2016-04-29 07:43:00

Uwajibijaki bora zaidi katika kilimo na madini, ili kutunza mazingira!


Baraza la Maaskofu Katoliki Zambia katika tamko lao baada ya kuhitimisha mkutano wa siku mbili uliokuwa unaongozwa na kauli mbiu “Utunzaji wa nyumba ya wote katika mtazamo mpana wa uwekezaji katika sekta ya uchimbaji wa madini na kilimo” wanasema wanamshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa Waraka wake wa kitume “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote; waraka unaofumbata utajiri mkubwa wa maisha ya kiroho na kijamii. Wametiwa moyo kwa kuwepo wa Kardinali Peter Turkson, Rais wa Baraza la Kipapa la haki na amani aliyetoa hotuba elekezi katika mkutano huu pamoja na uwepo wa viongozi wa Kanisa, Serikali na Jamii katika ujumla wao.

 

Maaskofu wanaguswa kwa namna ya pekee na uharibifu wa mazingira unaoendelea kufanywa katika sekta ya uchimbaji wa madini nchini Zambia, kazi inayofanywa na makampuni makubwa na kwamba, ujumbe ambao Kardinali Turkson amewashiriki katika hotuba yake elekezi wataifanyia kazi! Maaskofu wanakaza kusema, Waraka wa Baba Mtakatifu Francisko, Laudato si ni dira na mwongozo thabiti katika kukabiliana na uharibifu wa mazingira nyumba ya wote, changamoto ya kujenga na kudumisha majadiliano ya kina katika ukweli na uwazi, ustawi na maendeleo ya wengi ili kupata suluhu ya kudumu, katika mchakato wa kukabiliana na changamoto zinazotokana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Maaskofu wametiwa moyo na ushiriki wa umati mkubwa wa wadau kutoka katika sekta ya kilim ona uchimbaji wa madini walionesha umuhimu wa kulinda na kutunza mazingira, kwani licha ya sekta ya kilimo na madini kuchangia kwa asilimia kubwa ukuaji wa uchumi nchini Zambia, lakini kuna haja ya kuwa na busara katika uchimbaji wa madini na matumizi ya ardhi kwa ajili ya sekta ya kilimo, ili kweli kilimo kiweze kuwa ni endelevu zaidi, tayari kupambana na umaskini na kusaidia mchakato wa ustawi na maendeleo ya wengi.

Baraza la Maaskofu Katoliki Zambia linasema, changamoto zinazotolewa na Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa kitume, Laudato si, zilizofafanuliwa kwa kina na mapana na Kardinali Peter Turkson zinapaswa kufanyiwa kazi na familia ya Mungu nchini Zambia, ili kuwa na mwelekeo mpya na mpana zaidi kuhusu utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote mintarafu mazingira ya kiuchumi, kisiasa na kijamii.

Washiriki wa mkutano huu pamoja na mambo mengine, wanasema wanapenda kuonesha mshikamano wa umoja na upendo na maskini na waathirika wote wa mabadiliko ya tabianchi na uchimbaji mkubwa wa madini. Wanapenda kushikamana nao katika kuwapatia habari makini na majiundo endelevu ili kuwajengea uwezo wa kukabiliana vyema na changamoto za athari za mabadiliko ya tabianchi na uchimbaji mkubwa wa madini. Wajumbe wanatambua mchango mkubwa unaotolewa na sekta ya madini kwa uchumi, ustawi na maendeleo ya Zambia. Wanasema, umefika wakati wa kusimama kidete kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote pamoja na kuboresha maeneo ambayo kwa miaka mingi yalitumiwa katika uchimbaji wa madini, ili yaweze kutumiwa tena kwa shughuli nyingine! Ukweli, uwazi na uwajibikaji uweni utamaduni kwa wawezekezaji, serikali na viongozi wa jadi na kwamba, wananchi wapewe habari za uhakika kuhusu maendeleo na usalama wa maisha yao sanjari na kudumisha majadiliano na wadau wakuu!

Wajumbe wanasema, Baraza la Maaskofu Katoliki Zambia litaendeleza mchakato wa uragibishaji wa kilimo bora na endelevu kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wananchi wa Zambia; kwa kulinda na kutunza mazingira; kwa kushiriki kuzalisha na kumiliki mashamba ya kilimo. Kuhusu na mambo mtambuka, Maaskofu wanasema, kuna haja kwa Serikali ya Zambia kuibua sera na mbinu mkakati wa utunzaji bora wa mazingira; kusimama kidete kwa ajili ya mafao ya wengi katika shughuli za uwezekaji katika sekta ya kilimo na madini. Ziwepo sera zinazoratibisha vyema zaidi shughuli za uchimbiaji wa madini, wanyama pori, kilimo, maji na ardhi. Mwishoni, wajumbe wanasema, watasimama kidete kutekeleza kwa vitendo ushauri unaofumbatwa katika Waraka wa Kitume, Laudato si, kwa kuona kwamba, mafao ya wengi yanafundishwa shuleni.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.