2016-05-02 12:03:00

Liberia: Injili ya familia, uhuru wa kidini, kodi na vyama vya kisiasa!


Baraza la Maaskofu Katoliki Liberia, CABICOL, hivi karibuni limehitimisha mkutano wake wa mwanzo wa mwaka ambao umejadili pamoja na mambo mengine kuhusu mchakato wa Uinjilishaji wa kina, huduma katika sekta ya afya, elimu na masuala jamii; wamegusia haki na amani pamoja na dhamana ya vyombo vya mawasiliano ya jamii katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia. Kwa namna ya pekee, Maaskofu wa Liberia wamechambua kwa kina na mapana maisha na utume wa familia; uhuru wa kidini, kodi pamoja na masuala ya vyama vya kisiasa nchini humo!

Itakumbukwa kwamba, mkutano huu ulikuwa unaongozwa nakauli mbiu “Umuhimu wa Kanisa nchini Liberia kwa nyakati hizi: Uinjilishaji, afya, elimu, masuala ya kijamii, haki na amani pamoja na vyombo vya mawasiliano” Kanisa linatambua dhamana na wajibu wake wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, changamoto na mwaliko wa pekee kabisa kwa Familia ya Mungu nchini Liberia kuhakikisha kwamba, wanatekeleza dhamana hii kwa ukamilifu zaidi sanjari na kukazia majiundo ya awali na endelevu Seminarini na katika nyumba za malezi ya maisha ya kitawa na kazi za kitume.

Katekesi makini ziwasaidie waamini walei kuwa ni mashuhuda na vyombo vya Uinjilishaji kwa njia ya mfano bora wa maisha, wenye mvuto na mashiko kwa wale wanao wazunguka! Maaskofu wanayashukuru Mashirika ya kitawa na kazi za kitume yanayochapa kazi bila kuchoka nchini Liberia. Maaskofu wanawashukuru na kuwapongeza wafanyakazi katika sekta ya afya waliojisadaka kuwahudumia wagonjwa wa Ebola bila kujibakiza kiasi hata cha kuhatarisha maisha yao na wengine wengi kupoteza maisha yao.

Maaskofu wanawataka wananchi wa Liberia kuendelea kuzingatia sheria na kanuni za mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ebola sanjari na wadau mbali mbali kuendelea kufanya maboresho katika sekta ya afya. Kanuni maadili, sheria na miiko ya kazi ya wahudumu wa afya izingatiwe kwa ajili ya ustawi na mafao ya wengi. Baraza la Maaskofu Katoliki Liberia limeanzisha Baraza la Afya la Kanisa Katoliki Kitaifa, ambalo limepewa dhamana ya kuratibu, kusimamia na kuendesha shughuli mbali mbali zinazojitokeza katika sekta ya afya, ili kutoa huduma bora zaidi pasi na upendeleo!

Baraza la maaskofu Katoliki Liberia linatambua na kuthamini umuhimu wa elimu katika maisha ya binadamu na athari zake, kama ambavyo dhana hii inafafanuliwa vyema na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican katika tamko lao kuhusu Umuhimu wa Elimu ya Kikristo “Gravissimum Educationis”. Malezi na majiundo kwa vijana wa kizazi kipya ni mambo yanayopaswa kupewa kipaumbele cha pekee. Maaskofu wanakaza kusema, kuna haja ya kuendeleza mchakato wa maboresho ya elimu nchini humo.

Maaskofu wanawapongeza wafanyakazi wa Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki kwa huduma bora wanayoendelea kutoa kwa familia ya Mungu nchini humo na kwamba, huduma ya upendo ni utimilifu wa sheria zote ndani ya Kanisa. Waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema hawana budi kuendelea kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha tunu msingi za maisha ya binadamu, utu na haki zake msingi. Ni wajibu wa Kanisa kukema utovu wa nidhamu na mmonyoko wa maadili na utu wema, tayari kusaidia ujenzi na malezi ya dhamiri nyofu. Kanisa linatambua kwamba furaha na matumaini, uchungu na fadhaa ya binadamu hasa maskini ni furaha na matumaini, machungu na fadhaa ya Wafuasi wa Kristo.

Baraza la maaskofu Katoliki Liberia linawapongeza wadau mbali mbali katika sekta ya mawasiliano ya jamii kwa kazi kubwa wanayoitekeleza katika tasnia ya habari na mawasiliano ya jamii, changamoto ya kuwajibika zaidi, ili kwamba, uhuru wa kujieleza hauvunji heshima, maadili na utu wema. Maaskofu wanaendelea kukazia umuhimu wa kudumisha maisha na utume wa familia inayoundwa kati ya bwana na bibi kadiri ya mpango wa Mungu katika maisha ya binadamu. Familia iwe ni chachu ya haki, amani, upendo na mshikamano wa dhati dhidi ya utamaduni wa kifo kama kigezo cha kupata misaada ya maendeleo.

Kanisa linatambua fursa, shida, mahangaiko na changamoto zinazoendelea kuikumba familia kama anavyoelezea kwa kina Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wake wa kitume, Furaha ya upendo ndani ya familia, “Amoris laetitia”. Kanisa litaendelea kuonesha huruma, upendo na mshikamano na familia, ili ziweze kuwa kweli ni vyombo vya huruma na upendo; na mashuhuda wa Injili ya familia na maisha ya binadamu.

Baraza la Maaskofu Katoliki Liberia linaendelea kukazia umuhimu wa kukuza na kudumisha uhuru wa kidini; kwa kutambua tofauti zinazoweza kujitokeza, lakini kwa kuthamini utajiri mkubwa unaofumbatwa katika tofauti za kidini kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi. Kanisa litaendeleza mchakato wa majadiliano ya kidini na kiekumene ili kudumisha misingi ya haki, amani, ustawi na mafao ya wengi! Wananchi wanahamasishwa kulipa kodi kwa ajili ya maendeleo ya nchi, lakini Serikali nayo inapaswa kuondoa ukiritimba na urasimu katika huduma kwa jamii na kwamba, vyama vya kisiasa nchini humo viwe mstari wa mbele kukuza na kudumisha demokrasia, utawala bora, sheria pamoja na haki msingi za binadamu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.