2016-05-02 08:59:00

Pasaka ya Bwana iwe ni sherehe inayomwilisha upendo kwa jirani!


Bwana amefufuka kweli kweli, tufurahi na kushangilia kwani hii ndiyo sherehe kubwa na kiini cha ukombozi wa mwanadamu, kiini cha imani, matumaini na Habari Njema ya Wokovu inayotangazwa na Mama Kanisa kwa nyakati hizi. Kristo mfufuka anaonesha ushindi dhidi ya dhambi na mauti yaliyosababishwa na kiburi cha Adamu na Hawa na matokeo yake: dhambi, mateso, rushwa na kifo vikaingia duniani. Dhambi ikawafukia watu kutoka mbele ya uso wa Mungu mwingi wa huruma na mapendo!

Yesu Kristo kwa njia ya Fumbo la Umwilisho linalopata utimilifu wake kwenye Fumbo la Pasaka, akaonesha ile nguvu ya Mungu inayookoa. Kumbe, Fumbo la Ufufuko wa Kristo Yesu ni msingi thabiti wa maisha ya uzima wa milele na daraja na muungano kati ya binadamu na Mwenyezi Mungu. Sherehe ya Pasaka ni kielelezo makini cha ushindi wa upendo wa Mungu, aliyeipenda dunia hata akamtoa Mwanaye wa pekee, ili kila anaye mwamini, asipotee, bali awe na uzima wa milele.

Huu ni muhtasari wa Ujumbe wa Pasaka kutoka kwa Patriaki Kirill wa Moscow na Russia nzima, wakati huu Makanisa ya Mashariki yanapoadhimisha Pasaka ya Bwana. Lakini anasikitika kusema kwamba, waamini wanaadhimisha kwa shangwe na furaha Fumbo la Pasaka, lakini, bado kuna mateso na mahangaiko makubwa kwa watu sehemu mbali mbali za dunia; kuna chuki, uhasama na hali ya kutaka kulipizana kisasi. Utamaduni wa kifo unaendelea kuwaandama watu, kiasi hata cha kukosa matumaini kwa leo na kesho iliyo bora zaidi.

Patriaki Kirill anakaza kusema, Fumbo la Pasaka, haliondoi ukweli wa mambo duniani, lakini unapata mwelekeo mpya unaojikita katika matumaini yanayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu aliyefufuka kwa wafu. Kifo kadiri ya mafundisho ya Kanisa ni daraja la kukutana na Muumba, ili kusherekea maisha ya uzima wa milele. Kristo Mfufuka ameshinda dhambi na mauti, changamoto na mwaliko kwa Wakristo kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Mshikamano wa upendo ni fadhila muhimu sana katika maisha ya Kikristo, kwani yote yanapita lakini upendo unadumu milele. Upendo mkamilifu ni ule unaofumbatwa katika huduma kwa maskini na adui na hivyo unakuwa ni chemchemi ya neema na baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu, unaomwezesha mwamini kushinda ubaya kwa kutenda wema. Huu ndio upendo uliofundishwa na kushuhudiwa na Yesu kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko kutoka kwa wafu!

Wema na upendo vinaonesha nguvu ya Mungu, mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema anasema Patriaki Kirill kuikimbia dhambi kwa kujikita katika maisha ya sala, toba na wongofu wa ndani; lakini zaidi kwa kushiriki kikamilifu Mwili na Damu Azizi ya Kristo Yesu. Maadhimisho ya Fumbo la Pasaka iwe ni fursa ya kumshangilia Kristo aliyeshinda dhambi na mauti na hivyo kumkirimia mwanadamu maisha ya uzima wa milele. Wakristo wanapaswa kushuhudia kiini hiki cha imani kwa njia ya upendo kwa Mungu na jirani zao! Na kwa maneno haya, Patriaki Kirill wa Moscow na Russia nzima anahitimisha Ujumbe wake wa Pasaka kwa mwaka 2016.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.