2016-05-05 10:24:00

Iweni mashuhuda wa huruma ya Mungu!


Kanisa leo linaadhimisha Sherehe ya Kupaa Bwana Mbinguni. Leo zimetimia siku 40 tangu Sherehe ya Pasaka. Katika Sherehe hii Mama Kanisa anapata fursa ya kutafakari tukio lile la Kristo kupaa mbinguni wakati ambapo alilipatia pia utume wake akiwaambia “Enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi” na kuwafanya kuwa mashahidi wa Huruma ya Mungu ambayo ilifunuliwa na utume wake wakati wa maisha yake hapa duniani. Hivyo, sherehe hii ya leo inatukumbusha sisi kama wanakanisa utume huo tuliopewa na Kristo na kuwa mashahidi wa Injili ya Kristo. Kwa namna ya pekee, leo pia Kanisa linaadhimisha siku ya Mwasiliano ya kijamii Ulimwenguni. Katika ujumbe wake kwa siku hii Baba Mtakatifu anatuambia kwamba: “Mawasiliano na Huruma: Mkutano wenye kuzaa matunda”.

Somo la Kwanza katika Sherehe yetu linatupatia picha ya tukio hilo la kupaa kwa Bwana wetu Yesu Kristo. Kristo alikusanyika na wanafunzi wake, kabla ya kupaa aliwapatia utume huo wa kuwa mashuhuda wake: “Lakini mtapokea nguvu, akisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu; nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi”. Mitume ambao wanakuwa ni Kanisa la mwanzo kabisa wanapokea utume huo huku wakiongozwa na Roho Mtakatifu. Hapa ndipo tunaiona huduma ambayo Kanisa linapaswa kuiendeleza, yaani kuwa mashahidi wa Kristo Mfufuka na zaidi ni kuwa mashahidi wa huruma ya Mungu inayotimilika katika fumbo hili la Pasaka.

Kanisa linatumwa kuwa na uaminifu kwake Yeye aliyekuwa mwaminifu kwa Baba. Tendo hili la Kristo kupaa Mbinguni linatuonesha muunganiko wa Kristo na Baba yetu wa mbinguni na hivyo kuthibitisha kuwa yale yote ambayo aliyatenda yalikuwa ni kwa ajili ya kumfunua Yeye kwa sababu “Yeye na Baba ni wamoja”. Ubinadamu wetu ambao umetwaliwa na nafsi ya pili ya Mungu na kuunganika naye katika hali ya fumbo unapata uwakilishi katika ufalme wa mbinguni. Sisi tunaobaki kuwa wafuasi wake hapa duniani na zaidi sisi ambayo ni kaka na dada zake tunaalikwa kuwa na muunganiko naye na kumshuhudia katika ulimwengu huu. Tukio hili linatupeleka mbele zaidi kuona kwamba utume wetu wa kikristo unapaswa kujikita katika Mungu tu na si katika mambo ya kidunia. Baba Yetu wa mbinguni ndiye anayepaswa kupewa kipao mbele katika yote na hivyo utume wetu kama wana Kanisa unajikita katika kumfunua Yeye kwa watu wote.

Somo letu la pili katika adhimisho hili linakazia umuhimu wa Roho Mtakatifu katika Utume wa Kanisa, yaani utume huu wa kuwa mashahidi wa huruma ya Mungu. Mtume Paulo anaanza kwa kusema: “Mungu wa Bwana wetu Yesu Kristo ... awape ninyi roho ya hekima na ya ufunuo katika kumjua yeye; macho ya mioyo yenu yatiwe nuru, mjue tumaini la mwito wake jinsi lilivyo; na utajiri wa utukufu wa urithi wake katika watakatifu ulivyo...” Roho wa Mungu ambaye katika somo la Injili anatajwa kama ahadi ya Baba ni mwongozo na mwalimu kwa wanakanisa katika kuutambua utajiri wa mbinguni ambao umefunuliwa kwetu kwa njia Bwana wetu Yesu Kristo.

Kanisa katika kuupokea utume huo linapaswa kujikita katika maongozi ya Roho Mtakatifu kusudi kufikia malengo ya utume wake wa kuwa mashahidi wa huruma ya Mungu. Kanisa linapokea utume wa Kristo ambao alikuja kuutekeleza, yaani kutangaza habari njema ya wokovu na kuustawisha ufalme wa Mungu. Mwanzoni mwa utume wake Kristo alisema: “Wakati umetimia, na ufalme wa Mungu umekaribia; tubuni, na kuiamini Injili” (Mk 1:15) lakini leo hii anapotimiza utume wake hapa duniani analiachia Kanisa kuendeleza utume huo akiamini kwamba kwa njia ya Kanisa “mataifa yote watahubiriwa kwa jina lake habari ya toba na ondoleo la dhambi”.

Kanisa zima hivi sasa lipo katika Novena ya Roho Mtakatifu kwa ajili ya kujiandaa na Sherehe ya Pentekoste. Kila mmoja wetu anaalikwa kuzama ndani kabisa ya moyo wake na kumwomba Mungu kwa dhati mapaji saba ya Roho Mtakatifu ili tunapokuwa katika utume wetu tutekeleze yote kwa ajili ya kuufunua ukuu wake kwa mataifa. Pengine mimi na wewe tumekwisha kupokea Sakramenti ya Kipaimara miaka mingi iliyopita lakini mapito ya kidunia na changamoto mbalimbali za kiroho hutufanya kufifisha uwepo wa roho huyo ndani mwetu, matendo yetu ya kila siku yanaonesha usaliti wa utume wetu wetu huo wa kuwa mashahidi wa habari njema, basi ni wakati tena wa kujiandaa kumpokea Roho Mtakatifu kusudi atuongoze vyema na hivi kweli tuwe mashahidi wa kuifunua huruma ya Mungu.

