2016-05-06 09:54:00

Papa Francisko : Yesu daima yuko pamoja nasi katika mateso na uchungu wa maisha


Sisi sote tunahitaji faraja kutoka kwa Mungu, upendo wa Bwana usioweza kuondolewa kwa wote wanaomridhia. Ni maelezo ya Papa Francisko,  Alhamisi jioni,wakati akiongoza  mkesha wa maombi  katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro, kama sehemu ya maadhmisho ya Siku Kuu ya Kupaa Rabbi. Mkesha huo uliongozwa chini ya jina” kufuta  Machozi"kwa  nia ya kuwafariji wale wote walio katika hali  za  mateso.   Katika  Mkesha huu,mmoja wa  Wanafamilia waliokabiliwa na  mateso katika maisha yao , alitoa ushuhudu  wake juu ya  uchungu wa maisha waliyoyapitia  na jinsi walivyosaidiwa kupunguza uchungu huo. Aidha wakati wa Maombi haya , kulionyesha masalia  ya  Mama yetu wa Machozi  wa  Siracuse.  Masalia hayo yanahusiana na muujiza uliotokea  mwaka 1953, wakati  picha ndogo ya Moyo safi wa  Maria, iliiyokuwa imetundikwa juu ya Kitanda cha Wanandoa vijana Waitaliano, ilitoa machozi ya uchungu.

Baba Mtakatifu Francisko katika tafakari yake , kwa ujumla aliwatia moyo wote wenye uchungu na mateso , kwamba hawako peke yao, iwapo watazamisha mateso na uchungu wao  katika sala na tumaini kwamba Yesu na Maria wako karibu nao daima. Papa alionyesha kutambua wazi kwamba nyakati za  huzuni, mateso na ugonjwa, huwa  ni  wakati wa uchungu wa mateso na huzuni zinazotoka moyoni , ni wakati  ambamo mtu huhitaji kupata  neno la faraja , neno la kumfuta machozi yake.  Huu ni wakati ambapo  tunahitaji ukaribu wa mtu mwingine, walau kupata hisia  za huruma ya wengine kwamba wanajali.   Papa alieleza na kusema bila shaka kila mmoja amewahi kuguswa na wakati mgumu wa kuhuzunisha ,  wakati wa wasiwasi na  kuvunjika moyo kwa yalie yaliyotokea , kuona kama hakuna tena matumaini kwa nyakati zijazo. Na kwamba, hali hii ya uchungu na mateso,  inaweza kumpata mtu yeyote na wakati wowote. Kwa hiyo ni muhimu na vyema kwa kila mmoja kuwa tayari kuelewa uchungu na  mateso ya wengine na kuwa tayari kutoa msaada na faraja  hata kama  ukaribu huo hautoi jawabu  kamili la kutatua tatizo lakini husaidia kupunguza uchungu moyoni. 

  Papa alieleza na kutazama kwa kina hali za nyakati hizi akisema ni nyuso ngapi zenye huzuni tunazoziona kwa watu wengi  wanaotuzunguka pande zote? Watu wanaotokwa na  machozi mengi, machozi yanayomwagika juu ya uso  wa dunia kila siku ,  kutokana na sababu mbalimbali , na kutangeneza bahari ya majonzi inayolilia huruma,  huba na faraja.  Na alibalini kwamba, machozi yenye  uchungu  zaidi ni  yale yanayosababishwa na ukatili wa binadamu,  asiyekuwa na huruma, mwenye kuchinja wengine mbele ya jamii, familia, watoto , baba na mama. Ni uchungu gani wanaoupata wanafamilia hawa, Papa alihoji kwa masikitiko.Watu kama hao hukeshi wakilia tangu mapambazuko hadi machweo ya jua na usiku mzima.Kwao inakuwa vigumu kuona mapambazuko ya siku mpya.

