2016-05-04 13:49:00

Papa kupangusa machozi ya dhambi, machungu, sala na matumaini!


Naye Mwenyezi Mungu atafuta kila chozi katika macho yao, wala mauti haitakuwepo tena;  wala maombolezo, wala kilio, wala maumivu hayatakuwepo tena; kwa kuwa mambo ya kwanza yamekwisha pita! Hii ndiyo sehemu ya Maandiko Matakatifu inayoongoza mkesha wa sala ili “kupangusa machozi” inayotarajiwa kuongozwa na Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi, tarehe 5 Mei 2015 majira ya saa 12: 00 Jioni kwa saa za Ulaya. Itakumbukwa kwamba, hii ni Siku kuu ya Kupaa Bwana Mbinguni, ambayo inaadhimishwa mjini Vatican, kutokana na sababu za kichungaji, Sherehe hii itaadhimisha kwa kishindo, Jumapili ijayo tarehe 8 Mei 2016!

Mababa wa Kanisa katika miaka ya hivi karibuni kwa kuguswa na mahangaiko na mateso ya familia ya Mungu kutokana na sababu mbali mbali, wamekuwa wakitafakari sana kuhusu dhana ya kupangusa machozi kwa watu wa nyakati hizi wanaokumbana na: vita, majanga asilia, nyanyaso na dhuluma mbali mbali, ili kukimbilia na kuambata huruma ya Mungu isiyokuwa na mipaka. Kanisa linataka kuendelea kupangusa machozi ya watoto wa Mungu wanaokabiliwa na hali ngumu ya maisha kiasi cha kujikatia tamaa ya maisha!

Vita inaendelea kurindima sehemu mbali mbali za dunia na kuonekana kana kwamba, maovu yanashinda na kutawala. Kanisa linataka kukimbilia huruma na upendo wa Mungu unaofariji na kukomboa. Wakristo wawe na ujasiri wa kupangusa machozi ya watu wanaoteseka kutokana na sababu mbali mbali za maisha, kwa kuwajengea imani na matumaini kwa Kristo anayesikiliza na kuwasaidia kwa wakati muafaka. Katika shida na mahangaiko ya watu, Mama Kanisa anapenda kutumia dawa ya wema na huruma ya Mungu.

Mtakatifu Yohane Paulo II kunako tarehe 6 Novemba 1994 aliadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa kuyaweka wakfu Madhabahu ya Machozi ya Bikira Maria wa Siracusa! Alionesha umuhimu wa machozi yanayobubujika kutoka kwa waamini wanaotambua uzito wa dhambi wanaoubeba ndani mwao, ili kuonja huruma, upendo na msamaha wa Mungu. Kuna waamini ambao wamebanwa na machozi ya uchungu kutokana na shida na magumu wanayokabiliana nayo katika maisha, kiasi hata cha kudhani kwamba, wamesahaulika mbele ya wema na huruma ya Mungu. Ni watu ambao wameathirika kutokana na vita, dhuluma na nyanyaso za aina mbali mbali.

Ni machozi ya sala kwa Bikira Maria yanayowapatia waamini nguvu inayobubujika kutoka katika sala, wale wanaokimbilia ulinzi na tunza ya Bikira Maria; waamini wanaotaka kumwomba Mungu kupitia kwa Bikira Maria kwani wanatambua kwamba, hawana ubavu wa kusali vyema! Ni machozi ya matumaini yanayobubujika moyoni mwa waamini baada ya kukutana na Kristo Yesu, Bwana, Mwalimu na Mkombozi wa dunia; mwanga na amani ya watu, jamii na mataifa! Katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, Baba Mtakatifu Francisko anataka kwa mara nyingine tena, kupangusa machozi ya watu wa nyakati hizi ili kuwaonjesha Watu wa Mungu huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka! Unaweza kushiriki katika sala hii kwa kuwasaidia jirani zako katika shida na mahangaiko yao kama chombo na shuhuda wa huruma na upendo wa Mungu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

Unaweza kuwasiliana nasi kwa kutumia e mail ifuatayo:

engafrica@vatiradio.va

Au kuandika barua kwa anuani ifuatayo:

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican,

Vatican Radio,

Vatican city, 00120.








All the contents on this site are copyrighted ©.