,  inafaa kuchagua maneno na matendo , na kufanya kila jitihada za  kuepuka kutokuelewana, na  kuponya kumbukumbu  za waliojeruhiwa na kujenga amani na utulivu.  Papa anasisitiza maneno na matendo yetu lazima iwe ni nyenzo ya kutusaidia sote kuepuka  mzunguko wa matatizo  na kuhukumu na kulipiza kisasi , ambavyo kwa mara zote huleta utengano  kwa watu, kibinafsi na  hata kimataifa. Ni lazima kuepuka maneno yanayojenga chuki.  Kwa Wakristo lugha yao daima iwe ni kuleta faraja na mshikamano ,  hata katika  matukio yenye  kuchukiza,  wao ni  lazima  wawe imara kulaani uovu uliofanyika , lakini kamwe si kuvunja  mahusiano na mawasiliano.  

Papa amewaomba  wale wenye majukumu hasa ya uongozi kitaasisi na kisiasa, na watoa maoni kwa  umma,ni lazima wawe  makini na maneno yao,  hasa  wanapokosoa wengine wanaodhani wamefanya makosa, kwa kuwa katika hali hiyo ya kukosoana ni  rahisi kuingia katika mtego wa  kushutumiana na hivyo kuwasha moto wa  kutoaminiana, hofu na chuki.  Papa ameomba ujasiri  katika kuongoza watu, ili zaidi iwe ni  kuelekea mchakato wa maridhiano ma siyo utengano. Ni  muhimu daima kuwa na mtazamo chanya  na ujasiri bunifu  katika kutoa  ufumbuzi wa kweli  hata katika migogoro ya kale na nafasi ya kujenga amani ya kudumu. Papa alikamilisha na aya " Heri wenye kuleta amani, maana wataitwa watoto wa Mungu" (Mt 5: 7-9)








All the contents on this site are copyrighted ©.