Mawasiliano ya kijamii ni moja ya njia mahususi kwa Kanisa na hususani wanakanisa katika kuutekeleza utume wao huu. Baba Mtakatifu Fransisko katika Ujumbe wake wa siku hii ya Mawasiliano ya kijamii ananukuu Bula lake aliloandika maalum kwa kutangaza mwaka huu wa Jubilei ya Huruma ya Mungu aliposema: “Mwaka huo wa Jubilei tukiuishi katika huruma uwe nafasi ya kutufanya tuweze kuwa tayari zaidi kuzungumza ili tufahamiane vizuri zaidi na kuelewana; ufute kila aina ya kiburi na udhalilishaji na uondoe kila aina ya ukatili na ubaguzi” (Rejea Uso wa Huruma namba 23).

Ujumbe huo unatupatia changamoto katika matumizi yetu leo hii ya vyombo vya mawasiliano. Tunashukuru kwamba maendeleo ya Sayansi na Teknolojia yametuletea namna nyingi na zilizo bora zaidi za mawasiliano. Njia za mawasiliano zimekuwa ni rahisi na za haraka zaidi. Mmoja anaweza kuwa bara moja lakini akapata habari kutoka bara jingine kwa wepesi na urahisi kabisa. Mawasiliano katika ujumla wake hunuia kuwaunganisha wanadamu wao kwa wao na pia kumuunganisha mwanadamu na Mungu.

Neno la Mungu katika Sherehe ya kupaa kwa Bwana Mbinguni linatuagiza kwenda kutangaza habari njema ya wokovu kwa kuwa mashahidi wa Kristo. Huu ni utume wa kuitangaza huruma ya Mungu kwa mwanadamu ambaye anaitamani kwa hamu kubwa. Tunapotafakari matumizi ya vyombo vyetu vya habari leo hii tunashuhudia usaliti mkubwa wa malengo haya. Vyombo vya habari na kwa nafasi kubwa mitandao ya kijamii kama vile Whatsap na Facebook inatumika katika kuchafua na kuiharibu haiba ya mwanadamu. Mwanadamu kwa sababu zake binafsi iwe ni za kisiasa, kiuchumi au sababu za kutafuta umaarufu binafsi hutumia vyombo hivi kubomoa na si kujenga.

Mawasiliano ya kijamii badala ya kuitangaza huruma ya Mungu ambayo inapaswa kuonekana katika kuunganisha anatangaza habari ya kuharibu na kutenganisha. Huu ni usaliti mkubwa kwa utume tunaopewa wa kwenda kutangaza habari njema na kuwa mashahidi wa Injili ya Kristo. Baba Mtakatifu anaendelea kutuasa katika ujumbe wake huo kwa siku hii maalum ya mawasiliano ya kijamii kwamba: “Maneno na matendo yetu yote yanapaswa kuielezea huruma, ukarimu na msamaha wa Mungu kwa watu wote. Upendo kwa asili yake ni mawasiliano; hutupeleka katika uwazi na kushirikiana. Kama mioyo na matendo yetu yatachagizwa na upendo wa kimungu basi mawasiliano yetu yataguswa na nguvu za Mungu mwenyewe”.

“Kisha wakarudi Yerusalemu wenye furaha kuu. Nao walikuwa daima ndani ya hekalu, wakimsifu Mungu” Hivi ndiyo walivyokuwa mitume, watangulizi wetu hawa katika imani. Mambo matatu muhimu yanajitokeza na kusakafia kabisa mawazo tuliyotafakari katika sherehe hii. Kwanza kabisa ni utambulisho wa Kanisa lenye furaha. Hawakubaki wanyonge au wakiwa kwa sababu wameahidiwa Roho Mtakatifu. Hivi ndivyo linapaswa kuonekana Kanisa letu la leo. Pamoja na kupitia katika changamoto nyingi lapaswa kubaki daima katika furaha kwa kuwa Bwana Mungu yupo nalo na analiongoza, analitia nguvu na anatembea nao. Pili tunaambiwa kuwa mitume walikuwa daima ndani ya hekalu.

Huu ni uthibitisho wa hali ya sala ambazo ni chombo mahsusi cha kuendelea kuwaunganisha na Mungu na hivyo linaingia swala la tatu ya kumsifu Mungu daima. Kanisa katika hali ya sala linajiunganisha na Mungu na daima litatafuta kufanya yaliyo mapenzi yake. Ahadi ya Kristo kwamba hatotuacha yatima ndiyo inatutia nguvu na kuendelea kuunganika na Mungu kwa njia ya sala kusudi tuutekeleze utume wetu kadiri inavyotakiwa.

Tunaalikwa leo kuutambua utume wetu na kumpatia nafasi Roho Mtakatifu, mwalimu wetu na kiongozi wetu kusudi tuutekeleze utume huo kwa jina la Yesu na kuwa kweli mashahidi wa huruma ya Mungu. Tuviombee vyombo vyetu vya habari na wadau wake ili vitekeleze utume wake kweli na kwa dhati ili viweze kuwa daraja la kuunganisha binadamu na binadamu mwenzake na katika hali ya juu kabisa limuunganishe binadamu na Mungu. Vyombo vyetu vya mawasiliano viwe kweli ushuhuda wa huruma ya Mungu kwa wanadamu.

Na Padre Josefu Peter Mosha.








All the contents on this site are copyrighted ©.