Kwa uwepo wa mateso kama hayo, Papa anasema,  sote tunahitaji  kuwa na moyo wa  huruma na kuwapa wanaoteseka faraja  za kweli zinazotoka kwa Bwana . Sisi sote tunaitwa kufanya hivyo.  Tunahitaji  kuwakaribia na kupagusa machozi yao kwa huruma yake Yeye Bwana atakayekuja kufuta machozi yetu wote.

Papa aliendelea kutoa neno la faraja na  kuwatia moyo  wote akisema , katika mateso na huzuni zetu hatuko  peke yetu.   Bwana  wetu  Yesu Kristo tunaye mwamini anajua  nini maana ya mateso na uchungu wa kulia,   kwa kuwa aliyapitia mateso haya  katika maisha yake ya kibindamu.  Na hivyo, Mama Kanisa anatuhimiza kusonga  mbele na hija ya maisha kama ilivyokuwa Yesu, alimwona  Maria akitoa machozi kwa  kifo cha ndugu yake Lazaro. Wala  hakuweza  kujizuia kutoa machozi. Alikuwa  amezongwana uchungu wa  ndani  na kuanza kulia( Yn 11: 33-35). Maelezo ya Mwinjilisti Yohana,  yanalenga kutoonyesha kwa kiasi gani Yesu alishiriki katika huzuni na majonzi ya rafiki zake. Hili  linatupa  faraja  kwamba  wakati  wa Uchungu  na kulia Yesu anatujali,  yu karibu nasi akitufariji. Yesu  ana  uzoefu katika nafsi yake mwenyewe,  hofu ya mateso na kifo,  hamu na  kuvunjika moyo katika usaliti wa Yuda na Petro alipomkana,   maumivu  aliyoyapata kama ilivyokuwa wakati alipompoteza  rafiki yake Lazaro.

Papa alieleza na kuongeza wakati wa  machafuko, huzuni na uchungu wa kutoa  machozi, moyo wa Kristo uliotolea sala kwa  Mungu  Baba, maombi hayo yanakuwa ni  dawa ya kweli kwa mateso mateso yake .  Katika sala, sisi pia tunaweza kuhisi uwepo wa Mungu. Huruma yake  inayoonekana katika macho yake, yenye kutufariji na kutupa nguvu mpya katika kutumaini . Papa alitoa wito na tuwe  kama  Yesu, alivyosimama  mbele ya kaburi la Lazaro,  na kuomba  akisema: "Baba, nakushukuru kwa kuwa umenisikia. Nilijua kuwa unanisikiliza daima "(Yn 11: 41-42).  Na ndivyo sisi pia tunahitaji kuomba kwa uhakika kwa  Baba,tukiwa na imani kamili kwamba anatusikiliza, kwa maana upendo wa  Mungu, ulio miminwa mioyoni mwetu,  unaturuhusu sisi kumwomba Baba Yetu wa mbinguni na hakuna Mtu anayeweza kumtenga mbali na wanaompenda, kama Mtume  Paulo anavyoleza  "Ni nani atakayetutenga na upendo wa Kristo? Je ni  ugumu wa maisha, au dhiki, au mateso, au njaa, au uchi au upanga? ... Lakini, katika mambo hayo yote tunashinda zaidi ya kushinda kupitia  kwa yeye aliyetupenda.

Papa alieleza na kuonyesha imani yake kwamba,  wala mauti, wala uzima, wala malaika, wala watawala, wala yaliyopo, wala mambo yajayo, wala wenye uwezo, wala ya juu au  yaliyo chini, wala kitu kingine chochote katika viumbe wote, hayatakuwa  na uwezo wa kututenga na upendo wa Mungu katika Kristo Yesu Bwana. Na kwamba katika mguu wa  msalaba, Mama wa Yesu,  daima huko hapo tayari kutufuta machozi yetu.  Kwa mkono wake ulionyoshwa, yeye hutusaidia kuinuka na yeye huambatana nasi katika njia ya matumaini, alimalizia Papa. 








All the contents on this site are copyrighted ©.