2016-05-08 09:19:00

Oya! Hivi unatuachaje?


Watu wengine wanapotaka kupokea rushwa hutumia lugha ya kupugaza ili wasigundulike kama wanaomba rushwa. Mathalani, kabla mtu hajasaidiwa shida yake anaulizwa: “Utaniacha-achaje?”  Leo Yesu anatuacha na kupaa mbinguni. Tunaobaki tunaweza kumhoji: “Unatuacha-achaje?” Ukweli ni kwamba Yesu aliacha ulimwengu huu pale Kalvarini alipokufa msalabani aliposema: “Baba mikononi mwako naiweka roho yangu.” Katika Injili na Matendo ya mitume, Luka ametenganisha vituko vya kifo, ufufuko, kupaa na Pentekoste ili tuweze kuelewa vizuri uzito wa tendo la ukombozi alilofanya Yesu hadi ufufuko wake.

Ili kuelewa jinsi Yesu alivyowaacha-acha wafuasi wake, tuone kwanza hali halisi ya kisaikolojia waliyokuwa nayo wafuasi pale walipotokewa mara ya kwanza Yerusalemu. Ilikuwa ni jioni ya siku ya Pasaka wanafunzi walikuwa pamoja wakisikiliza habari toka kwa wafuasi wale wawili wa Emau. Yesu akasimama katikati yao, ndipo kukawa patashika: “Wakashituka, wakaogopa sana, na wakaona shaka mioyoni mwao.” (Lk 24:37-38). Hoja ya wafuasi kushtuka, kuogopa na kuona shaka ilitokana na kuamini macho yao, kwani machoni pa ulimwengu Yesu alikuwa ameshindwa au tungeweza kusema kwa lugha ya mitaani, “amechemsha.” Kumbe machoni pa Mungu Yesu ni mshindi. Mungu amemtukuza kama mtoto mpendwa aliyependezwa naye. Kinachohitajika kwa wafuasi ni kubadili fikra kwamba Yesu hakushindwa bali amefaulu.

Kwa hiyo leo kazi kuu ya Yesu ni kuwasaidia wafuasi kubadili fikra na kuelewa mawazo ya Mungu jinsi yalivyotofauti na fikra za binadamu. Nasi tunaalikwa kubadili fikra na mtazamo wa mambo. Tutafanikiwa tu kubadili fikra zetu tukifuata maagizo ya Yesu anayesisitiza karibu mara mbili. “Ndivyo yatatimizwa kama ilivyoandikwa katika torati ya Musa, katika manabii na katika zaburi. Na Injili ya leo inaanza hivi: “Ndivyo ilivyoandikwa, kwamba Kristo atateswa na kufufuka siku ya tatu.”

Inabidi kuongoka ili kuelewa wazo hilo la Mungu la kuufanya ulimwengu mpya kwa njia mwanae. Aidha yabidi kuutangaza wongofu huo ulimwenguni kote. Anayeendelea kufikiri kwamba mtu aliyefaulu ni yule anayeamuru, anayetawala, anayewakandamiza wengine, anayejifikiria mwenyewe, huko ni kushindwa na siyo fikra za watoto wa Mungu. Wongofu wa kuhubiriwa ni ule wa kubadilika kutoka fikra hizo na kujielekeza kwenye maisha ya kujitoa nafsi kwa ajili ya wengine. Huo ndiyo utume pekee wa kanisa.

Kazi ya utume tunayokabidhiwa na Yesu ni ile ya kuongoa na ya kuwafanya watu wabadilishe mtazamo wa maisha yao. Watu wajikite katika kufuata mfumo wa maisha ya yule aliyefanikiwa katika maisha, na ambaye amejihakikisha katika ufufuko, katika hukumu aliyofanya Mungu katika maisha ya Yesu. Kanisa halina budi kuuonesha ulimwengu kwamba kumezaliwa jumuia mpya yenye kuishi maisha ya Yesu. Huo ndiyo wongofu ambao kanisa linatakiwa kuushuhudia na kuwaalika watu kuuishi.

Halafu “na kwamba mataifa yote watahubiriwa kwa jina lake habari ya toba na ondoleo la dhambi” Hapa tunaalikwa kuutangaza wongofu katika uelewa potovu wa msamaha wa  dhambi. Fikra zetu juu msamaha wa Mungu zina wazo moja tu kwamba, pale tunapotenda dhambi tunastahili adhabu ya Mungu. Lakini tukijuta na kumwomba radhi Mungu anatulia na anatusamehe. Aina hii ya msamaha ndiyo iliyoandikwa kwenye Misahafu. Lakini tunasahau kwamba Mungu hakasiriki, wala hanuni, tena hamwadhibu mtu yeyote kwa sababu Mungu ni upendo. Anachofanya Mungu tunapokosea au kutenda dhambi ni kujaribu kutuelewesha kuwa njia tuliyochagua (dhambi) tumechemsha kwani haitatufikisha kwenye malengo tunayokusudia.

