2016-04-29 15:23:00

Lindeni na kutetea uhuru wa kuabudu ili kudumisha amani!


Askofu mkuu Bernardito Auza, mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Umoja wa Mataifa, Alhamisi tarehe 28 Aprili 2016 kwa kushirikiana na wadau mbali mbali ameandaa kongamano lililokuwa linaongozwa na kauli mbiu “Kulinda uhuru wa kidini na haki msingi za binadamu: Sitisha mauaji ya kimbari dhidi ya Wakristo na waamini wa dini nyingine. Lengo la kongamano hili ni kuwatetea Wakristo ambao wamekuwa ni wahanga wa vita, nyanyaso na dhuluma sehemu mbali mbali za dunia.

Wajumbe katika kongamano hili wamejadili kwa kina na mapana dhamana ya kuwalinda, kuwatetea na kuwaendeleza Wakristo wanaoteseka na kunyanyasika sehemu mbali mbali za dunia kutokana na misimamo mikali ya kiimani na kidini, ili hatimaye, Jamii iweze kusimama kidete kulinda na kutetea uhuru wa kuabudu. Wajumbe wamesikiliza shuhuda mbali mbali zilizotolewa na Wakristo kutoka katika maeneo yenye vita inajikita katika misimamo mikali ya kidini kama vile Syria, Iraq na Nigeria ambayo imegeuka kuwa ni uwanja wa mauaji na nyanyaso zinazofanywa na Kikundi cha kigaidi cha Boko Haram.

Sehemu ya tatu ya kongamano hili imejikita katika mateso na mahangaiko ya wanawake waliobakwa na kunyanyaswa kijinsia katika maeneo ya Mashariki ya Kati. Kongamano hili limehudhuriwa na wawakilishi wa kudumu wa Nchi za Jumuiya ya Kiislam kwenye Umoja wa Mataifa, viongozi wa Kanisa kutoka Nigeria; Mapadre na baadhi ya watawa wanaofanya utume wao kwenye mazingira magumu  na hatarishi nchini Syria na Iraq.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.