2016-05-02 08:28:00

Simameni kidete kulinda na kudumisha amani duniani!


Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu kwa vikosi vya ulinzi na usalama kutoka sehemu mbali mbali za dunia imekuwa ni fursa kwa mara nyingine tena ya kukazia umuhimu wa kufunda watu katika kukuza, kudumisha na kuendeleza utamaduni wa amani, maridhiano, mshikamano na upendo! Huu kimsingi ndio unaopaswa kuwa ni dhamana na utume wa wanajeshi na askari wa vikosi vya ulinzi na usalama.

Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican wakati wa maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili tarehe 1 Mei 2016, kama sehemu ya kuhitimisha maadhimisho ya wanajeshi na askari wa vikosi vya ulinzi na usalama! Maadhimisho haya yamekwenda sanjari na kumbu kumbu ya miaka 30 tangu Waraka wa kitume wa “Huduma za Maisha ya Kiroho kwa Wanajeshi” “Spirituali Militum Curae” ulipochapishwa na Mtakatifu Yohane Paulo II.

Kardinali Parolin amekazia umuhimu wa kujenga na kudumisha amani. Ieleweke hapa amani kadiri ya Mafundisho ya Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican siyo tu kutokuwepo kwa vita, wala haiwezi kupunguzwa kuwa tendo la kudumisha uwiano kati ya nguvu zipinganazo. Tena amani si tu utawala wa mabavu, bali inaitwa kwa usahihi kazi ya haki (Isa. 32:17). Amani ndilo tunda la utaratibu uliowekwa katika jamii ya mwanadamu na Mwasisi wake; nao hauna budi kutekelezwa na wanadamu watarajiao sana haki iliyo kamili zaidi siku kwa siku. Maana mafao ya wengi yameratibiwa katika kiini chake na sheria ya milele, lakini katika mwendelezo wa muda mafao hayo hubadilika mara kwa mara kuhusu matakwa yake ya kila siku! Amani ni afya, ustawi na maendeleo endelevu, zawadi kutoka kwa Yesu Mfufuka.Wanajeshi na askari wa vikosi vya ulinzi na usalama wanapaswa kujitambua kuwa ni wahudumu wa usalama na uhuru wa mataifa. Nao, wakitekeleza wajibu wao kwa unyofu, wanachangia kweli katika kuimarisha amani.

Kardinali Parolin anakumbusha kwamba, Mtakatifu Yohane wa XXIII katika Waraka wake wa kichungaji, Pacem in Terris alikaza kusema, amani inajikita katika: ukweli, uhuru, haki na upendo. Hii ni dhamana ambayo Mwenyezi Mungu amemkabidhi binadamu kuiendeleza daima akijitahidi kuwa mwaminifu kwa mpango na Ufalme wa Mungu.

Maadhimisho haya yameandaliwa na Baraza la Kipapa kwa ajili ya Maaskofu kwa kushirikiana na Baraza la Kipapa la kuhamasisha Uinjilishaji Mpya ambalo limepewa dhamana ya kuratibu maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Itakumbukwa kwamba, Jumamosi iliyopita wanajeshi na askari hawa walikutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake mahujaji na wageni wakati huu wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu.

Katika salam zake kabla ya Ibada ya Misa takatifu Askofu mkuu Santo Marcianò wa Jimbo la Kijeshi nchini Italia kwa niaba ya Maaskofu wa Majimbo ya Kijeshi, wanajeshi, askari pamoja na familia zao, amewashukuru wadau mbali mbali waliofanikisha maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu kwa wanajeshi na askari wa vikosi vya ulinzi na usalama na kwamba, kilele chake ni maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu ambayo imeongozwa na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican.

Askofu mkuu Marcianò amekaza kusema, Jubilei ni kipindi cha furaha inayobubujika kutoka katika huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake; Mungu ambaye amewaumba, akawakomboa na anaendelea kuwategemeza katika maisha na utume wao kama wanajeshi na askari wa vikosi vya ulinzi na usalama sehemu mbali mbali za dunia. Huruma ya Mungu ina majina, sura na historia ya watu mbali mbali wanaotumwa kutekeleza dhamana na wajibu wao kati ya watu na kwenye matukio mbali mbali! Wote hawa wanapaswa kuonjeshwa huruma ya Mungu isiyokuwa ni mipaka!

Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu kiwe ni kipindi muafaka cha kusimama kidete, kulinda, kutetea na kudumisha amani, ulinzi na usalama hususan kwa maskini na wanyonge ndani ya jamii, huduma ambayo inapaswa kutolewa kwa njia ya ushuhuda wa maisha. Wanajeshi na askari wa vikosi vya ulinzi na usalama wanapaswa kuwa ni vyombo makini vitakavyozuia na hatimaye kusitisha vita, kinzani na mipasuko ya kijamii; wawe mstari wa mbele kulinda na kutetea Injili ya maisha; kwa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa haki na amani duniani.

Kanisa limewashukuru na kuwakumbuka wanajeshi na askari wote waliopoteza maisha yao wakiwa katika shughuli za ulinzi na usalama kwa raia na mali zao. Kanisa pia limewaombea wanafamilia wa wanajeshi na askari! Baba Mtakatifu Francisko anawataka wanajeshi na askari wa vikosi vya ulinzi na usalama kuwa ni mashuhuda wa matumaini ya Kikristo na uhakika wa ushindi wa upendo dhidi ya chuki na uhasama; amani dhidi ya vita, kinzani na mipasuko ya kijamii.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

Unaweza kuwasiliana nasi kwa kutumia e mail ifuatayo:

engafrica@vatiradio.va

Au kuandika barua kwa anuani ifuatayo:

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican,

Vatican Radio,

Vatican city, 00120.

 








All the contents on this site are copyrighted ©.