2016-04-30 10:26:00

Askari ni wahudumu wa: amani, usalama na upatanisho wa kijamii!


Hata mtu akiwa ndani ya Kristo amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita! Tazama yamekuwa mapya. Lakini vyote pia vyatokana na Mungu aliyetupatanisha sisi na nafsi yake kwa Kristo, naye alitupa huduma ya upatanisho; yaani Mungu alikuwa ndani ya Kristo, akiupatanisha ulimwengu na nafsi yake, asiwahesabie makosa yao; naye ametia ndani yetu neno la upatanisho. Waamini ni wajumbe wa Kristo katika mchakato wa upatanisho na kwamba, wanapaswa pia kujipatanisha na Kristo katika maisha yao. Yeye asiyejua dhambi alimfanya kuwa dhambi kwa ajili ya binadamu, ili wapate kuwa haki ya Mungu katika Yeye!

Huruma na upatanisho ndicho kiini cha Katekesi ya Maadhimisho ya Jubilei ya huruma ya Mungu iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi, tarehe 30 Aprili 2016 kwa mahujaji na wageni waliokuwa wamefurika kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Mwenyezi Mungu anamkirimia daima mwanadamu fursa za msamaha, mwaliko kwa mwamini kukimbilia tena na tena huruma ya Mungu kwa kuambata neema inayotolewa na Mwenyezi Mungu.

Kutokana na huruma na upendo wake mkuu, Mwenyezi Mungu amemtoa Mwanaye wa Pekee, Yesu Kristo aliyeteswa na kufa Msalabani na Msalaba huo, ukawa ni daraja linalomuunganisha mwanadamu na Mwenyezi Mungu. Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu iwe ni fursa kwa kila mwamini kupokea kwa moyo mkunjufu mwaliko wa kujipatanisha na Mungu, kujipatanisha katika Jumuiya pamoja na kusaidia mchakato wa ujenzi wa umoja na upatanisho kati ya watu wa mataifa. Baba Mtakatifu anakaza kusema, kwa kujipatanisha na Mungu pamoja na jirani, mwamini anaonja uponyaji, utulivu na amani ya ndani, huku akiendelea kuchangamotishwa na Mungu ili naye aweze kuwa ni chombo na shuhuda wa upatanisho kwa ngazi mbali mbali ndani ya jamii, ili hatimaye kujenga na kudumisha utandawazi wa amani, haki na mshikamano.

Kwa namna ya pekee kabisa, Baba Mtakatifu Francisko ametambua uwepo wa askari wa vikosi vya ulinzi na usalama kutoka sehemu mbali mbali za dunia, waliongia kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro kwa maandamano makubwa huku wakiongozwa na Bendi za Muziki. Askari hawa wamekumbushwa kwamba, kazi yao kimsingi ni huduma ya amani, usalama na upatanisho wa kijamii.

Baba Mtakatifu amewatia shime askari hawa kwa kuwataka kamwe wasikate tamaa wanapokumbana na matatizo na changamoto katika maisha na utume wao; bali wajitahidi kukua na kukomaa katika imani na matumaini kwa msaada wa upendo wa Mungu. Kwa njia hii, Askari hawa watakuwa ni alama ya matumaini ya Kikristo kwa kutambua kwamba, upendo unashinda maovu na amani inatawala dhidi ya uhalifu na vita! Askari wawe mashuhuda na vyombo vya upatanisho; wajenzi na watunzaji wa amani.

Katika katekesi hii, Baba Mtakatifu ametambua uwepo wa Askari wa vikosi vya ulinzi na usalama kutoka Kenya na amewatakia wote upendo na huruma ya Mungu kwa familia, ndugu na jamaa zao. Amewataka waamini kujenga familia bora, Kanisa dogo la nyumbani, mahali ambamo mtu anaonja: upendo, ukarimu na msamaha wa Mungu.

Baba Mtakatifu amewataka mahujaji kutoka Mashariki ya Kati kujipatanisha na kuambata msamaha wa Mungu, ili kushinda dhambi, kwani Mwenyezi Mungu, kwa huruma na upendo wake, anamwinua mtu aliyeteleza na kuanguka katika dhambi. Lakini ni wajibu wa mwamini binafsi kutambua kwamba, kweli anahitaji huruma ya Mungu na hapo Mwenyezi Mungu ataweza kumkirimia chemchemi ya furaha ya maisha mapya! Waamini waendelee kuwa ni mashuhuda wa tunu msingi za maisha ya Kikristo kwa kuonesha ukarimu kwa maskini na watu wenye shida zaidi. Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko amewaweka waamini na mahujaji wote chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

Unaweza kuwasiliana nasi kwa kutumia e mail ifuatayo:

engafrica@vatiradio.va

Au kuandika barua kwa anuani ifuatayo:

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican,

Vatican Radio,

Vatican city, 00120.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.