Mungu ametupatia maisha haya na kututakia tuwe kama binadamu wenye utu na wenye furaha. Kumbe tunapopotoka na kuchepuka kutoka kwenye njia sawa, hapo Mungu hatoi adhabu bali anatusamehe bure. Msamaha wa Mungu ni kule kutufanya tuelewe njia sahihi kwa njia ya Neno lake, na kwa njia ya maisha ya ndugu wale waliofanya uchaguzi wa kufuata Injili. Huu ndiyo msamaha wa Mungu. Msamaha ni njia inayotuongoza kwenye mwendo sawa wa maisha. Tunapofahamu na kupokea msamaha wake, hapo tunajutia uchaguzi tulioufanya na tutaanza kuishi maisha kadiri ya Mungu. Kwa hiyo dhambi zetu hazimuathiri Mungu hata kidogo, bali hutuharibu sisi. Aidha Mungu hakasiriki bali yeye ni upendo na anatutakia kwa namna yoyote ile tufahamu njia tunayotakiwa kuifuata.

Utume wa Kanisa ni kutangaza msamaha kwa ushuhuda wa maisha kwamba kanisa limesamehewa, yaani limetengwa na dhambi ambayo ni uchaguzi wa vigezo vya ulimwengu huu. Kwa hiyo kanisa linatakiwa liwe jumuia iliyosamehewa na kwamba limepokea msamaha huo na maisha yake yanafanana na mapendekezo ya Injili. Kuwa shahidi wa ukweli huo haimaanishi kupiga siasa tu la hasha bali yabidi kuishi mang’amuzi ya zawadi hiyo bure ya Kristu. Baada ya Yesu kuhakikisha kwamba amewapa wosia wa wafuasi wake, sasa anawapatia zawadi ya mwisho kabla ya kuwaaga.

Kisha Yesu akawangoza mpaka hadi Betania, akainua mikono na kuwabariki. Alama pekee mchungaji anayeongoza kundi lake. Tena anawabariki, kazi hiyo ya kuhani (padre) anapokuwa hekaluni. Katika sura ya kwanza ya mwinjili Luka, kitendo cha kwanza ambacho Zakaria alishindwa kukifanya alipotoka hekaluni ni kushindwa kuongea, halafu alishindwa pia kuinua mikono yake na hivi alishindwa kabisa kuwabariki watu. Kwa hiyo kutoka hapo ilipofungwa baraka ya kuhani Zakaria, leo tunaikuta tena baraka Yesu kwa mitume wake na kwa ulimwengu mzima. Kubariki maana yake ni kutakia maisha endelevu, au kuwa na uzao zaidi. Kuwa hiyo kubariki maana yake kutakiana maisha mema sisi kwa sisi.

Na alipokuwa katika kubariki alijitenga nao, akachukuliwa juu mbinguni. Mwinjili ameichukua picha hii ya kuchukuliwa Yesu mbinguni, kutoka masimulizi ya watu mbalimbali waliopaishwa angani katika mazingira ya kutatanisha. Mathalani Romulus aliyefifia kwa maajabu ndani ya kimbunga kule Kwilinale-Roma. Kadhalika Hercules kwa vile alikuwa mtoto wa mama binadamu na baba mungu Zeus alichukuliwa mbinguni bila kufa. Huku kupaishwa angani kwa maajabu tunasoma pia katika Biblia. Enok alipokuwa anatembea pamoja na Mungu mara hawakumwona kwani alichukuliwa na Mungu (Mwanzo 5:24). Mwingine ni nabii Eliya alichukuliwa na upepo wa kimbunga ndani ya gari la moto (2Wafalme 2:11). Luka anachukua masimulizi haya ili kutueleza kwamba, mwisho wa maisha haya siyo kifo, bali ni kuhitimika maisha au uzima wa kibaolojia. 

Huu ni ukamilifu wa maisha ya milele yaliyozawadiwa na Yesu, aliye wa kwanza aliyejidhihirisha kwa ukamilifu maisha hayo ya kimungu. Yesu anapobariki na kuondoka kwenda angani siyo kuachana na ulimwengu, bali kutoka mbinguni anatuona vizuri zaidi kwani hajafungwa na mipaka ya ulimwengu huu. Yuko nasi kwa namna nzuri zaidi, kwani anaifahamu hali halisi ya ulimwengu huu na mizengwe yake.

Kwa hiyo mitume wakarudi wakiwa wamejaa furaha kubwa. Katika wingi wa furaha wameelewa kwamba maisha ya kutoa ndiyo maisha yenyewe yaliyofanikiwa, kwamba Kristu hakuacha ulimwengu, bali yuko kwa namna ya pekee zaidi. Furaha hii pia ndiyo aliyoanza kuiandika mwinjili, alipotoa tangazo la furaha, pale malaika anapomwambia Zakaria “Utakuwa na furaha kubwa sana kwa kuzaliwa kwa Yohane mbatizaji.” Kwa Maria anasema Elizabeta anamwamkia kuwa: “furahi Maria, uliyependwa na Mungu.” Pale Bethlehemu malaika wanapowaambia wachungaji “Msiogope; kwa kuwa mimi ninawaletea habari njema ya furaha kuu itakayokuwa kwa watu wote.” Leo tunapata ahadi ya furaha, ya ulimwengu mpya utakaokuwa na furaha. Hivi hata mitume wamejaa furaha, kwani wameelewa ni maisha gani yaliyofanikiwa kwani wameona yametimilika katika mwalimu wao, sasa wanafurahi kwani hata wao wanajisikia kushiriki katika maisha hayo ya upendo. “Wakarudi Yeruslemu wenye furaha kuu.”

Heri kwa sikukuu ya kupaa Bwana Mbinguni.

Na Padre Alcuin Nyirenda, OSB








All the contents on this site are copyrighted ©.